loader
Picha

Usafiri mwendokasi vurugu tupu

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam uliotegemewa kuwa mkombozi kwa wananchi, sasa umegeuka majanga. Hatua hiyo inatokana na mradi huo kugubikwa na matukio yanayoashiria kusuasua kwa uendeshaji wake na kuathiri ufanisi.

Katika hatua inayotishia usalama wa utoaji wa huduma hiyo, jana abiria waliokuwa katika kituo cha mabasi hayo, eneo la Kimara Korogwe walikosa uvumilivu na kushuka kutoka ndani ya kituo na kusimama barabarani kwa zaidi ya saa moja kuzuia mabasi hayo kupita.

Abiria hao walichukua hatua hiyo baada ya kusimama kituoni kwa zaidi ya saa mbili wakisubiria huduma hiyo, huku mabasi hayo yakipita kituoni hapo bila kusimama.

Kutokana na uchache wa mabasi yaliyokuwa yanatoa huduma, madereva walikuwa wakipakia abiria katika kituo cha Kimara Mwisho na walipokuwa wanafika Kituo cha Korogwe hawakusimama, jambo lililosababisha kituo hicho kufurika abiria.

Baadhi ya abiria waliwasiliana na namba za huduma kwa mteja za Kampuni inayoendesha Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) ili kuomba msaada, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda ndipo walipoamua kuingia barabarani na kusimama ili kuzuia mabasi hayo kutokupita kuelekea Kimara Mwisho.

Hatua hiyo ya abiria hao kusimama barabarani ililazimu mabasi zaidi ya manane kufika eneo hilo, lakini madereva wakigoma kufungua milango, jambo lililosababisha askari kuingilia kati kuwatoa abiria waliokuwa barabarani na kuruhusu mabasi hayo kuelekea kituo cha Kimara Mwisho bila kusimama kupakia abiria Katika kituo cha Korogwe.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akienda eneo la Posta, Nakeso Abiud alisema licha ya uharaka wa kufika lakini kwa ujumla usafiri huo umekuwa ni mateso makubwa kwani wakazi wa eneo hilo hawana mbadala.

Alisema alifika kituoni hapo tangu saa 12: 54 asubuhi lakini akijikuta akiondoka hapo saa 3:03 asubuhi, jambo ambalo linakuwa si la haraka tena bali ni mateso ya kusimama ndani ya kituo kwa muda wote.

Abiria mwingine Alfred Hans alihoji uwepo wa mabasi machache lakini huduma ya kukatisha tiketi ikiendelea katika vituo.

Kutokana na hatua hiyo iliyoambatana na zomeazomea kwa askari, abiria wengi waliingia kituoni humo bila kulipa nauli kutokana na maofisa wa Udart kushindwa kusimamia umati wa watu waliokuwepo eneo hilo.

Makonda awaka Kutokana na sakata hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameingilia kati kwa kuagiza wasimamizi wote wa mradi huo kukutana naye leo asubuhi katika kituo cha Kimara Mwisho.

Makonda alitoa agizo hilo saa chache baada ya kuzagaa kwa picha kwenye mitandao ya kijamii zikionesha abiria wakigombea moja ya basi la mwendokasi katika kituo cha Kimara huku wengine wakipitia dirishani kutokana na uchache wa mabasi hayo jana.

Akizungumza jana Makonda alisema; “Sifurahishwi na namna mradi wa mwendokasi unavyoendeshwa kwani matarajio ya Rais (John Magufuli) ni kuona changamoto za muda mrefu ya usafiri kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam ukigeuzwa historia kupitia mradi huu.

“Kwa sababu hiyo basi naagiza watendaji wote wanaosimamia mwendokasi nikutane nao kesho (leo) saa 12:30 asubuhi wanieleze kwa nini hakuna hatua madhubuti walizochukua huku wakishuhudia kero kubwa wananchi wanaopitia.

“Nitumie fursa hii kuwaomba radhi wananchi kwa kero hii na niwaahidi kuwa jambo hili litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni, tukutane kesho mapema mwendokasi Kimara,” alisisitiza.

Kusuasua kwa huduma za Udart Kauli ya Makonda imekuja ikiwa ni siku chache baada ya mvutano mkubwa uliodumu kwa miezi saba sasa baina ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na Kampuni ya Udart na kusababisha mabasi 70 mapya kukwama katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ikielezwa kuwa ni kutokana na mabasi hayo kutolipiwa kodi.

Mradi huo wa mabasi yaendayo haraka ulianza Mei, 2016 ukiwa na mabasi 140. Kati ya mabasi hayo, 39 ni makubwa yenye urefu wa mita 18 na uwezo wa kubeba abiria 155, na mengine 101 ni ya urefu wa mita 12 na uwezo wa kubeba abiria 90.

Msemaji wa Kampuni ya Udart, Deus Bugaywa alikaririwa akisema kuwa usafiri huo umegeuka shubiri, kwani, wizi uliokuwapo enzi za mabasi ya Uda pekee umerejea, msongamano ndani ya mabasi umerejea, uhakika wa usafiri si mkubwa.

“Watu hawaoni tofauti ya usafiri wa daladala na mwendokasi,” alikaririwa Bugaywa akizungumza kuhusu mabasi 70 yaliyozuiwa kutoka bandarini kusubiri kibali cha Dart.

“Mabasi (yaliyopo) yanaharibika mara kwa mara kwa kuwa yanabeba abiria kupita uwezo wake.”

Kwa mujibu wa Udart, mradi huo ulianza na mabasi 140 na ulikuwa ukihudumia abiria 50,000 lakini ongezeko la watu jijini Dar es Salaam limesababisha abiria kuongezeka hadi kufikia kati ya 150,000 na 200,000 ambao wanahudumiwa na idadi ileile ya mabasi.

Ofisa Habari wa Dart, William Gatambi amesema kuwa wakala huyo akiwa msimamizi wa mradi huo hawawezi kupokea bidhaa ambayo haijalipiwa kodi.

Alidai kuwa Udart wanajua hawajalipa kodi, lakini wanajaribu kutafuta huruma ya wananchi ili Dart waonekane kikwazo.

“TRA na Dart zote ni ofisi za Serikali, hatuwezi kuwa chanzo cha kuisababishia serikali hasara ya kukosa kodi yake, kisa tuna uhaba wa mabasi. Udart wafuate taratibu zote sisi mbona hatuna shida,” amesema Gatambi.

Akijibu madai hayo Bugaywa wa Udart amesema: “Masuala ya kodi yanashughulikiwa na mamlaka nyingine na wala hayahusiani na utoaji kibali. Wao (Dart) wanachotakiwa ni kuangalia kama mabasi hayo yamekidhi vigezo kulingana na mkataba.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema kodi inayodaiwa katika mabasi hayo ni ya forodha na endapo italipwa yataachiwa.

Kayombo hakuwa tayari kutaja kiwango cha fedha kinachodaiwa kwa maelezo kuwa hayo ni masuala ya ndani kati yao na mteja.

Alifafanua kuwa sheria zinataka bidhaa ikiagizwa ilipiwe kodi ndani ya siku 60 tangu imefika bandarini na ikishindikana basi taratibu nyingine za kisheria zinafuatwa.

Tiketi kero nyingine mwendokasi Changamoto nyingine ambayo inaikabili mradi huo wa mwendokasi ni tiketi ambazo zimekuwa kero kubwa kwa abiria ambao wamejikuta wanauziwa tiketi bandia.

Zaidi ya miezi mitano sasa mfumo wa kuscan tiketi na kadi ambao ulikuwa unatoa idadi kamili ya makusanyo yaliyopatikana hazifanyi kazi na tiketi zimekuwa zikitolewa kwa njia ya ‘manual’ kitendo ambacho kimeshusha makusanyo kutoka kati ya Sh milioni 20 na Sh milioni 25 kwa siku hadi kufikia Sh milioni 10.

Uchunguzi wa habari leo umebaini kuwa baadhi ya maofisa wameweza kughushi tiketi na kuwauzia watu wazima tiketi ya wanafunzi, huku wale wanaopanda njiani kuanzia Kituo cha Kibanda cha Mkaa mpaka Stop Over wanapewa tiketi ya Sh 400 ambapo dereva haichani anazinyoosha vizuri na baadaye zinauzwa tena kwa kuwa mashine za kuscan tiketi kwenye vituo vya Mbezi zimeondolewa kabisa.

Hivi karibuni wakusanya fedha zaidi ya 50 kituo cha mabasi hayo kituo cha Kimara na Gerezani waliripotiwa kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kutoa tiketi feki kwa abiria.

Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi ya Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikiingia katika mifuko ya wajanja.

Sumatra watema cheche Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema imeanza kushughulikia tatizo la msongamano wa abiria kwenye mabasi hayo ya mwendokasi.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, aliliambia HabariLeo kuwa, wameshakutana na Udart na kuzungumza nao kuhusu tatizo la msongamano wa abiria kwenye mabasi yao.

Kahatano alisema katika kikao chao na Udart, Septemba 27, mwaka huu, walikubaliana kuchukua hatua kadhaa ili kudhibiti tatizo.

Kwa mujibu wa Kahatano, moja ya hatua ambayo Sumatra wameichukua ni kuiagiza Udart kubadilisha muda wa mabasi yake kuanza kazi.

Alisema badala ya mabasi hayo kuanza kazi saa 11 alfajiri, wamewaagiza yaanze kazi saa 10 alfajiri.

Alisema kutokana na mabadiliko hayo, wamewataka Udart kutoa matangazo kwenye mabasi yao na kuyabandika matangazo hayo kwenye vituo vya mabasi hayo ili wananchi wajue mabadiliko hayo.

Alisema kuwa uwezo wa mabasi hayo ni kubeba abiria 160 kwa mabasi makubwa na mabasi madogo yana uwezo wa kubeba abiria 80; alisema kwa sasa Udart wana jumla ya mabasi 140.

Alisema kuwa Sumatra pia imelielekeza Jeshi la Polisi kuyakagua mabasi hayo mara kwa mara ili kuhakikisha yako salama pamoja na kufuatilia mwendokasi kwa usalama wa abiria.

Aidha, Kahatano alisema sababu iliyotolewa na Udart kuhusu msongamano wa abiria kwenye magari yao ni kutokana na polisi wa usalama barabarani kuyasimamisha mabasi hayo kwenye makutano ya barabara kwa muda mrefu.

Alisema Udart wanaona kitendo hicho kinachangia msongamano kwa kuwa kinaathiri mzunguko wa kawaida wa mabasi hayo, hivyo kusababisha msongamano wa watu kwenye vituo hali inayosababisha pia msongamano kwenye mabasi hayo.

Katika kuhakikisha tatizo la msongamano kwenye mabasi hayo linadhibitiwa, Kahatano alisema kuwa mipango ya baadaye ya Sumatra ni kuyaunganisha mabasi hayo kwenye Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Mabasi nchini (VTS).

Mpango mwingine wa baadaye wa Sumatra ni kuona kama kutakuwa na haja ya abiria kupanda mabasi hayo kwa foleni ili kudhibiti msongamano.

Imeandikwa na Lucy Lyatuu, Vicky Kimaro na Matern Kayera, Dar.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi