loader
Picha

Bodi soko la Feri kutumbuliwa kwa ubadhirifu

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza kuvunjwa kwa Bodi ya Soko la Samaki Feri, Dar es Salaam, akieleza kuwa licha ya kutochaguliwa kihalali, wajumbe wamekuwa wakijiidhinishia malipo ya posho ya mamilioni ya fedha.

Amesema Kamati aliyoiunda Septemba, mwaka huu imebaini Bodi hiyo iliyoundwa mwaka 2015 na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imejitengea malipo ya kiinua mgongo cha Sh milioni 20 kila mjumbe, jumla yao wakiwa tisa hivyo zilitengwa jumla ya Sh milioni 180 kwa ajili yao.

Waziri Mpina aliyetoa maagizo hayo kwa viongozi wa Manispaa ya Ilala, pia aliyakataa matumizi ya Sh milioni 50.4 zilizoidhinishwa na Bodi hiyo kama malipo ya posho za vikao na aliagiza matumizi hayo yaondolewe kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019.

“Haiwezekani ukaenda kuilipa Bodi Sh milioni 54 katika soko ambalo hata choo tumeshindwa kuchimba,” alisema akiwa sokoni hapo. Alisema, gharama za uendeshaji Soko la Samaki la Feri hazilingani na hali halisi hivyo mikataba itapitiwa upya.

Aliagiza mikataba yote kwenye soko hilo ipitiwe upya na kama kuna matumizi mabaya ya fedha hatua zichukuliwe. Alisema, matumizi kwenye soko hilo lazima yahakikiwe kuona uhalisia wake.

Alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ahakikishe matundu 24 ya vyoo vya kisasa yanachimbwa kuanzia leo kwenye soko hilo na hadi ifikapo Juni 30, mwakani, miundombinu yote kwenye eneo hilo iwe imekarabatiwa. Miongoni mwa maeneo yatakayokarabatiwa ni eneo la kukaushia samaki, eneo la wajasiriamali na jokofu la kuhifadhia samaki.

Mpina alisema, hataki kusikia masuala ya mchakato, anataka kazi ya kuchimba vyoo ifanywe haraka, na kwamba, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Uvuvi na Mhandisi wa Wizara watajua watakapopata michoro ya vyoo hivyo.

Awali Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Komakoma akisoma taarifa ya mambo kadhaa waliyobaini katika uchunguzi wao kwenye soko hilo, alibainisha kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa majukumu kati ya Menejimenti ya Soko na Bodi ya usimamizi wa soko, ambapo sehemu kubwa majukumu ya Menejimenti yanaonekana kuwa ndiyo majukumu ya Bodi.

Alibainisha kuwa Kamati inaona haiwezekani halmashauri ambaye ndiye mmiliki wa soko awe chanzo cha mapato ambapo fedha yote inayokusanywa inatumika hapo hapo bila chanzo kupewa gawio hata kidogo.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa mengine waliyobaini ni pamoja na mfumo wa maji taka ya vyooni kuelemewa kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watumiaji wa mfumo huo kutoka watu 2,000 kwa siku hadi 15,000.

Alisema pia eneo la feri linalotumika kushushia samaki na mazao ya bahari limejaa mchanga hivyo kusababisha mazao hayo kushushwa mbali hatua ambayo imechangia uharibifu wa mazingira na usumbufu kwa wafanyabiashara.

Msemaji wa Chama cha Wavuvi Wadogo Wadogo(Chawawani), Faki Mbaruku akizungumza kwa niaba ya wavuvi alipongeza hatua ya Waziri kuagiza kuvunjwa kwa Bodi hiyo, lakini akashauri kuwa uongozi wote wa soko hilo ungefumuliwa.

“Hilo ndilo wavuvi wengi tunalolitamani ungefumua uongozi wote tuanze upya, hatuoni manufaa yao kwetu,” alisema Faki. Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliiagiza Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam impe haraka taarifa ya mapato na matumizi ya Soko la Samaki la Feri.

Rais Magufuli alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na Manispaa ya Ilala washughulikie kero za wavuvi na wajasiriamali katika eneo hilo ukiwemo ushuru na vyoo. Alitoa maagizo hayo kupitia kwa Katibu wake, Ngusa Samike wakati akikabidhi Sh milioni 20 kwa Umoja wa Wavuvi Wadogo Kigamboni (UWAWAKI).

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Beatrice Moses, Tudarco

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi