loader
Picha

Benki ya Dunia kuwekeza kwenye sayansi, teknolojia

BENKI ya Dunia imeahidi kuwekeza zaidi nchini katika sayansi na teknolojia ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa lengo la kuisaidia Tanzania kukuza uchumi wa viwanda na kuondoa umasikini kwa wananchi wake.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipoteta na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Hafez Ghanem katika mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mjini Bali, Indonesia.

Dk Mpango alisema Benki ya Dunia imeamua kuwekeza katika teknolojia kwa kuwa ni eneo sahihi linaloweza kukuza uchumi wa Taifa kwa zaidi ya mara mbili kutokana na tafiti ilizofanya.

“Kimsingi Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia amefurahia ajenda za maendeleo za Tanzania kuhusu kujenga uwezo wa rasilimali watu katika kukuza uchumi wa viwanda na ameahidi kuanza kwa kuwekeza zaidi kwa watoto wenye umri mdogo ili mipango ya maendeleo ya nchi iwe endelevu,” alieleza Dk Mpango.

Waziri Mpango alimweleza Makamu wa Rais wa Benki hiyo Tanzania imeweka mikakati ya kujenga uchumi wa viwanda ikitumia malighafi za ndani kuongeza ajira kwa wananchi wengi.

Kuhusu umuhimu wa sekta binafsi kwa maendeleo ya nchi, Waziri Mpango alisema Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Ghanem, aliahidi kuwekeza zaidi katika miradi ya pamoja kati ya Sekta ya Umma na ile ya Binafsi (PPP).

Aliahidi kuwekeza kwa kuiwezesha Serikali na wadau wengine kupata mafunzo mbalimbali yatakayoongeza ujuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo katika nchi zilizofanya vizuri katika eneo hilo ili kuongeza ufanisi wakati wa utekelezaji.

Kamishna na Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles Kichere, alisema mfumo wa dunia ya sasa unazitaka nchi kujitegemea kimapato. Alisema TRA itaongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuwa WB imeahidi kuboresha miundombinu ya ukusanyaji mapato.

Waziri Mpango ameiomba Benki ya Dunia iendelee kuisaidia Tanzania kwa rasilimali fedha kuwezesha miundombinu ya kukuza uchumi ikiwemo miradi ya nishati ya umeme, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), miradi ya maji.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ameahidi kutembelea Tanzania mwanzoni mwa mwaka ujao kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo kati ya benki hiyo na Serikali ya Tanzania.

Mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bali imewakutanisha wadau wa masuala ya fedha wakiwemo Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali kujadili Sera na misaada inayotolewa na taasisisi hizo.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maaalumu, Bali

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi