loader
Picha

Taharuki kutekwa bilionea MO Dewji

VYOMBO vya usalama nchini vinaendelea na uchunguzi na msako wa kumtafuta tajiri kijana zaidi barani Afrika, Mohamed Dewji ‘MO’, ambaye alitekwa nyara mapema jana asubuhi na watu wasiojulikana.

MO (43) ambaye ana utajiri wa Dola bilioni 1.5 ikiwa ndiye tajiri nambari moja Afrika Mashariki, alitekwa wakati akiingia katika eneo la kufanyia mazoezi jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, MO alifika katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila siku alfajiri kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

Hata hivyo, punde aliposhuka tu kwenye gari yake, watu wasiofahamika walijitokeza na kufyatua risasi hewani kisha kumnyakua na kutokomea naye kusikojulikana. Nani kamteka Mo? Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kuwa waliomteka mfanyabiashara MO ni watu wawili wazungu ambao msako mkubwa unafanywa kuhakikisha wanakamatwa pia.

Mambosasa alisema jana mchana saa kadhaa baada ya tukio kuwa Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu kwa mahojiano kuhusu kutekwa kwa mfanyabiashara huyo. Aidha mpaka saa 8:46 mchana wa jana alipotafutwa, Kamanda huyo alisema kuwa hakuna taarifa mpya na kwamba polisi ilikuwa ikiendelea na kazi yake ya kumtafuta.

Mapema jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa vyombo vyote vya usalama viko kazini na kwamba wananchi wawe watulivu kwa kuwa ufuatiliaji unafanyika ili kumuokoa.

Jinsi tukio lilivyotokea Mambosasa alipozungumza na wanahabari waliofika kwenye eneo la tukio (Hoteli ya Colosseum) alisema kuwa waliomteka MO ni wazungu wawili. “Asubuhi ya leo wazungu wawili walikuwa na gari aina ya Toyota Surf.

Kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa ndani na lingine nje, gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la Mo Dewji lililokuwa limepaki,” aliwaeleza wanahabari na kuongeza kuwa; “Na Dewji akiwa ndani ya gari hilo wazungu wawili wakatoka na kufyatua risasi hewani kisha kumbana MO Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake, na kisha kumpakia katika gari lao aina ya Toyota Surf kisha wakaondoka naye kwenda kusikojulikana.”

Hata hivyo mashuhuda walisema kuwa mfanyabiashara huyo alitekwa akiwa hana walinzi wowote na hata gari alilokuwa analitumia, alikuwa anaendesha mwenyewe. Familia yashikwa na bumbuwazi Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na operesheni ya kumtafuta, gazeti hili lilimkuta baba mzazi wa MO, Gullamabbas Dewji akiwa na baadhi ya wanafamilia kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Alipozungumza na gazeti hili majira ya saa 6:31 mchana na hata baadaye saa 6:57 mchana, Gullam alisema kuwa kila kitu kiko chini ya Polisi na kwamba Polisi inapambana kwa hali na mali kuhakikisha mtoto wake anapatikana. “Kwa sasa polisi inaendelea na uchunguzi, naamini MO atapatikana kwani nina imani kubwa na kazi inayofanywa na jeshi letu la polisi,” alisema Gullam.

Katika hatua nyingine, kikundi cha uokoaji kwenye maafa cha jamii ya Kiasia nchini cha KSIJ Task Force kimesema kuwa kina imani kuwa mwanachama wao, MO atapatikana. Ofisa Usalama wa kikundi hicho, Rithiwani Rattansi akiwa nje ya eneo la tukio alisema, “MO atapatikana, polisi wetu wanafanya kazi.” Taharuki yatanda mitaani Watanzania ikiwemo viongozi kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakieleza kushangazwa na kusikitishwa kwao na kisa cha kutekwa kwa bilionea huyo.

Baadhi wameeleza wasiwasi na kuomba kila anayeweza kuwa na taarifa kushirikiana na vyombo vya dola;. Mapema saa 2: 36 asubuhi jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano, January Makamba aliandika katika ukurasa wake wa Twitter; “Nimezungumza na baba yake @ moodewji. Habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli.

Nimetikiswa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo. Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.” Majira ya saa 3 kamili asubuhi, Mbunge wa Kigoma Mjini, Z itto Kabwe (ACT Wazalendo) aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter; “Nimeshtushwa na kuumizwa na habari za kutekwa kwa ndugu yetu @ moodewji leo alfajiri akiwa anakwenda mazoezini hapa Dar.

Kila mmoja wetu mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumwokoa asaidiane na vyombo vyetu vya dola. Mola atamsaidia MO na familia yake katika mtihani huu.” Naye Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) kupitia Twitter majira ya saa 3: 03 aliandika; “Inasikitisha na kustua tukio hili la @ moodewji kutekwa aina hii ya uhalifu inaota mizizi ana familia ana watoto ana ndugu tuendelee kumuombea kwa Allah na kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama Allah amlinde.”

Mashirika ya Kimataifa, balozi zashtushwa Ubalozi wa Italia nchini kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter ilisema kuwa imeshtushwa na taarifa za kutekwa kwa MO jana na kusema kuwa wanaiombea utulivu familia ya mfanyabiashara huyo tajiri na mwenye ushawishi mkubwa nchini.

Nayo Taasisi ya Forbes imetoa taarifa hiyo ya kutekwa kwa MO na kusema kuwa inasikitisha isipokuwa wanaomba apatikane akiwa salama. Aidha vyombo mbalimbali vya habari duniani vimetoa habari kuhusu kutekwa kwa tajiri huyo.

Vyombo kama BBC ya Uingereza, CNN ya Marekani, DW ya Ujerumani, RFI ya Ufaransa, Business live ya Z ambia, Citizen TV, The East African na vyombo vingine vya Kenya, pamoja na mitandao mingine mingi duniani vimeelezea tukio hilo. Mo Dewji ni nani ? Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, Mo Dewji ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Mo mwenye umri wa miaka 43 ndiyo tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni mwa matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika. “Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo. Mohammed Dewji ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya METL iliyoanzishwa na baba yake miaka ya 1970.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia inaingiza mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh trilioni 2.5) kwa mwaka. Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli. Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

METL ina shughuli zake katika nchi sita barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo zaidi. Dewji ni mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya, elimu na maendeleo jamii. Mbali na biashara na shughuli za jamii, Mo Dewji amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kati ya mwaka 2005 hadi 2015, na sasa ni mwekezaji mkuu kwenye Klabu ya Soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi