loader
Picha

Chadema ‘kususia’ ajali Mv Nyerere kwamkimbiza mbunge

KUKOSEKANA kwa ushiriki mzuri wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere iliyotokea Ukerewe mkoani Mwanza mwezi uliopita, kumesababisha Mbunge wa Jimbo hilo Joseph Mkundi (Chadema) kukihama chama chake na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumzia uamuzi wake huo jana, Mkundi alisema hiyo ni sababu kubwa kati ya sababu tatu za kuhama kwake. Alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo iliyoua watu 228 mwezi uliopita, viongozi wa Chadema hawakushiriki kikamilifu katika kushughulikia suala hilo.

Alisema badala yake viongozi hao walitumia muda mwingi kuilaumu serikali kwa kile walichodai kushindwa kuchukua hatua stahiki ya kuwanusuru abiria waliokuwa kwenye kivuko hicho, hatua iliyomkera na kumsikitisha.

Aliitaja sababu nyingine ya kukihama chama hicho kuwa ni kukosekana kwa mfumo mzuri wa kusikiliza wabunge ndani ya chama. “CCM imenivutia kwa sera zake na uwezo wake wa kutatua na kufuatilia mambo hasa kero za wananchi wangu kwa ukaribu zaidi, kitu ambacho ni kizuri katika kuwasaidia wananchi.,”alisema na kuongeza: “Nimehamia CCM bila ya kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu ila nina mapenzi na chama hiki kikubwa chenye sera zinazoeleweka na kutekelezeka.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile alisema chama chake kimepokea barua ya Mbunge Mkundi inayoelezea kuhamia CCM akitokea Chadema na kuwa uongozi wa wilaya umemkaribisha kwa mikono miwili.

Alisema “Sisi hatuna hiyana manake huyu kuja kwake kwenye chama hiki ni kwamba amependa sera na utendaji kazi wetu kwa hiyo hakuna shida ya yeye kuhamia chama hiki, tunatarajia kuendelea kuchapa naye kazi kwa kadiri iwezekanavyo.” Mbali ya Mkundi, hivi karibuni wabunge wengine watatu wa Chadema walikihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Dk Godwin Mollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga) na Julius Kalanga (Monduli) na walitetea viti vyao kwenye uchaguzi mdogo. Vifungu vya 37 (1) b na 46 (2) vya Sheria ya Uchaguzi vinaipa Mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini kutangaza jimbo kuwa wazi na kuitisha uchaguzi mdogo hivyo kwa kitendo cha Mkundi kuihama Chadema kwa sasa inasubiriwa kauli ya NEC kuhusu tarehe ya uchaguzi mdogo.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi