loader
Picha

‘Ewe Dodoma si mdogo tena miongoni mwa majiji duniani’

ILIKUWA vigumu kumshawishi mkazi wa Dodoma na vitongoji vyake pamoja na halmashauri zote saba za Kondoa Mji na Vijijini, Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chamwino na jiji la Dodoma kwamba serikali inahamia Dodoma.

Hata pale Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohamia Dodoma rasmi mwaka juzi na kujitambulisha kwao, wakazi wa Dodoma wakiwemo wenyeji wa asili ya mkoa huu ambao Wagogo, waliendelea kutoamini.

Pamoja na mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wasaidizi wao pamoja na watendaji wengine kuanza kufanya kazi kutokea Dodoma sambamba na ongezeko la majengo kama ya LAPF, Hazina na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, bado ilikuwa ngumu kuwashwishi wana-Dodoma kwamba mambo ndio yanaendelea kuiva.

Hata alipohamia Dodoma Makamu wa Rais mwishoni mwa mwaka jana, bado wapo ambao hawakuamini kwamba Dodoma ni makao makuu ya serikali. Kwenye vijiwe vya kahawa, vya kushona viatu, kuuza magazeti na vijiwe vingine vingi ungeweza kusikia maongezi ya watu wasioamini kwamba serikali kwa asilimia 100 inahamia Dodoma na Dar es Salaam kubaki jiji la biashara.

Sababu ya kutoamini ni ndogo tu. Kwamba tangu Oktoba 1, 1973 serikali ilipotangaza Dodoma kuwa makao makuu ya nchi hadi leo, ahadi za kuhamia Dodoma ziliendelea kuwepo bila kutekelezwa.

Kwamba hata Bunge lilipohamia rasmi Dodoma, wengi walidhani ni mwanzo mzuri wa hatua hiyo ya serikali kuhamia Dodoma lakini viongozi na wawakilishi wa wananchi wakawa ni watu wa kuja bungeni na kuondoka baada ya Bunge.

Kimsingi wana-Dodoma waliendelea kuamini kwamba wazo la Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere linaendelea kubaki kuwa ndoto za mchana. Wenyeji wengi, angalau walianza kuamini dhamira ya serikali ya kuhamia Dodoma kuanzia Aprili 26, 2018 katika Uwanja wa Jamhuri wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Z anzibar.

Hii ni pale Rais John Magufuli alipotangaza kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa jiji. Baadhi ya wananchi kama Juma Chabruma alisema: “Sasa inawezekana kuna ukweli kwamba Serikali itahamia Dodoma, hata hivyo hatujaamini vizuri. Iliwahi kufanyika hivyo huko nyuma. Viongozi wakahamia hapa Dodoma lakini baadaye, mmoja mmoja akawa anarejea Dar es Salaam.”

Amina Chaurembo naye anasema kwamba kwa wakazi wa Dodoma kuona viongozi wakija Dodoma na kudai wamehamia na baada ya muda kuona wanarudi Dar es Salaam ni jambo walilolizoea. Lakini baadhi ya wakazi wa Dodoma, hususani wasomi, wanasema walianza kuamini kwamba serikali inahamia Dodoma pale sheria ya kuhamia Dodoma iliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni.

Kuletwa muswada wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma, kuliwapa nguvu ya ziada wananchi na hasa walipoona wabunge wa mkoa wa Dodoma, wakichachamaa kuhakikisha muswada unapita.

Mbunge Joel wa Chilonwa, Job Ndugai wa Kongwa, George Lubereje wa Mpwapwa, Goerge Simbachawene wa Kibakwe, Edwin Sannda wa Kondoa Mjini na Dk Ashatu Kijaji wa Kondoa Vijijini ni miongoni mwa waliotoa mchango chanya kuunga mkono muswada huo.

Wengine waliofanya vivyo hivyo ni Juma Nkamia wa Chemba, Omari Baduel wa Bahi, Antony Mavunde wa Dodoma Mjini, Livingstone Lusinde wa Mtera pamoja na wabunge wa Viti Maalumu, Fatuma Taufiq na Felista Burra.

Pamoja na kuchangia walieleza umuhimu na ubora wa Dodoma, wakaeleza vivutio na sifa za wakazi wa Dodoma pamoja na mambo kadha wa kadha na hivyo wakawakaribisha wabunge na watanzania kwa ujumla kujenga na kuwekeza Dodoma, jiji lililopimwa na kupangwa vizuri.

Hatimaye historia iliandikwa Septemba 4, 2018 wakati Bunge hilo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika Ndugai na baadaye Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge walilipopitisha rasmi sheria inayoitambua Dodoma kuwa makao ya serikali.

Kampeni na juhudi za kushawishi za wabunge na Watanzania hazikuishia bungeni kwani baada ya muswada kupitishwa kuwa sheria, kila mbunge alikuwa na kazi ya kuwaaminisha wapigakura wake katika jimbo lake kwamba sasa Dodoma ni makao makuu ya nchi kisheria.

Kwa kumbukumbu za mkazi wa Dodoma, Prasdus Mazengo hata jiji la Dar es Salaam lilioanzishwa mwaka 1946 kuwa makao makuu ya nchi, halikutokana na sheria ya Bunge isipokuwa Dodoma.

Mazengo ambaye kitaaluma ni mwanasheria anasema, sheria hiyo pamoja na kuwa na vifungu maalumu vya namna ya kuendeleza makao makuu ya nchi, faida nyingine ni kwamba haiwezekani kiongozi kwa matakwa yake yawe ya kisiasa au ya kijiografia akaamuka na kuhamisha makao, lazima kwanza alete muswada bungeni ili sheria ya sasa ibadilishwe na muswada huo uridhiwe na wabunge theluthi mbili.

“Pamoja na wabunge theluthi mbili, ni lazima Rais wa nchi akubali kubadilisha sheria ya Dodoma kuwa makao makuu, na kutunga nyingine. Ni kazi ngumu mno kwa sasa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi kisheria,” anasema.

Historia ya Dodoma kuwa si jiji Dogo miongoni mwa majiji duniani na kupata hadhi ya kuwa makao makuu ya nchi, ilianza kwa kusomwa muswada huo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo.

Muswada huo wa mwaka 2018, ambao sasa ni sheria, inauitambua Dodoma kisheria kuwa ni makao makuu ya serikali ya Jamhuri ya Muungano. “Chimbuko la hoja ya kutunga sheria hii ni kukosekana kwa sheria inayotambua na kuweka misingi ya uendelezaji wa makao makuu ya nchi,” anasema Jafo.

Jafo anasema, “Pamoja na jitihada zilizofanywa na serikali katika kuendeleza makao makuu ya nchi, kukosekana kwa sheria inayotambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, kulisababisha uendeleza wa halmashauri hiyo kutofikia malengo.

“Hivyo, msingi wa kutunga sheria hii na kutambua kisheria jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, kunalenga katika kuendeleza halmashauri hiyo kwa kuzingatia sheria iliyotungwa.” Kitendawili cha kuhamia Dodoma kilishindikana kuteguliwa katika awamu nne zilizotangulia kutokana na sababu nyingi zikiwemo za kiuchumi, hasa baada ya Tanzania kuingia katika vita na Uganda na kuyumba kwa uchumi duniani. Kingine kilichochangia ni kutokuwepo kwa sheria ya kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi.

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi