loader
Picha

Simba yaahirisha mazoezi kumuombea Mo Dewji

BAADA ya kutekwa na watu wasiojulikana kwa shabiki mkubwa wa Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji, uongozi wa Simba uliahirisha mazoezi ya timu hiyo jana ili wachezaji na benchi la ufundi kushiriki katika kumuombea mfanyabiashara huyo mkubwa.

Mbali na kuwa mfanyabiashara, Mo pia ni mwekezaji wa klabu ya Simba anayetarajiwa kununua hisa 49. Simba ipo kwenye mchakato wa mabadiliko kutoka kumilikiwa na wanachama mpaka kwenda kwenye mfumo wa hisa ambapo Mo anatarajiwa kununua hisa 49 na zilizosalia kubaki kwa wanachama.

Mapema jana, MO (43) alitekwa akijiandaa kuingia kwenye mazoezi katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay Dar es Salaam. Mo hufanya mazoezi hapo kila siku alfajiri.

Inadaiwa, jana aliposhuka kwenye gari lake kwa ajili ya kuingia kwenye mazoezi, walijitokeza watu wasiojulikana na kufyatua risasi juu kisha kutokomea na mfanyabiashara huyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema jeshi lake linafuatilia kwa karibu tukio hilo na kutoa onyo kwa waliohusika kumrudisha mfanyabiashara huyo mzima.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema: “Uongozi wa klabu ya Simba kwa mashauriano na benchi la ufundi chini ya kocha Patrick Aussems limeamua kuahirisha mazoezi ya timu leo (jana) ili kutoa fursa kwa wachezaji na benchi la ufundi kushiriki ipasavyo kwenye dua na sala kwa ajili ya kiongozi wetu Mo”.

Manara alisema klabu inawaomba watanzania na wanaoitakia mema nchi wasiache kumuombea uhai na uzima Dewji. Mo, ambaye zaidi ya miaka 10 iliyopita amewahi kuwa mfadhili wa Simba, amekuwa msaada mkubwa wa klabu hiyo tangu msimu uliopita kwani licha ya kufanyika mchakato wa kwenda kwenye mfumo mpya, amekuwa akitoa misaada kadhaa ikiwemo fedha za usajili wa baadhi ya wachezaji na kuajiri makocha.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi