loader
Picha

Ukaguzi mpya vyeti feki waja

SERIKALI imejipanga kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika wizara, taasisi na mashirika ya umma ili kubaini watumishi wenye vyeti feki waliobakia kwenye utumishi wa umma.

Imewaonya viongozi waliofumbia watumishi hao wenye vyeti feki kuwa watachukuliwa hatua. Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alibainisha hilo jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa kikaokazi cha wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dk Ndumbaro alisema hatua hiyo, inatokana na kuwapo na tofauti kati ya orodha ya watumishi waliohakikiwa na wale wanaolipwa mshahara. “Hili la kutowajibika kwa baadhi ya wakuu wa Idara za Utawala na Utumishi imejitokeza katika uhakiki wa vyeti vya watumishi ambapo baadhi ya watumishi hawakuhakiki mpaka ofisi yangu ilipotoa maelekezo zaidi ya mara tatu, hii ilionesha walikuwa na maslahi binafsi na wahusika au kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Dk Ndumbaro.

“Naamini hata leo kuna baadhi ya taasisi zina watumishi wenye vyeti feki, maofisa utumishi mko hapa maelekezo mmepewa, lakini wengine wanaongopa lawama, siwatishi lakini iko siku itakuja, tutakapomkamata mtu mwenye cheti feki katika taasisi yako na wewe siku hiyo hiyo kibarua chako kimeota nyasi.

“Haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais (John Magufuli) kwamba wenye vyeti feki waondolewe, lakini bado kuna watu wa aina hiyo kwa kuwalea, ama ndugu na jamaa au kuogopa siasa, lakini maelekezo watu wenye vyeti feki waondoke,” alisema.

Dk Ndumbaro aliongeza, “Tunao mkakati wa kufanya ukaguzi kwa sababu sisi tunajua idadi ya watu ambao vyeti vyao vilihakikiwa na idadi ya watu wanaolipwa mshahara, tunaona kuna tofauti katika maeneo mengi kati ya watu waliohakikiwa na wale ambao wanalipwa kwenye payroll.”

Alisema ukaguzi na uhakiki huo, utafanyika pia kwenye taasisi, kampuni na mashirika ya umma ambayo hayako kwenye mfumo wa ulipaji mshahara wa Serikali Kuu. “Na zile taasisi ambazo hazilipwi kwenye mfumo wetu, nazo tutazitembelea kuona tofauti kati ya watumishi waliohakikiwa na wale wanaolipwa mshahara.

Tutakapofanya ukaguzi baada ya maelekezo ya zaidi ya miaka miwili sidhani kama mtakuwa na mtu wa kumlaumu, mtajilaumu wenyewe kwa uzembe na kutotekeleza maagizo ya serikali,” alifafanua Katibu Mkuu Utumishi.

Aidha, alisema utumishi wa umma unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo baadhi zinasababishwa na wakuu wa idara za utumishi na utawala kutozingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kushughulikia masuala mbalimbali na kuwataka kufanya kazi kwa utashi wao.

“Baadhi yenu mmekuwa mkiwapandisha vyeo watumishi wakati hawana sifa zilizoainishwa katika muundo wa utumishi, wote tunajua cheo kinatakiwa apewe mtu mwenye sifa ya ofisa mwandamizi.

Hali hii imekuwa ikiwaathiri watumishi husika kwa sababu maombi ya kubadilisha mishahara ili ilingane na vyeo vipya yasipoidhinishwa na Ofisi ya Utumishi huwashusha ari na morali ya kazi,” alieleza.

Aidha, aliwakumbusha kusimamia vyema rasilimali za umma huku akiwataka kuwapongeza wale wanaofanya kazi na kuadhibu wazembe kulingana na taratibu. Pia aliwakumbusha kuhusu mabadiliko ya sheria, ambayo inaweka uwiano katika taasisi na kuondoa watumishi kujijengea himaya katika taasisi moja na kuwa hiyo itajenga uhai na afya katika utumishi wa umma.

“Katibu Mkuu amepewa mamlaka ya kuwahamisha kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine ili kuboresha ufanisi na tija katika utumishi wa umma. Baadhi ya waajiri wameanza tabia ya kukataa kuwaruhusu watumishi wao kuhama,” alisema.

Akizungumzia elimu za watumishi, waliwataka maofisa utumishi kuwashauri nini cha kusoma kulingana na mahitaji ya taasisi husika na kuwa watumishi wengi wanashindwa kupata haki zao kwa kuwa na mchanganyiko wa elimu.

“Taaluma ya mtumishi inatambuliwa kwa shahada yake ya kwanza, sasa ukienda kusoma shahada ya pili mambo tofauti ukirudi hutanufaika,” alisema. Kauli hiyo ya mfumo wa elimu, aliitoa kutokana na Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Afya), Dk Zainabu Chaula kueleza kuwapo kwa wingi wa malalamiko ya watumishi, ambao wamekuwa wakisoma vitu tofauti na walivyoajiriwa hivyo kushindwa kufanyiwa mabadiliko ya kiutumishi.

“Kuna malalamiko ya mtumishi ambaye kaajiriwa na diploma ya walimu, baadaye akasoma shahada ya kwanza ya ustawi wa jamii, alivyoona hailipi akaenda kusoma masuala ya rasilimali watu, mtu kama huyo hata akiwa na digrii tatu atabaki kuwa mwalimu,” alifafanua.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Doroth Mwaluko alikemea tabia ya maofisa utumishi kufanya kazi ya kiupolisi, badala ya kuwa waelimishaji, washauri na wasioendekeza majungu.

Alisema kutowajibika ipasavyo kwa watendaji hao, kumekuwa chachu ya kusababishia serikali madeni makubwa kwa kushindwa kufanya maamuzi kwa wakati, kuibua lawama na manung’uniko kutoka kwa watumishi na wananchi.

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais (Menejimenti ya Utumishi ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi