loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Elisha Osati Daktari kijana mwenye tuzo ya Ujerumani

VIJANA ni nguzo kuu, hiyo ni imani tulionayo na wakiwezeshwa na kupewa misingi imara wana uwezao mkubwa wa kulikwamnua taifa kutoka katika hatua moja kwenda hatua nyingine bora zaidi.

Katika kila sekta wako vijana wanaofanya mambo mazuri, ikiwemo sekta ya afya ambayo ina vijana wanaojitoa kuhakikisha kwamba kwa uwezo walionao wanaifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi na afya za watu kuimarika.

Dk Elisha Osati ni mmoja wa vijana imara waliosimama katika sekta ya afya. Daktari huyo anasema anaamini ana mchango mkubwa aliotoa katika sekta hiyo ndio maana jina lake liliteuliwa na isiwe mtu mwingine na pia katika chama na kutetea sekta ya afya.

Kijana huyu daktari ni Rais mteule wa Chama cha Madaktari hapa nchini (MAT) ambaye anatarajiwa kusimikwa urais Oktoba 26, mwaka huu, kushika nafasi hiyo ambayo alikuwa anaishikilia kwa sasa Dk Obadia Nyongole anayemaliza muda wake.

Hivi karibuni Dk Osati alishinda tuzo ya madaktari viongozi vijana duniani inayotolewa nchini Ujerumani, tuzo ambayo kwa nchi za Afrika wamepata madaktari vijana watano pekee. Historia yake Alizaliwa Novemba 1983, Rorya mkoa wa Mara akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu.

Alimaliza Shule ya Msingi Mbagala Kuu na kujiunga na Shule ya Sekondari Azania 2003 na baadaye Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Same. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) kwa ajili ya Shahada ya Kwanza na kuhitimu mwaka 2011.

Baadaye alifanya mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Temeke. Mwaka 2013 aliajiriwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kama daktari katika idara ya magonjwa ya ndani, kitengo cha magonjwa ya damu ambako alifanya kazi kwa miaka mitatu.

Baadaye alirudi kusoma masomo ya kibingwa akisomea magonjwa ya ndani na katika chuo hicho cha Muhas na kuhitimu na sasa ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, kazi anayofanya katika hospitali ya taifa Muhimbili.

Akizungumzia zaidi maisha yake na hatua mbalimbali alizopitia, ikiwa ni pamoja na kushika nafasi za uongozi hadi kufika hapo alipo sasa, Dk Osati anasema, “tangu nikiwa shule ya msingi nilikuwa kiranja wa usafi, monita na kiongozi wa masuala ya afya na sekondari nilikuwa mwenyekiti wa majadiliano shuleni, tulikuwa tukifanya sana majadiliano katika shule mbalimbali, nilikuwa katibu msaidizi wa gazeti, mhariri msaidizi wa gazeti la shule, nilikuwa nahodha wa timu ya Moira.”

Anasema akiwa sekondari alikuwa mwenyekiti msaidizi wa Umoja wa wanafunzi wa Katoliki katika shule ya Azania na Jangwani (AzaJangwa TWCS) na kwa Same Sekondari alikuwa waziri wa taaluma na pia kiongozi YCS wa jimbo la Same na Mwanga.

Kwa mujibu wa Dk Osati alipofika Muhas alikuwa nahodha wa timu ya mpira wa miguu wa chuo akiwa mwaka wa kwanza na mwaka wa pili akawa waziri wa michezo na mambo ya jamii, mwaka wa tatu na nne alichaguliwa kuwa kiongozi wa wanafunzi katika sekta ya afya.

Lakini pia alikuwa kiongozi wakati wanafunzi wote wanaochukua Shahada ya Uzamili wa vyuo vyote vya afya nchini. TAFITI Dk Osati anasema akiwa Shahada ya Kwanza kwa kushirikiana na mwanafunzi wenzake walifanya utafiti kuangalia ni vitu gani vinawafanya wafanyakazi kuridhika kazini katika hospitali mbalimbali.

“Hii ni katika hospitali za umma na za binafsi nilikuwa naangalia ni kitu gani kilikuwa kinawafanya waridhike zaidi, utafiti ambao tulifanya tukiwa mwaka wa nne chuoni, huu utafiti ulikuwa mzuri sana,” anasema.

Utafiti mwingine alioshiriki kufanya ni pamoja na mgonjwa wa selimundu waliyembadilisha damu na kumwekea damu isiyo na wadudu bila kutumia mashine. “Kawaida hufanywa na mashine, lakini sisi tulifanya bila mashine wagonjwa wawili na tulifanikiwa kabisa wagonjwa hao wakapona, kwa hiyo tukasema unaweza kufanya huduma hiyo kwa vifaa mlivyonavyo tu,” anasema.

Mwingine ni wa kuangalia ubora wa afya kwa wagonjwa wa Ukimwi na utumiaji wao wa dawa na vipimo kwa ujumla. TUZO Mwaka huu aliteuliwa kupata tuzo ya madaktari viongozi vijana ‘Young Physician Leadership Award’ inayotolewa na taasisi ya Inter-Academy Partnership wakitambua vijana waliofanya vizuri katika uongozi katika kipindi cha mwaka mmoja wakishirikiana na Tanzania Academy of Science iliyo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) na ndio iliwasilisha jina lake.

Katika tuzo hiyo vijana 24 duniani wametambuliwa na watano kati yao ni kutoka Afrika. Tuzo hiyo wanapewa vijana ambao umri wao ni chini ya miaka 40. “Kila nchi kuna akademia za sayansi na kwetu ipo inaongozwa na Profesa Ester Mwaikambo wao wanamtambua mtu, kwa hiyo wanakuita na utapeleka wasifu wako (CV) wataangalia vitu ulivyofanya kwa mwaka mzima wakiona unafaa basi wanakupendekeza, kisha wao wanakaa na kuangalia wanaofaa.

Kwa hiyo kwa mwaka huu duniani ni vijana kama 24,” anasema Dk Osati. Kwa Afrika nchi nyingine zinazopokea tuzo hiyo ni Cape Verde, Sudan, Afrika Kusini na Misri. Wiki iliyopita Dk Osati alitunukiwa Tuzo ya Uongozi katika Sekta ya Afya kwa Madaktari vijana, mjini Berlin, Ujerumani.

Tuzo hiyo imetolewa na Shirika la Inter-Academy Partnership (AIP) Dk Osati anasema wiki hii yuko nchini Ujerumani kupata mafunzo ya wiki mbili kisha alipata nafasi ya kuwakilisha mada katika Mkutano Mkuu wa Afya (World Health Summit) baada ya kuchagua mada ya kuwakilisha.

“Mimi nimezungumzia huduma bora ya afya kwa wote nchini kwetu, changamoto zake pamoja na fursa nimechagua hilo kwa sababu ni kaulimbiu ya nchi pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO),” anasema na kuongeza kwa wananchi kupata huduma bora ni jambo la msingi.

“Na kwa kaulimbiu ya Rais kujenga viwanda itawezesha uwekezaji nafuu na hivyo dawa na vifaa tiba kupatikana kwa bei nafuu na huduma bora kwa wote, pia tutapata nafasi ya kutoa mada katika mkutano mwingine wa wawekezaji wa kampuni za dawa na vifaa tiba nitawasilisha pia mada kama hiyo,” anasema.

Aidha alipata fursa ya kushiriki kwenye jukwaa la umoja wa Ujerumani na Afrika mkutano ambao Ujerumani wanaangalia wapi wataweza kuwekeza katika sekta ya afya na katika mkutano huo Dk Osati anasema alizungumzia changamoto na fursa zilizopo ili kuona wanaweza kushirikiana vipi na Tanzania kuboresha afya.

“Kwangu mimi hii ni faraja kubwa, binafsi na familia yangu, chama chetu MAT na sekta nzima ya afya,” anasema Dk Osati. MAT Anasema katika uongozi wake, anaoutumikia sasa kama makamu wa Rais, falsafa yake ni kujenga uhusiano mzuri na wenzake pamoja na kuwa na uhusiano mzuri na serikali kwa kuheshimiana katika maamuzi yote.

“Mwanzoni uhusiano kati ya chama cha madaktari na serikali haukua mzuri lazima tuseme kweli, shida ilikuwa ni mawasiliano tu, hata nyumbani kama hakuna mawasiliano hakuna amani, jambo zuri ni kushirikishana bila kuogopana, hiyo tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sasa,” anasema.

Anasema sasa serikali imeelewa malengo ya MAT na wao wako tayari kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali na pia kupokea ushauri.

Nafasi ya Urais Akirudi kutoka katika mkutano huo wa kimataifa, anakwenda kushiriki mkutano wa 50 wa MAT utakaofanyika Oktoba 26 mwaka huu na ndipo atasimikwa kuwa Rais wa chama.

Mkutano huo utafanyika mjini Dodoma katika ukumbi wa Mtakatifu Gasper. Mwaka 2016, Dk Osati aliteuliwa kuwa Rais Mteule wa Chama cha Madaktari (MAT), kwa utaratibu waliojiwekea, rais akishateuliwa hutumikia kama makamu wa rais nafasi ambayo anaitumikia kwanza kwa miaka miwili kabla ya kuapishwa sasa kuwa rais kamili.

“Tunafanya hivi ili kiongozi aweze kupata uzoefu kwa sababu anafanya kazi kama makamu wa rais na uchaguzi unaofuata sasa ndio unasimikwa kuwa Rais na anayeteuliwa tena anakuja kuwa makamu… lakini Rais aliyemaliza muda wake Dk Obadia Nyongole anabakia kwenye baraza nafasi atakayoitumikia kwa miaka miwili kisha ataondoka,” anasema.

Dk Osati anasema anaanza kuitumikia nafasi ya rais bila shida kwa sababu ameshapata uzoefu wa namna ya kufanya kazi akiwa kama makamu wa rais, anatambua changamoto ziko wapi, hivyo mfumo kwao wanaona ni mzuri unawasaidia na inakuwa sio kazi mpya sana.

MIONGONI mwa vitu vinavyoweza kututofautisha binadamu ni namna tunavyopokea changamoto ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi