loader
Picha

Kitendawili cha mwandishi ‘kupotea’ Ubalozi wa Saudia

HIVI karibuni ulimwengu ulipatwa na mshituko kutokana na kupotea kwa mwandishi raia wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi. Tarehe 2 mwezi huu, mwandishi huyo aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, lakini baada ya hapo hakuonekana na ndipo maswali mengi yanaulizwa.

Kuna wanaosema ametekwa nyara na kusafirishwa hadi Saudia. Na wengine wanasema ameuliwa na akakatwa vipande kisha akatolewa ubalozini kwa kutumia masanduku. Ubalozi wenyewe unadai kuwa Khashoggi alimaliza shughuli zake hapo ubalozini na akatoka.

Hata hivyo, kamera za usalama zinaonesha akiingia lakini haonekani akitoka. Siku mbili kabla ya kupotea kwake, Khashoggi alifika hapo ubalozini kuomba cheti cha talaka ili aweze kufunga tena ndoa na mchumba wake, Hatice Cengiz, raia wa Uturuki.

Akaambiwa arudi tarehe 2 Oktoba ili kuchukua cheti hicho. Akarudi na mchumba wake ambaye alisubiri nje. Baada ya saa mbili mwanamke huyo aliingiwa na wasiwasi ndipo alipoanza kudadisi.

Vyombo vya usalama vya Uturuki vikafanya uchunguzi na inasemekana walipata video ikionesha jinsi Khashoggi alivyoteswa na kuuliwa. Gazeti la Washington Post limesema katika chombo cha kurekodi zinasikikia sauti ya Khashoggi akihojiwa kwa nguvu. Ripoti pia inasema makomando 15 waliwasili hapo ubalozini kutoka Saudia wakati Khashoggi akiwa hapo.

Baada ya muda wakaondoka wakiwa wamebeba masanduku yakiwa na viungo vyake. Ndege zao mbili ziliondoka Istanbul, moja ikielekea Cairo na ya pili ikaelekea Dubai. Swali ni kwa nini ndege hizo hazikurudi Saudia zilikotoka? Maswali mengi yanahitaji kujibiwa iwapo utafanyika uchunguzi huru na wa kina.

Kwa mfano, hao makomando 15 walifika ubalozini kwa kazi gani? Je, ni kweli kuwa operesheni ilitokana na maagizo ya mwana mfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman (MBS)? Yeye amekabidhiwa madaraka kamili na baba yake, mfalme Salman na ni vigumu kuwa hakuwa anaelewa chochote. Tayari serikali za Uturuki na Saudia zimekubali kuendesha uchunguzi kwa kushirikiana.

Kama hii ikifanyika basi ushahidi wa kwanza utakuwa ni video ya siri iliyonasa picha na sauti wakati Khashoggi akiwa ubalozini hapo. Kilichofanyika ni kuwa Khashoggi alivaa saa ya mkononi yenye kamera. Chochote kilichonaswa kilikuwa kinarushwa hadi simu ya kiganjani aliyokuwanayo mchumba wake aliyekuwa anasubiri nje. Video hii ilishindwa kunasa vizuri wakati Khashoggi anateswa lakini hata hivyo sauti iliendelea kunaswa na kusikika.

Simu hii yenye video na sauti sasa iko mikononi mwa wanausalama wa Ururuki. Na gazeti la Washington Post linasema serikali ya Uturuki imewasilisha ripoti yake kwa serikali ya Marekani.

Uturuki pia inadai kuwa ina ushahidi mwingine nao ni kuwa walichunguza maji taka yanayotoka hapo ubalozini na wamekuta matone ya damu katika karo nje ya ubalozi. Sasa Uturuki tayari imefanya uchunguzi ndani ya ubalozi na nyumbani kwa balozi.

Humo ndani huenda wakagundua matone ya damu au alama za vidole. Rais Trump amemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje kwenda kuonana na mfalme Salman na mwanamfalme MBS.

Trump pia amezungumza nao kwa simu kisha akawaambia wanahabari kuwa hakuna ushahidi kuwa wao wanahusika. Ajabu ni kuwa hata kabla uchunguzi haujamalizika yeye atajuaje kuhusu ushahidi? Watawala wa Saudia wamesema yote haya ni uzushi mtupu na wao hawahusiki na tukio hili. Mwanzo walisema Khashoggi alimaliza shughuli zake na akatoka ubalozini.

Kama ni hivyo mbona hakuonekana? Baadae wakasema ni kweli aliuliwa hapo ubalozini lakini kitendo hicho kilifanywa na mlinzi wa mwanamfalme bila yeye mwenyewe kujua. Nchini Marekani wengi wanataka kujua ukweli.

Ni kwa sababu Khashoggi ni mkazi wa Marekani na watoto wake ni raia wa Marekani. Amehamia Marekani kwa sababu amekuwa akikosoa ufalme wa Saudia na akiwa huko amekuwa akiandika makala mbalimbali kukosoa ubalozi huo.

Nchini Marekani kuna wajumbe wa baraza la seneti ambao wamejitokeza kutoka chama tawala cha Republican na chama cha upinzani cha Democrat. Hawa wanasema kama watawala wa Saudia wanahusika na kupotea au kuuawa kwa Khashoggi basi itabidi Marekani irekebishe uhusiano wake na watawala hao.

Tayari mwenyekiti wa kamati ya seneti ya uhusiano wa kimataifa amemuandikia barua Rais Trump ikimtaka aweke vikwazo dhidi ya utawala wa Saudia. Barua hii inaungwa mkono na maseneta na wawakilishi 22 kutoka vyama vyote viwili. Trump ametamka bayana kuwa kwa vyovyote vile asingependa kuvunja uhusiano na Saudia kwani kwa kufanya hivyo ni Marekani ndio itakayoumia.

Alisema Saudia imeagiza silaha za dola bilioni 110 kutoka Marekani. Maana yake Trump anatanguliza biashara na kuweka kando uhuru wa habari na wanahabari, haki za binadamu na demokrasia. Ukiacha hiyo biashara ya silaha, Marekani imewekeza dola bilioni 55 nchini Saudia. Mwaka 2017 tu kampuni 16 kutoka Marekani ziliingia Saudia zikianzisha miradi mipya ya dola takriban milioni 100.

Halafu kuna kikundi kilichoanzishwa na rais mstaafu Clinton cha Glover Park Group kwa madhumuni ya kuwakilisha maslahi ya watawala wa Saudia nchini Marekani. Wao wanalipwa ujira wa dola 150,000 kila mwezi kwa kazi hii. Kampuni kama Lockheed Martin na Raytheon zinapata mabilioni kutokana na mauzo ya silaha bila kujali kuwa silaha hizo zimesaidia kuua raia wasiopungua 16,000 nchini Yemen.

Ni biashara hii ndiyo Trump anataka kuilinda. Lakini licha ya kampuni hizo kufaidika hata yeye binafsi amekuwa akifaidika kutokana na biashara zake na Saudia. Wakati wa kampeni yake mwaka 2015 alisema hadharani kuwa watawala wa Saudia wananunua nyumba kutoka kwake. Alisema wanamlipa dola milioni 40 hadi 50. Akaongeza, “Iweje halafu niwachukie watawala hawa? Nawapenda mno!” Hata watawala hao wanapozuru Marekani huwa wanakaa katika hoteli za Trump.

Kwa mfano, katika hoteli yake iliyo Washington kampuni inayowakilisha Saudia ililipa zaidi ya dola 270,000 kati ya Oktoba 2016 na Machi 2017 Si Trump peke yake anayefaidika na utajiri wa Saudia, bali wanasiasa na watendaji wa serikali wanalipwa ili waeneze “sifa” za Saudia (lobby). Mwaka 2015, kwa mfano, watawala hao walitoa dola milioni 18 kwa mawakala 145 wanaofanya kazi hiyo nchini Marekani.

Kwa mfano, kampuni ya Glover Park Group ilianzishwa na maofisa waliokuwa wakimtumikia Rais Clinton. Kampuni hiyo imekuwa ikilipwa dola 150,000 kila mwezi na ubalozi wa Saudia mjini Washington.

Kampuni nyingine ni BGR ambayo imekuwa ikilipwa dola 80,000 kwa mwezi. Kazi yao ni kuhakikisha magazeti yanaiandika vizuri Saudia. Pia wabunge wengi kutoka vyama vya Republican na Democrat wamekuwa wakipokea zawadi nono kutoka Saudia. Kama haya yangefanyika hapa Afrika basi wangesema ni hongo. Jambo hili linawafanya watawala wa Marekani kushindwa kuulaumu utawala wa Saudia katika kupotea kwa Khashoggi.

Ni maslahi binafsi. Na hii siyo tu Marekani bali hata nchi zingine nazo zinasita kujitokeza. Kwa mfano, Canada imekuwa ikiiuzia Saudia silaha za kivita zinazotumika dhidi ya raia wa Yemen. Mkataba wa dola bilioni 15 ulisainiwa mwaka 2014 wakati wa utawala wa chama cha Conservative. Chama hicho kikashindwa uchaguzi na sasa serikali ya Liberal inaendelea kutekeleza mkataba huo chini ya waziri mkuu Justin Trudeau.

Hata Uingereza, Ufaransa na Ujerumani nazo zimekuwa zikiiuzia Saudia silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola. Kwa kweli biashara hii imezidi kushamiri tangu Yemen kushambuliwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Ujerumani imekaa kimya baada ya kupotea kwa Khashoggi. Kwa kweli wiki moja kabla ya kupotea kwake, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani aliisifu Saudia kuwa ni “nchi inayolinda amani na utulivu katika mashariki ya kati na duniani.”

Hispania hapo mwanzo iliamua kuzuia biashara ya silaha na Saudia kutokana na mashambulizi ya Yemen. Lakini baada ya muda ikageuza uamuzi huo na sasa biashara ya silaha inaendelea.

Wakati sakata la Khashoggi linaendelea watawala wa Saudia wameitisha mkutano mkuu wa matajiri duniani kuanzia tarehe 23 hadi 25 mwezi huu. Nia ni kuwafanya waendelee kuwekeza na kufanya biashara na Saudia.

Wengi wamekubali mwaliko lakini wengine wanaona aibu kwa sababu hawataki kuchafuliwa majina yao. Wawakilishi wa serikali za Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa na IMF wamejitoa dakika za mwisho.

Huenda wengine wakajitoa na mkutano mzima sasa umo mashakani. Ni vizuri tukakumbuka kuwa Uingereza iliishutumu Urusi kuwa iliwalisha sumu raia wa Kirusi wanaoishi Uingereza, Sergei Skripal na binti yake.

Mara moja Uingereza, Marekani na nchi za magharibi ziliiwekea vikwazo Urusi na kuwafukuza mabalozi wake. Je, kama na watawala wa Saudia watathibitika katika mauaji ya Khashoggi nchi hizo zitachukua hatua gani? Au mkuki kwa nguruwe?

HIVI karibuni Wizara ya Nchi Ofi ...

foto
Mwandishi: Nizar Visram, Dar es Salaam

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi