loader
Picha

Kasi ya TRA iigwe na taasisi nyingine

SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imefanya mambo mengi katika kipindi hiki cha miaka mitatu, lakini kubwa zaidi ni jinsi inavyotatua haraka changamoto zinazojitokeza katika utendaji wa kazi wa kila siku.

Tunasema hivyo kwa kuwa hakuna kero ambayo imeachwa kufanyiwa kazi na mamlaka zinazohusika kila inapowekwa mezani.

Tumeshuhudia Rais John Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wanachapakazi usiku na mchana huku wakuu wa mikoa na wilaya wanavyotatua kero za wananchi papo kwa hapo na mawaziri wakizunguka kila kona ya nchi kwa kasi ile ile.

Ni hivi karibuni, gazeti hili lilifanya utafiti katika mitaa kadhaa ya kibiashara Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuona jinsi wafanyabiashara wanavyoihadaa serikali katika ulipaji kodi, lakini ndani ya muda mfupi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikachukua hatua mara moja.

Kutokana na utafiti wa gazeti hili ambalo linaendelea kutoa taarifa kwa jinsi linavyozipta, TRA imefanya operesheni kali ya kukamata wanaoghushi risiti za kielektroniki (EFDs) katika eneo hilo na kufanikiwa kuwatia mbaroni wafanyabiashara wadanganyifu na sasa imetangaza operesheni hiyo kufanyika nchi nzima kwa wanaoiibia serikali.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi wa mamlaka hiyo, Richard Kayombo hakusita kulieleza gazeti hili kuwa mamlaka hiyo imeamua kuifanya operesheni hiyo kitaifa na iwapo yeyote atabainika, hatua kali zitachukuliwa.

Akasema kupitia operesheni hiyo, watakaokamatwa watalipa faini, kufungwa jela au mizigo yao kutaifishwa.

Katika operesheni kali inayoendelea katika eneo la Kariakoo, wafanyabiashara na wateja wao ambao si waaminifu, tayari wamekamatwa na risiti feki huku wengine wakikutwa wakiuza bidhaa bila kutoa risiti.

Pamoja na kukamata wale ambao wanakiuka taratibu za kodi, Kayombo anasema wataendelea kutoa elimu juu ya faida ya kulipa kodi ili kuwawezesha wafanyabiashara kuona umuhimu wa kufanya biashara kwa uaminifu, weledi na umakini huku wakipata faida iliyo sahihi na serikali wka upande wake ikipewa kilicho chake.

Katika operesheni hii ya Kariakoo, Kayombo anasema wafanyabiashara wengine wamekutwa wakitoa risiti ambazo hazielezi thamani halisi iliyotolewa na mteja lakini pia wengine wanatumia risiti moja kusafirisha mizigo tofauti kwa nyakati tofauti.

Tunaamini wafanyabiashara kote nchini waelewe kwamba serikali haijalala, wachukue hatua ya kufanya biashara yao kwa umakini huku wakilipa kodi stahiki kuepuka usumbufu huo wa kufunfiwa biashara, kufungwa, kulipa faidi na adha nyinginezo.

Kwa kuwa tayari operesheni hii inaonesha mafaniko makubwa katika eneo la Kariakoo, tunaamini TRA kwa mikoa mingine itafanya kweli ili kukomesha tabia hii chafu kwa kuwa inaharibu sifa za wengine ambao wanafanya biashara kwa uadilifu.

Ni matarajio yetu kwamba, Tanzania ya viwanda inawezekana kama kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Ikumbukwe kwamba unalipa kodi kwa manufaa ya taifa zima, hivyo kukwepa kodi kwa njia yoyote ile ni kukwamisha juhudi za Rais Magufuli na serikali yake lakini pia ni kurudisha nyuma maendeleo ya taifa zima.

Tulipe kodi kwa kuinua uchumi wa taifa letu leo na vizazi vijavyo na tunazihimiza taasisi nyingine kuiga kasi ya TRA katika kutatua changamoto zinazoletwa mezani.

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi