loader
Picha

Mnada wa mifugo Kirumi utakavyonufaisha wafugaji, taifa

Serikali ya awamu ya tano iinatimiza miaka mitatu huku dhamira yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa viwanda ikitekelezwa kwa vitendo katiika sekta zote.

Uchumi huu utafikiwa ikiwa mapato ya Serikali yataongezeka kupitia usimamizi thabiti wa ukusanyaji wa mapato na maduhuli ya Serikali. Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakusudia kuongeza usimamizi na udhibiti wa upotevu wa makusanyo yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake.

Kupitia sekta ya Mifugo kwa mwaka 2018/2019, Wizara imejipangia kukusanya jumla ya Sh 50,000,000,000.00. Mojawapo ya mikakati ya kufikia lengo la makusanyo hayo ni kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo yote nchini zenye nia ya kuwafanya wafanyabiashara ya mifugo, mazao ya mifugo na pembejeo za mifugo kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Oktoba 16, 2018, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha rasmi mnada wa kimataifa wa mpakani wa Kirumi mkoani Mara ili kutoa fursa kwa wafugaji nchini kupata soko la uhakika la mifugo yao.

Mnada huo utasaidia kudhibiti utoroshaji wa mifugo mipakani kwenda nchi jirani. Katika uzinduzi wa mnada huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anawataka viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi za vijiji, wilaya kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za mifugo badala ya hali ilivyo sasa ya kuiacha ikitoroshwa kwenda nchi za nje kwa kuamini kwamba jukumu la ulinzi wa rasilimali hizo ni la Wizara ya Mifugo na Uvuvi pekee na hivyo, ikosesha serikali mapato.

Anamwagiza Katibu Mkuu wa Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabrieli kufunga minada yote ya mifugo iliyofunguliwa kinyemela kwani imekuwa kichocheo cha upotevu wa mapato ya Serikali.

Kadhalika, Waziri Mpina anawaonya wanaoanzisha minada hiyo bila kufuata taratibu zilizopo akisisitiza wachukuliwe hatua kali za kisheria. Mpina anaagiza kuanza mara moja kuihakiki minada yote nchini ili kuibaini iliyoanzishwa kinyume cha sheria ifutwe.

“Wapo watu wanafungua minada kila sehemu wanaamua tu, wakati taratibu za ufunguzi wa minada wanazijua kabisa ya kwamba ni lazima wizara iridhie kufunguliwa kwa mnada huo,” anasema.

Amesema Serikali inapotaka kuanzisha mnada inakuwa na malengo ya kuhakikisha biashara ya mifugo inafanyika vizuri na kwamba, uanzishaji holela wa minada unadhoofisha mipango inayowekwa na Serikali jambo lisilokubalika.

Waziri Mpina anasema wizara yake itaendelea na doria za mara kwa mara ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake ili kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa kwa jumla.

“Tutakuwa na makundi 14 yatakayofanya kazi kwenye kanda mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na minadani, njia kuu za kusafirishia mifugo, mipakani na njia zisizo rasmi,” anasistiza Waziri Mpina.

Anataja baadhi ya sheria zitakazotumika katika doria hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17ya Mwaka 2003 na kanuni zake za Mwaka 2010; Sheria ya Nyama Na.

10 ya Mwaka 2006 na Kanuni zake za Mwaka 2011 na Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Na. 13 ya Mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka2016. Nyingine ni Sheria ya Biashara ya Ngozi Na.

8 ya Mwaka 2008 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2010; Sheria ya Maziwa Na. 8 ya Mwaka 2004 na Kanuni zake za Mwaka 2007, Sheria ya Biashara Na. 25 ya Mwaka 1972 na Kanuni zake na Sheria ya Fedha Na.6 ya Mwaka 2001 (iliyorekebishwa Mwaka 2004) na Kanuni zake za Mwaka 2004.

“Nyingine ni Sheria ya Uhujumu Uchumi (Economic and Organized Control Crime) ya Mwaka 2002 (iliyorekebishwa Mwaka2016), Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Sheria ya Viwango Tanzania (TBS).

Anasema baadhi ya makosa ambayo wizara itachukua hatua za kisheria kuwa ni pamoja na kutolipa ushuru wa mifugo na tozo ya kibali cha kusafirisha mifugo, kutokuwa na leseni ya biashara ya mifugo na mazao yake, na kupatikana na kibali bandia.

Makosa mengine ni kuingiza mazao ya mifugo yasiyoruhusiwa nchini, kutorosha mifugo kwenda nje ya nchi-(Watatozwa faini bila kutaifishwa), kutorosha mazao ya mifugo kwenda nje ya nchi-(Watatozwa faini bila kutaifishwa) na kuuza mazao na pembejeo za mifugo zilizokwisha muda wa matumizi (expired) na zisizo na ubora.

Waziri huyo anaamini sekta ya mifugo ni muhimu katika kuongeza pato la Taifa na kwa mtu mmoja mmoja. Katibu Mkuu Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel anasema kufunguliwa kwa mnada huo kutasaidia usimamizi na kudhibiti utoroshaji wa mifugo na kuongeza mapato ya Serikali.

Anasema mnada wa Kirumi umewekwa kimkakati na unatarajiwa kuvutia wafanyabiashara wa mifugo kutoka nchi za jirani na kuliingizia taifa mapato makubwa. Waziri Mpina anawataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanapanga matumizi bora ya ardhi na kuwawezesha wafugaji kupata huduma zinazostahili ikiwemo malisho na maji badala ya hali ilivyo sasa ambapo kimakosa, baadhi ya viongozi wanaiona mifugo kama laana kwa taifa.

Anamuagiza Katibu Mkuu (Mifugo) kuanzisha haraka ofisi itakayotoa huduma ya vibali kwa watu wanaotaka kusafirisha mifugo nje ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabishara hao hulazimika kwenda hadi jijini Mwanza kufuatilia vibali hivyo.

Ameagiza kupelekwa kwa mitungi ya kupandikiza mbegu bora ya mifugo katika Mkoa wa Mara na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa gharama isiyozidi Sh 5,000 tofauti na ilivyo sasa ambapo hulazimika kugharamia hadi Sh 100,000 kupata huduma hiyo. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima anasema Serikali ngazi ya mkoa huo itaendelea kuwachukulia hatua kali watu wote wataoshiriki vitendo vya utoroshaji mifugo kwenda nje ya nchi.

Anawaonya wanaondeleza wizi wa mifugo akisisitiza kuwa, hawatapata nafasi katika kipindi hiki cha utawala wa Serikali ya Awamu Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Malima anasema tayari mkoa huo umepokea mwekezaji wa kiwanda cha maziwa kitakachokuwa na uwezo wa kusindikiza tani 200,000 kwa siku. Anasema kiwanda hicho kitakuwa ukombozi kwa wafugaji wa mkoa huo kupata soko la uhakika la maziwa yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Mara, Mrida Mshoja anasema ng’ombe walikuwa wanatoroshwa kwenda Kenya na kwamba, kufunguliwa kwa mnada huo kutawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao na kumshukuru Waziri Mpina kwa kufanikisha azima ya kuanzisha mnada huo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Makoye anasema kuanzishwa kwa mnada wa Kirumi, ni ukombozi mkubwa kwa wafugaji wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Tanzania kwa jumla kwa kuwa utatoa hamasa kwa wafugaji kunenepesha mifugo yao na kuuza bei nzuri hivyo kujipatia kipato.

Anapongeza jitihada za Waziri Mpina za kuanzisha mnada huo na Dawati la Sekta Binafsi katika Wizara hiyo litakalokuwa kiunganishi muhimu baina ya wafugaji, serikali na benki ili wapate mitaji na kuwekeza kikamilifu katika sekta hiyo tofauti na hali ya sasa.

FEBRUARI 27 kila mwaka ni siku kubwa kwa watu wa ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi