loader
Picha

Usimamizi hafifu madini ulivyoikosesha Tunduru mapato kwa miaka 21

WILAYA ya Tunduru iliyopo mkoani Ruvuma imebarikiwa na utajiri wa madini mbalimbali ya vito na endapo madini hayo yangesimamiwa tangu yalipoanza kuchimbwa mwaka 1995, serikali ingepata mapato makubwa kupitia kodi na ushuru wa madini hayo.

Afisa Madini wa Wilaya ya Tunduru, Abraham Nkya anasema Idara ya Madini imesimamia ipasavyo wanunuzi wakubwa wa madini ya vito katika wilaya hiyo ambapo kwa mara ya kwanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 wamelipa ushuru wa huduma katika Halmashauri ya Tunduru kiasi cha Sh milioni 66.

“Hatuwezi kuwalaumu wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kwa kutolipa kodi mbalimbali serikalini tangu mwaka 1995, wanaostahili kulaumiwa ni watendaji waliokuwepo madarakani katika kipindi hicho kwa kuwa walishindwa kufanyakazi ya usimamizi wa madini haya kwa mujibu wa sheria.

Usimamizi ulikuwa ni hafifu hali iliyoikosesha serikali mapato,’’ anasema Nkya. Uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya machimbo ya kata za Muhuwesi, Ngapa na Majimaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru umebaini kuwa tangu mwaka 1995 sio wachimbaji wadogo wala serikali ya mitaa na serikali kuu ambao wamenufaika kikamilifu na uwepo wa madini ya vito katika wilaya ya Tunduru.

Charles Mwasomba ni Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wilayani Tunduru anayesema uchimbaji wa madini ya vito unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo utata wa masoko ya madini hayo.

Anasema kuna wakati soko linapatikana kwa shida kutoka na uweli kwamba madini yanayopatikana Tunduru ni madogo madogo aina ya safaya. Hata hivyo, anasema wanunuzi wengi wa madini kutoka nchini Sirilanka na Thailand wanapenda madini makubwa aina ya kristobei na Alezander ambayo yanapatikana Tunduru lakini ili kuyachimba yanahitaji mtaji na vifaa vya kisasa ambavyo wachimbaji wengi wadogo hawana.

“Wachimbaji wengi wadogo wanachimba madini ya safaya ambayo wanunuzi wake wanapatikana kwa msimu, hali ambayo inasababisha wachimbaji kukosa soko la uhakika na kusababisha wakati fulani kujikuta mtu unakata mtaji na kuishi maisha magumu,’’ anasema Mwasomba.

Castroy Makiwa, Mchimbaji mwingine mdogo eneo la Muhuwesi, Tunduru anaitaja changamoto ya masoko katika madini ya vito kuwa ni kubwa na hivyo anaiomba serikali kuona namna ambavyo itahamasisha soko la uhakika kwa wachimbaji wadogo wa Tunduru.

Kadhalika anakiri kwamba wachimbaji wadogo wanatumia vifaa duni vya sululu na chepe, hali ambayo inasababisha uchimbaji kuwa mgumu na hivyo anaomba serikali iangalie namna inavyoweza kuwasaidia.

Makiwa anasisitiza kuwa bei ya madini pia haina uhakika kutokana na ukosefu wa masoko na kwamba mchimbaji anapopata madini yake huwa hana uhakika kwamba atauza kwa bei gani na kwamba imekuwa ni bei ya kukadiriwa zaidi.

“Leo unaweza kuuza gramu ya vito shilingi 7,000, kesho ukashangaa gramu hiyo hiyo unauza shilingi 3,000, kwa hiyo biashara ya madini ya vito haina uhakika. Hakuna vipimo vya uhakika zaidi ya vipimo vya kupima pointi na gramu na kuanza kukadiria bei, hivyo huwezi pia kujua madini haya nitapata shilingi ngapi,’’ anasema Makiwa.

Kwa upande wake, Mohamed Abdul Karim, mchimbaji mdogo katika eneo la Ngapa wilayani Tunduru anasema wachimbaji wadogo waliopo Tunduru ni tofauti na wachimbaji waliopo katika migodi mingine Tanzania kwa sababu wanafanya uchimbaji wa sensa katika mabonde ya mito likiwemo bonde la mto Muhuwesi na Ngapa.

Hata hivyo, anasema tamko la serikali la kuagiza wachimbaji hao kutoka nje ya mto na kwenda kuchimba nchi kavu linawaletea changamoto kwa sababu wachimbaji hao hawana vifaa bora, hali ambayo inaathiri mapato.

Anasema hata wanunuzi wa madini hayo wanategemea madini ambayo yanachimbwa na wachimbaji wadogo katika mabonde ya mito. “Naiomba serikali ituruhusu kuendelea kuchimba kwenye mabonde ya mito kwa sababu uchimbaji wetu wa kutumia sululu na chepe hauwezi kuharibu mazingira, uchimbaji wa madini ya vito hautumii mashine kubwa kama ilivyo katika migodi mingine.

Tukichimba mvua ikinyesha ile sehemu iliyochimbwa inajifukia,’’ anasema Karim. Anasema uchimbaji wa nchi kavu unahitaji vifaa vya kisasa pamoja na vifaa ambavyo vinaweza kuangalia madini yapo umbali gani sambamba na mtaji wa kutosha, jambo ambalo wachimbaji wadogo hawana uwezo huo.

Mrisho Ally Mrisho, mchimbaji mdogo anayeishi katika kijiji cha Majimaji wilayani Tunduru, anatoa rai kwa serikali kuwasikiliza wachimbaji wadogo katika wilaya hiyo ambao anasema wameanza kuchimba tangu mwaka 1995 lakini mpaka sasa hawajanufaika ipasavyo na uwepo wa madini ya vito katika wilaya hiyo.

Anasema manufaa kwa miaka yote hiyo hayapo kwa sababu uchimbaji unaofanyika ni mdogo unaoanza kipindi cha kiangazi kuanzia mwezi Juni hadi Desemba. Anafafanua kwamba wanachimba wakati wa kiangazi kwa sababu wakati wa masika uchimbaji huwa mgumu.

“Wanunuzi wa madini ya vito wanaofika kununua madini haya katika wilaya ya Tunduru wanatoka nchi za Thailand na Sirilanka. Kwa bahati mbaya wao ndio wanapanga bei na sasa hapo hatuna kauli,’’ anasema Mrisho.

Mrisho anashauri Wizara ya Madini kufika katika wilaya ya Tunduru ili kutoa elimu endelevu ya kutambua madini ya vito kwa sababu wachimbaji wanafanyakazi ya uchimbaji bila kuwa na elimu sahihi ya madini.

Mrisho pia anashauri Wizara ya Madini iwakutanishe wachimbaji wadogo na wanunuzi wa kati na wakubwa wa madini wakati wa kutoa elimu hiyo. Anasisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wa kisasa na kuzifahamu aina mbalimbali za madini kwa sababu wilaya ya Tunduru inachimba aina mbalimbali za madini ambazo wachimbaji wengi hawazijui aina zake, ubora na thamani zake, hali ambayo inasababisha kuendelea kunyonywa na wanunuzi wajanja,’’ anasisitiza Mrisho.

Uchunguzi umebaini kuwa wachimbaji wadogo wengi wa Tunduru, licha ya kuanza kuchimba madini tangu mwaka 1995 hadi sasa bado hali zao ni duni. Moja ya sababu iliyochangia hali hiyo ni kwamba wachimbaji wanapata madini ambayo hawatambui thamani yake na soko lake kwani anayejua thamani ya madini hayo ni mnunuzi ambaye amemwacha huru na kwamba mnunuzi huyo anaweza kukudanganya ili kunufaika na madini hayo.

Wachimbaji wadogo wanatoa rai kwa serikali kuwawezesha vifaa na mtaji kama kweli imedhamiria uchumi wa madini kumilikiwa na watanzania. Katibu wa Wachimbaji wadogo katika Wilaya ya Tunduru, Expedito Mdululu anasema wachimbaji wadogo wameanzisha vikundi vyao ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Katibu huyo ambaye hadi sasa ana miaka 23 ya uchimbaji wa madini katika wilaya ya Tunduru, anatoa rai kwa serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji cha Taifa kuitazama kwa macho matatu Wilaya ya Tunduru.

Anahimiza wenye mitaji kwenda Tunduru ili kuwekeza katika sekta ya madini ambayo anakiri kwamba bado haijawanufaisha watanzania. “Wilaya ya Tunduru ina utajiri wa karibu aina zote za madini ya vito isipokuwa tanzanite. Madini yaliopo Tunduru ni safaya, Alexanderyte, Krizobery, almasi, dhahabu, pink safaya, blue safaya, topaz, wats, spinery, Changecoureganet, redganet, silicon, Rubi na madini mengineyo mengi,’’ anasema Mdululu.

Akizungumzia umilikishwaji wa leseni za madini kwa wachimbaji wadogo Mdululu anasema,wachimbaji hao walimilikishwa kihalali leseni za uchimbaji katika Bonde la mto Muhuwesi kupitia Ofisi ya madini ya Kanda ya Kusini na kwamba wameletewa taarifa kuwa hivi sasa hawaruhusiwi kuchimba maeneo ya mto huo kwa madai ya kuharibu mazingira ya mto.

“Sisi uchimbaji wetu ni mdogo sana tunatumia mikono yetu kwa kusaidiwa na vifaa vya sululu na chepe na uchenjuaji wetu hautumii kemikali hatarishi kama zebaki, wanatuambia tunasababisha kina cha maji ya mto kupungua na kuwaua wadudu wanaoishi kwenye maji, lakini mvua zikinyesha wala huwezi kujua kama palichimbwa,’’ anasema Mdululu.

Katibu huyo wa Wachimbaji wadogo anaiomba serikali kuwaruhusu kuchimba kwa kuwa leseni zao zinawaruhusu na kwamba wamewekeza kwa gharama kubwa katika uchimbaji kwa miaka mingi hivyo kuwakataza kuchimba katika bonde la mto Muhuwesi ni kuwaingiza katika umaskini. Serikali kupitia Idara ya Madini imeagiza uchimbaji wa madini kwenye bonde la mto Muhuwesi kufanyika kati ya mita 60 hadi 100 nje ya mto, hali ambayo inaleta changamoto kwa wachimbaji hao wadogo.

KATI ya nchi zinazokuja kwa kasi katika kuboresha sekta ya ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi