loader
Picha

Tushirikiane kuhifadhi vyura wa Kihansi

ILIRIPOTIWA hivi karibuni kuwa vyura wa aina ya pekee, wanaopatikana nchini Tanzania tu, zaidi ya 9,800 wamerudishwa maeneo yao ya asili ya Kihansi katika safu za Milima ya Udzungwa mkoani Morogoro kutoka Marekani.

Tunawapongeza wataalamu wetu kwa hatua hiyo kubwa. Tunafahamu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wataalamu wetu waliwachukua vyura 500 wa awali Kihansi na kuwapeleka Marekani kwa ajili ya kuwahifadhi katika maabara maalumu, kutokana na tishio la kutoweka.

Hakuna ubishi kwamba kazi iliyofanyika kutoka vyura hao 500 waliopelekwa kuhifadhiwa na kisha kurejeshwa hao zaidi ya 9,800, ni hatua kubwa mno.

Ni hatua kubwa na ya kipekee, inayostahili kupongezwa na kuendelezwa na kila mtu ili viumbe hao adimu, waweze kuendelea na kuongezeka kwa manufaa ya Taifa letu na watu wengine duniani kote wenye mapenzi mema na viumbe wa aina hii.

Wakati juhudi hizo za uhifadhi wa viumbe hao adimu duniani zinaendelea, tunatoa mwito maalumu kwa wananchi wa mikoa ya Iringa na Morogoro, yaliko makazi ya vyura hao waliorejeshwa katika maeneo yao ya asili ya Kihansi, kutoa kila ushirikiano unaohitajika.

Hatua hiyo itawezesha juhudi za kuwahifadhi, zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wataalamu wetu, zisivurugwe.

Pia tunapongeza juhudi zinazofanywa na wataalamu wetu, kwa kutaka eneo hilo la asili wanaloishi vyura hao yaani Kihansi, kuwa katika mchakato wa kuwa eneo la hifadhi.

Hatua hiyo itawezesha eneo hilo kuendelea kuwa na viumbe hao kwa muda mrefu zaidi.

Tunaomba kuwa mtu yeyote atakayekuwa kikwazo katika mikakati hii muhimu ya kuhifadhi viumbe hao, asipewe nafasi. Tunapendelea kuwa wale watakaojaribu kufanya hivyo, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Tunasisitiza kwamba wataalamu wetu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), waendelee kushirikiana na kushikamana, kufuatilia kwa umakini maisha ya vyura hao adimu.

Taasisi hizi muhimu na zenye wataalamu wa kazi hiyo, zipewe ushirikiano wa kila aina katika kutekeleza majukumu yao ya kuhifadhi vyura hao adimu kwa gharama yoyote ile.

Kwa ujumla, kwa kuwa vyura hao ni adimu na wanapatikana Tanzania tu, kama madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee, tunapendekeza kuwa kama inawezekana, iundwe taasisi rasmi ya kusimamia hifadhi ya vyura hao wa Kihansi. Zipo faida lukuki za kuwahifadhi viumbe hao adimu.

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi