loader
Picha

Watahiniwa kidato cha 4 waandaliwe kisaikolojia

JUMATATU Novemba 5, 2018 wanafunzi wa kidato cha nne katika shule mbalimbali za sekondari nchini wataanza kufanya mitihani yao ya mwisho.

Tunawapongeza walimu, wazazi na walezi wao kwa kazi kubwa ya malezi waliyoifanya hadi kuwafikisha katika kilele hiki cha masomo ambacho pia, ndicho mwamuzi wa hatima yao kielimu kwa siku za usoni.

Kadhalika, tunawapongeza watahiniwa kwa safari ndefu yenye milima na mabonde inayolenga kujenga maisha yao, familia na taifa kwa jumla kunufaika kuwa na wasomi na wataalamu katika fani mbalimbali.

Tunasema ni milima na mabonde kwa kuwa hakuna asiyejua ugumu uliopo ndani ya safari nzuri ya elimu likiwamo suala la nidhamu na uadilifu hivyo, kuhitimu si jambo la mzaha, bali linalohitaji juhudi na pongezi.

Ingawa tunaamini vijana hao wameandaliwa vya kutosha, lakini tunasema malezi hayana mwisho hivyo, wazazi, walezi na hasa walimu wanao wajibu kuendelea kushirikiana kuwalea na kuwaandaa zaidi ili wanapoingia katika mtihani, waingie wakijiamini kwamba wanakwenda kufanya vizuri na kushinda katika mitihani, na siyo kushindana wala kushindwa.

Mbali na kuandaliwa zaidi kisaikolojia kukabiliana na mitihani kwa ari ya ushindi, pia waimarishwe kuzingatia uadilifu na utii kabla, wakati na baada ya mitihani yao ili usemi kuwa: “Kamba hukatikia pembamba” usipate nafasi kwao.

Miongoni mwa mambo tunayopenda kushauri yaendelee kufanywa na walimu, ni pamoja na hasa kuzidi kuwajenga, kuwatia moyo, kuwaondoa ‘homa ya mtihani’ na kuwapa mbinu sahihi na halali za kujibu mitihani kwa usahihi ili wafaulu.

Hizi ni pamoja na kuwa na vifaa vya kutosha, mwandiko mzuri, uchaguzi sahihi wa maswali ya kuanza kujibu, nidhamu na matumizi sahihi ya muda na kuwa makini katika kufuata maagizo na maelekezo ya wasimamizi wa mitihani, na mitihani (maswali) yenyewe. Tunasema, waendelee kuhimizwa kujisomea badala ya kuwaacha wengine wapotoshane kwa usemi kuwa:

“Ng’ombe hanenepi siku ya mnada” unaotumiwa mara nyingi na wanafunzi au watu wazembe kupotosha maana kusudiwa.

Tunasema, muda wa siku mbili au tatu zilizosalia, usitumike kuwaangamiza watoto kwa baadhi ya watu wakiwamo baadhi ya walimu wasio waadilifu na wasimamizi wa mitihani, kujaribu kuwafundisha au kuwashirikisha wanafunzi mbinu za udanganyifu katika mitihani kwani kufanya hivyo, ni kuwachimbia kaburi la maisha na pia, kujihatarisha wenyewe.

Sisi tunaamini walimu na wanafunzi kwa muda wote wametimiza wajibu wao vema na hivyo, muda uliobaki ni wa kukamilisha hivyo, hakuna sababu ya wanafunzi kuwa na hofu, wala walimu kuwajaza hofu kiasi cha wengine kuwashawishi kushiriki udanganyifu.

Ni matamanio yetu kuona na kusikia mitihani ya kidato cha nne mwaka huu imemalizika, bila kuwapo udanganyifu, wala upuuzi wa watahiniwa kuchora ‘mazombi’ maana tunaamini kuwapo kwao sekondari hakukuwa ajali wala bahati mkosi, bali walichaguliwa kutokana na uwezo wao, hivyo watafanya vizuri na watafaulu zaidi.

Kwa hiyo, muda wa siku mbili tatu uliobaki, watahiniwa kidato cha nne waandaliwe zaidi kielimu na kisaikolojia kufanya vizuri zaidi.

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi