loader
Picha

Wanaoendesha kwenye makazi ya watu wabanwe kuepusha ajali

MITAANI ndipo tunapoishi, tunapokutana na familia zetu na kufurahia utulivu wa nyumbani baada ya harakati mbalimbali za kutafuta maisha, ingawa utulivu huu unaonekana kuleta hofu miongoni mwa wakazi kutokana na maendeleo tuliyoyasubiri kwa muda mrefu ya kujengewa barabara kwa kiwango cha lami. Barabara hizi ambazo zimejengwa katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam linalokadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 4 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na maendeleo ya ujenzi wa barabara za mitaani, bado jiji hili linakabiliwa na changamoto za miundombinu kutokana na ongezeko la watu, hasa ikizingatiwa kuwa takriban asilimia 75 ya maeneo ya makazi ambako barabara hizi zinapita hayajapimwa. Ni kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuanzisha mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam yaani Dar es Salaam Metropolitan Project au (DMDP) kwa manispaa zote za jiji ili kuboresha maeneo ya watu wenye kipato kidogo yaliyojengwa holela kwa makubaliano kati ya serikali na Benki ya Dunia.

Manispaa ya Ilala yenye eneo la zaidi ya kilometa za mraba 300 na wakazi wapatao milioni 1.2, imetengewa Sh bilioni 115 kwa mradi wote ambao unaendelea kutekelezwa kwa awamu mbili za miaka mitano mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2025. Taarifa kutoka Manispaa ya Ilala iliyothibitishwa na Ofisa Uhusiano, Tabu Shaibu, inaeleza kuwa hadi sasa manispaa hiyo imeingia mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 49.84 katika kujenga kilometa 25.84 za barabara za mitaani kwa kiwango cha lami.

Barabara hizi ni chachu ya maendeleo, lakini kutokana na ujenzi holela wa makazi kumekuwa na changamoto mbalimbali za kiusalama kwa baadhi ya barabara ambazo zinaonekana ni nyembamba na kusababisha madereva kuendesha katikati, kuegesha gari barabarani au mbele ya nyumba zilizo karibu na barabara.

Miongoni mwa wakazi wanaoishi kando ya barabara katika eneo la Mongolandege Mpera, aliyejitambulisha kwa jina moja la Dominata au mama Brian, ameelezea wasiwasi wake kutokana na hali ya usalama katika eneo hilo, kutokana na ujenzi unaoendelea kwa kukosa njia za watembea kwa miguu.

“Pamoja na kuwa ujenzi haujakamilika, kwa sasa tumekuwa tukishuhudia ajali kutokana na matumizi holela ya barabara, ambapo watembea kwa miguu wamekuwa wakichanganyika na vyombo vya moto kama magari, bajaj na pikipiki ambavyo baadhi ya madereva hawako makini na hivyo kuongeza hatari ya kutokea kwa ajali,” alisema Mama Brian.

Trafiki akichukua maelezo baada ya kutokea ajali barabarani.

Mkazi mwingine Kuluthum, ambaye ni mama lishe jirani na eneo la Shule ya Msingi Mongolandege ambapo barabara inaonekana kuwa nyembamba na kona kali, amesema watoto wapo kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na ajali kama mamlaka husika hazitachukua hatua za usalama barabarani, ikiwemo kuweka matuta katika eneo hilo.

Mhandisi John Magori, ambaye pia ni msimamizi wa miradi ya DMDP katika Manispaa ya Ilala amekiri kuwepo na changamoto za usalama barabarani katika maeneo ambayo mradi unaendelea kutekelezwa kwenye kata mbalimbali zikiwemo za Ukonga, Kiwalani na Gongo la Mboto. “Ni kweli baadhi ya barabara ni nyembamba na maeneo mengine kuna kona kali, ni matarajio yetu kuwa kampuni zinazofanya kazi ni za viwango vya kimataifa zitazingatia usalama wa watumiaji kwa kuweka alama za barabarani katika maeneo husika pindi mradi utakapokamilika,” alisema Magori.

Aidha mhandisi huyo wa manispaa ya Ilala amelitaka jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kuendelea kuwasaidia kutoa elimu, ingawa kampuni hizo pia zimekuwa zikitoa elimu ya usalama barabarani kwenye kata na serikali za mitaa kwa kuwa moja ya vigezo kwa wataalamu hao ni kuzingatia suala la usalama na utunzaji wa mazingira.

“Elimu ni muhimu itolewe kwa watumiaji wa barabara, hasa madereva wazembe wanaoendesha kwa kasi bila kuzingatia usalama. Tunatarajia maeneo haya kuwekwa matuta na vibao vinavyoelekeza punguzo la mwendo kasi usiozidi kilomita 50 kwa saa na yale yenye kona kali au vivuko, mwendo kasi uwe kati ya kilomita 10 hadi 30 kwa saa,” alisema. Kumekuwa na ongezeko la matumizi ya vyombo vya usafiri, zikiwemo bodaboda na bajaji ambazo kiuchumi zimeongeza soko la ajira kwa vijana wengi, lakini pia magari yameongezeka yakiwemo yale yanayochepuka kutoka njia kuu kwa kukwepa foleni, hali ambayo inachangia hatari ya ongezeko la ajali kwa wakazi wanaoishi kando ya barabara hizi.

Suala la elimu ya matumizi bora ya barabara linaungwa mkono pia na Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoani Dar es Salaam, George Tarimo pale aliposisitiza kuhusu sera ya serikali katika kutoa elimu. “Uzoefu unaonesha ajali nyingi kwenye maeneo haya zimekuwa zikisababishwa na madereva wa bodaboda ambao wengi hawana leseni, hawajui umuhimu wa kuvaa kofia ngumu kwa ajili ya usalama lakini wengine wanaendesha wakiwa wamelewa,” anasema Mhandisi Tarimo.

Mratibu huyo wa Tarura ameongeza kuwa, baadhi ya madereva wanaoendesha mitaani hawafuati sheria, aidha kwa kupuuza au kwa kutozijua na kinachoongeza hofu ni kuona kama vile madereva hao wako juu ya sheria kwa kuendesha vyombo hivyo wanavyojisikia. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia kwa Mkuu wa kitengo cha sheria cha jeshi hilo, Deus Sokoni, kimepongeza hatua ya serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara katika manispaa za jiji la Dar es Salaam, lakini akasisitiza adhabu kali dhidi ya madereva wazembe wanaokiuka kwa makusudi sheria na hivyo kuwa chanzo cha ajali na kusababisha uharibifu wa mali, majeraha na vifo.

Aidha Kamanda Sokoni ameelezea changamoto mbalimbali zinazolikabili jeshi hilo kikosi cha usalama barabarani, ikiwemo idadi ndogo ya askari ambapo kwa mujibu wa takwimu za jeshi hilo uwiano uliopo ni (1:17,000) yaani askari mmoja kwa watu elfu kumi na saba. Kutokana na maeneo haya kukosa usimamizi wa askari wa usalama barabarani, kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria ikiwemo kutoheshimu watembea kwa miguu wanaovuka barabara hasa wazee na watoto kwenye maeneo ambayo hayajawekwa alama za kuvukia.

“Utaona ni jinsi gani tunavyokabiliana na tatizo hili, kwani idadi ya askari wa usalama barabarani tulionao kwa nchi nzima ni takriban 5,000, hivyo sio jambo rahisi kusambaza askari katika barabara zote na ndio maana tunasisitiza madereva wafuate sheria ili kuwapa haki watumiaji wengine wa barabara na endapo tutakukamata kwa makosa ya uzembe tutakushughulikia,” alisisitiza

FEBRUARI 27 kila mwaka ni siku kubwa kwa watu wa ...

foto
Mwandishi: Adam Lutta

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi