loader
Picha

Wanaoendesha kwenye makazi ya watu wabanwe kuepusha ajali -2

KATIKA toleo lililopita, mwandishi wa makala haya, ADAM LUTTA aliishia katika kipengele kinachoonesha kuwa, uwiano wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ni 1:17,000 yaani askari mmoja kuhudumia watu 17,000. Endelea.

Kutokana na maeneo haya kukosa usimamizi wa askari wa usalama barabarani, kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria, ikiwemo kutoheshimu watembea kwa miguu wanaovuka barabara hasa wazee na watoto kwenye maeneo ambayo hayajawekwa alama za kuvukia.

“Utaona jinsi tunavyokabiliana na tatizo hili, kwani idadi ya askari wa usalama barabarani tulio nao kwa nchi nzima haikidhi mahitaji halisi, hivyo sio jambo rahisi kusambaza askari katika barabara zote,” anasema Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Deus Sokoni ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Kikosi cha Usalama barabarani.

Anaongeza: “… Ndio maana tunasisitiza madereva wafuate sheria ili kuwapa haki watumiaji wengine wa barabara na endapo tutamkamata mtu kwa makosa ya uzembe, tutakushughulikia.” Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi nchini, kwa kipindi cha mwaka 2017, watuhumiwa 2,524,042 walikamatwa kwa makosa ya usalama barabarani yaliyosababisha vifo 2,705 na majeruhi 6,169 kutokana na ajali.

Hata hivyo, jeshi hilo limekuwa likijitahidi kutoa elimu ya usalama barabarani kwa jamii katika maeneo ya wazi na katika mikusanyiko ya watu kama vile kwenye vituo vya mabasi au katika shule na kuwasaidia wanafunzi kuvuka barabara katika maeneo yaliyo jirani na shule hizo. Mwalimu kutoka Kitengo cha Elimu kwa Umma katika Kikosi cha Usalama Barabarani, Sajini Happy anasema pia wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kufikisha elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari vya umma na hata vile vya binafsi zikiwemo redio na televisheni.

“Kuhusu usalama wa wanafunzi katika maeneo ya shule, huwa tunatumia vipeperushi na vibao vinavyowawezesha kujisimamia wenyewe wakati wa kuvuka barabara vijulikanavyo kama ‘Junior patrol,’ lakini pia kuwaandalia maswali na mashindano mbalimbali kuhusu usalama wao wawapo barabarani,” anasema.

Uendeshaji wa kizembe ni hatari haijalishi unaendesha maeneo gani ingawa hakuna sehemu hatari zaidi kwa dereva mzembe kama kuendesha katika makazi ya watu. Kuendesha kwa usalama ni muhimu muda wote unapokuwa kwenye chombo cha moto iwe ni katika barabara za mitaani au barabara kuu, ingawa kuendesha kwenye barabara zilizo katika makazi ya watu kunahitaji umakini zaidi kwa vile maeneo hayo mara nyingi kuna watembea kwa miguu na watoto wanaocheza.

Maisha ya familia moja yanaweza kubadilika kabisa kutokana na uzembe uliofanywa na dereva awe wa gari au bodaboda kuendesha katika makazi ya watu bila kufuata kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Kimsingi, ajali za mara kwa mara zinazosababisha vifo au majeruhi katika maeneo haya husababishwa na madereva wazembe wanaoendesha kwa kasi bila kuzingatia hali halisi ya maeneo hayo. Ndiyo maana madereva wanashauriwa waendeshe kwa mwendokasi usiozidi kilomita 50 kwa saa au kilomita 20 hadi 40 kwa saa pale ambapo hakuna alama inayomuongoza. Uchunguzi unaonesha kuwa, madereva wengi wanaoendesha katika maeneo haya hawazingatii kanuni za usalama ikiwemo mwendokasi.

Kadhalika, wapo waendesha bodaboda na baadhi ya abiria wasiotaka kuvaa kofia ngumu ili kujiepusha na madhara makubwa pindi ajali inapotokea. Ripoti ya matukio ya usalama barabarani ya mwaka jana iliyotolewa na Jeshi la Polisi, inaonesha kuwa asilimia 86 ya ajali zote nchini ni matokeo ya makosa madogo madogo ya kibinadamu. Makosa haya husababishwa na uzembe mbali na makosa yatokanayo na ubovu wa vyombo ambayo ni asilimia 8 na sababu nyingine za miundombinu ya barabara zikichangia kwa asilimia 6.

Makosa madogo madogo ya usalama barabarani yaliyozoeleka katika maeneo ya makazi ya watu ni pamoja na kuegesha vibaya na kutofunga mikanda. Aidha, makosa mengine ni kutokuwa na vizuizi vya kuwakinga watoto wawapo ndani ya vyombo vya usafiri, mwendo kasi, kutozingatia alama za barabarani, kutumia simu wakati wa kuendesha na kuendesha bila ya leseni.

Wengine huendesha kwa mbwembwe bila kuzingatia ubora wa vyombo wanavyoviendesha, kutovifanyia ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara, na wengine kuendesha wakiwa wamelewa hasa wale wenye tabia za kupita kwenye baa za karibu wanaporejea nyumbani wakiamini wameshatoka kwenye barabara kuu. Hao, hawazingatii athari zinazoweza kutokea kwa kuendesha wakiwa wamelewa.

Hii si kwa madereva wa magari pekee, bali hata waendesha bodaboda ambao ndio usafiri mkubwa unaotumiwa na wakazi wengi wa maeneo haya. Kwa kipindi cha mwaka jana, ajali 223 za bodaboda ziliripotiwa na Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Ilala na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 207. Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani Dar es Salaam, Mhandisi George Tarimo anasema ajali hizo ambazo mara kwa mara husababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva.

Anasema wengine huendesha wakiwa wametumia kilevi ikiwemo pombe maarufu ya ‘viroba.’ Ingawa ipo sheria nchini inayoruhusu dereva kuendesha akiwa ametumia kilevi kwa kiwango kilichoruhusiwa kisheria ambacho kitaalamu kinasomeka (0.08g/dl), bado kiwango hicho ni kikubwa ukilinganisha na kile kilichopitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) cha (0.05g/dl).

Ikumbukwe kuwa, wapo baadhi yao wanaotumia pombe za kienyeji kama gongo zisizopimwa kitaalamu. Meneja wa Tarura katika Wilaya ya Ilala, Samwel Ndoveni anatoa rai kwa watumiaji wa barabara za mitaani kutopuuzia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ongezeko la ajali. “Suala la kulipwa fidia ili kupisha upanuzi wa barabara linategemea na aina ya mradi kwani kuna miradi yenye fungu linaloruhusu fidia na mingine fungu haliruhusu.”

“Kwa mradi wa DMDP, siwezi kuuzungumzia kwa kuwa hatujakabidhiwa rasmi japo kuna maelekezo huo mradi uje Tarura ila kwa sasa bado tunasubiri mwongozo,” anasema Ndoveni.

Meneja huyo anaongeza kuwa, sasa wanaendelea na utekelezaji wa miradi yote ya ukarabati wa barabara inayofadhiliwa na Road Fund.

KATI ya nchi zinazokuja kwa kasi katika kuboresha sekta ya ...

foto
Mwandishi: Adam Lutta

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi