loader
Picha

JPM na mafanikio ya TRA katika ukusanyaji mapato

UJENZI wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kutoka Morogoro hadi Dodoma na baadaye kufi ka Mwanza na Kigoma, ni moja kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu Tano chini ya Rais John Magufuli.

Katika kipindi cha miaka mitatu sasa, Serikali ya Awamu ya Tano, imefanya mambo mengi na makubwa ya kimaendeleo kwa wananchi ukiwemo ujenzi wa reli hii inayokuza matumaini ya Watanzania mintarafu kupata uhakika wa usafiri utakaoboresha maisha na shughuli zao.

Kukamilika kwa mradi huu, kutafungua fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi ndani na nje ya nchi kwa kuwa Tanzania inapakana na nchi nyingi ikiwemo Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Malawi.

Kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Ujenzi wa mradi huu ulianza Mei, 2017 baada ya Rais Magufuli kuuzindua Aprili 12,2017 katika Stesheni ya Pugu na unajengwa na Kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkezi kwa ubia na Kampuni ya Mota-Engil Africa ya Ureno.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ina urefu wa kilomita 205 ikijumuishwa na kilomita 95 za njia za kupishania treni, hivyo kufanya reli yote kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuwa na urefu wa kilomita 300.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogo- sa, anasema ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 32 na kwa kipande cha kutoka Morogoro kwenda Dodoma, ujenzi huo umefikia asilimia 4.

Kadogosa anasema ujenzi wa reli yote kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utagharimu Sh trilioni 7 ambazo ni fedha za Serikali. Miongoni mwa kazi zinazoendelea kufanyika katika kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ni ulazaji we reli kwenye mataruma katika eneo la Soga mkoani Pwani.

Kazi hii ya ulazaji mataruma ilianza Septemba mwaka huu baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kufanya uzinduzi rasmi. Katika uzinduzi huo, Waziri Kamwelwe anasema ujenzi wa reli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia ahadi iliyotolewa na chama hicho wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Maizo Mgedzi, anamweleza Waziri kuwa tani 7,250 za vyuma vya reli hiyo kutoka kampuni ya NIPPON ya Japan, vinatosha kulazwa katika umbali wa kilomita 60 na kuongeza kuwa, tani nyingine za vyuma vya reli zaidi ya 7,000 zingewasili mwezi uliopita.

Katika hilo, Kadogosa anasema hadi sasa zaidi ya kilomita 15 zimeshalazwa kwenye reli na kazi inaendelea. Mbali na ulazaji wa reli kwenye mataruma hayo, HabariLeo limeshuhudia kazi nyingine za ujenzi kama vile ujenzi wa madaraja, mitaro na utengenezaji wa mataruma ya zege zikiendelea eneo la Soga mkoani Pwani. Ubora wa reli Mgedzi anasema ubora wa reli ya kisasa inayojengwa Tanzania uko juu ikilinganishwa na ubora wa reli zilizoshajengwa katika baadhi ya nchini barani Afrika.

Anazitaja baadhi ya nchi barani Afrika zilizojenga reli ya kisasa (SGR) kuwa ni Ethiopia, Afrika Kusini, Kenya na Morocco. Anasema, reli zilizojengwa katika nchi hizo, zina uwezo wa kupitisha treni zenye mwendokasi wa kilomita 120 kwa saa tofauti na reli inayojengwa hapa nchini itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zenye mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa.

“Reli tunayojenga itatumia treni za umeme tofauti na nchi nyingine nyingi ambazo treni zao zinatumia mafuta ya dizeli. Pia, reli yetu itakuwa na uwezo wa kupishanisha treni zenye urefu wa kilomita mbili tofauti na nchi nyingine ambazo treni zao hazizidi kilomita moja. “Kwa hiyo, viwango vya ubora wa reli tunayojenga hapa nchini viko juu ikilinganishwa na nchi nyingine,” anaeleza Mgedzi.

Uwezo wa reli Kwa kuzingatia viwango vya ubora, reli hii itakuwa na uwezo wa kupitisha mzigo wa tani kati ya milioni 17 hadi 25 kwa mwaka ikilinganishwa na reli ya sasa ambayo uwezo wake wa kupitisha mizigo kwa mwaka ni tani milioni tano tu.

Kuhusu abiria, Mgedzi anasema kuwa kutokana na urefu wa njia za kupishanisha treni, reli hii inaweza kusafirisha kiwango kikubwa cha abiria lakini kwa kuanzia itakuwa ikisafirisha abiria wasiopungua milioni 1.2 kwa mwaka.

Idadi ya stesheni Reli hii ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakuwa na jumla ya stesheni sita ambazo ni Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro.

Ujenzi wa uzio Ili kuhakikisha watu wanakuwa salama na treni nayo inafanya safari zake kwa usalama muda wote, TRC imekusudia kujenga uzio kuanzia mwanzo hadi mwisho wa reli hii. Uzio huu umeelezwa kuwa utasaidia kuzuia ajali kutokana na watu na wanyama kukatisha reli.

Mbali na kuepusha ajali, Mgedzi anasema kwa kuwa reli hii itahusu matumizi ya mifumo ya umeme, inaweza kuwa hatari pia kwa watu kama uzio hautajengwa. Ujenzi wa daraja Ilala Meneja Msaidizi wa mradi huo wa TRC, Machibya Masanja, anasema ujenzi unaoendelea wa daraja lenye urefu wa kilomita 2.8 kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Barabara ya Mandela karibu na Kiwanda cha Bakhresa, utasaidia kuepusha ajali kati ya treni, magari na watembea kwa miguu.

Anasema daraja hili litakuwa na nguzo 100 za zege. Gazeti hili limeshuhudia nguzo hizo zikianza kuwekewa kofia zake ili kuziunganisha. “Kwa jumla kutakuwa na madaraja 25, lakini pia kutakuwa na madaraja 18 ambayo reli itapita juu na barabara kupita chini, madaraja mengine ambayo reli itapita chini na barabara kupita juu yatakuwa 30, na madaraja ambayo ni reli juu ya reli (SGR na reli ya zamani) yatakuwa matano, wakati idadi yote ya makaravati yaliyounganishwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yatakuwa 246,” anaeleza Masanja.

Mfumo wa umeme Kwa kuwa uendeshaji wa reli hii ya kisasa utahitaji kiasi kikubwa cha umeme wa hadi KVA 220 ambazo zitapunguzwa hadi kufikia KVA 25 kwa ajili ya matumizi, kutajengwa njia ya umeme inayojitegemea ili kuendeshea treni na kukidhi mahitaji mengine ya uendeshaji wa mradi huu.

Masanja anasema njia hii ya umeme haitaingiliana na shughuli nyingine za mfumo wa umeme wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco). Anafafanua kuwa kutajengwa mitambo mingine ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia inayozalishwa hapa nchini.

Umeme unaozalishwa kwa gesi utasaidia uendeshaji wa mradi huu ikiwemo treni za umeme kupatikana wakati wote hata kama umeme wa Tanesco utakuwa umekatika au kutokea dharura yoyote ile.

Idadi ya safari Dar-Moro Kwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya usafiri, kukamilika kwa mradi huu kutawezesha kuwepo kwa treni tatu za abiria kama hatua ya mwanzo zitakazokuwa zikienda na kurudi kati ya Dar es Salaam na Morogoro kila siku.

Kwa mujibu wa Mgedzi, treni moja ya abiria inaweza kufanya safari zaidi ya 3 au 4 kwa siku kati ya Dar es Salaam na Morogoro, na hivyo kwa siku kunaweza kuwa na safari kati ya tisa hadi 12, lakini idadi ya safari inaweza kuongezeka kulingana na mahitaji.

“Unapoanza na kitu kipya, una hatua ya mwanzo ya kuvutia wateja na ili wateja waweze kuvutika unahitaji kutoa huduma ya uhakika, usafiri wa kasi na pasipo kupoteza muda kwa kusimama simama njiani, mambo hayo yatavutia tu wateja,” anaeleza Mgedzi.

Uhai wa reli Kuhusu uhai wa reli ya kisasa inayojengwa Tanzania, Mgedzi anasema madaraja ya reli yana uwezo wa kudumu kwa miaka 100, wakati reli yenyewe ambacho ni chuma kinachokanyagwa na kusuguliwa na tairi la chuma la treni, lina uwezo wa kudumu kwa miaka 40 kabla ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Kwa msingi huo, ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea nchi ni moja ya matunda ya uongozi siasa safi na uongozi bora unaozingatia maendeleo ya watu unaosimamiwa na Rais John magufuli, tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015 baada ya uchaguzi.

KATI ya nchi zinazokuja kwa kasi katika kuboresha sekta ya ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi