loader
Picha

TFF yamuita Manji

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kama wanachama wa Klabu ya Yanga wanamtambua Yusuf Manji kuwa bado ni Mwenyekiti wao, wamhimize ajitokeze kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa kalenda iliyotangazwa na kamati hiyo mwanzoni mwa wiki hii, fomu za kuwania nafasi mbalimbali ndani ya Yanga zinaanza kutolewa leo na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Januari 13, mwakani. Kauli ya kamati hiyo inakuja siku moja baada ya baadhi ya viongozi wa matawi ya Yanga kudai bado wanamtambua Manji kama Mwenyekiti wao na kugoma uchaguzi wao kusimamiwa na TFF.

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) iliiagiza TFF kusimamia uchaguzi huo, kwa vile Yanga haina kamati yake ya uchaguzi. Uamuzi huo wa BMT umekuja baada ya kufanya mazungumzo mara kadhaa na viongozi wa Yanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Malangwe Mchungahela alisema hawana tatizo nani klabu hiyo inamtaka isipokuwa wanachohitaji ni nafasi zilizo wazi zijazwe kwa kufuata utaratibu uliowekwa.

“Kama wanamtaka Manji sawa, wamwambie aje achukue fomu, au kama wanataka wamchukulie, lakini uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa, hatuangalii nani alizungumza, ni matawi mangapi yalikutana au ni baadhi tu,” alisema.

Manji anayeng’ang’aniwa na wanayanga hao, alijiuzulu zaidi ya mwaka mmoja uliopita kutokana na mambo yake binafsi na nafasi hiyo ya mwenyekiti iko wazi. Hata hivyo, licha ya mwenyekiti huyo kuwahi kuonekana uwanjani katika moja ya mechi zao, hakuwahi kujitokeza hadharani kutangaza nia ya kurudi tena isipokuwa wanachama hao wamekuwa wakijipa imani kuwa anarudi.

Nafasi nyingine zilizo wazi ni makamu mwenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Clement Sanga na wajumbe wanne wote walijiuzulu kwa nyakati tofauti. Suala la uchaguzi limepokelewa kwa hisia tofauti na wanachama wa klabu hiyo wengine wakiunga mkono ufanyike na baadhi wakileta vikwazo na kuleta sababu kuwa hawataki uwepo.

Mmoja wa wadau muhimu wa klabu hiyo ambaye ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema wanachotakiwa kufanya Yanga waisaidie klabu badala ya kuirudisha nyuma.

Alisema yeye kama mmoja ya wanachama na shabiki anasikitika kuona baadhi ya watu wanapinga suala la uchaguzi huku wakijua wazi kuna matatizo mengi na yanahitaji kupata viongozi kupitia uchaguzi mkuu.

TIMU nne zinazopeperusha bendera ya nchi kimataifa kwenye Ligi ya ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi