loader
Picha

Jamii ishiriki kupunguza vifo kwa wajawazito

JUZI Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ikiwa na lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga nchini.

Kwa sasa vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000 ambapo kupitia kampeni hiyo, lengo ni kufikia vifo 292 ifikapo mwaka 2020. Ni vema sasa jamii kuwa makini ili mama mjamzito asaidiwe na jamii nzima inayomzunguka.

Naamini kampeni hii, itahamasisha viongozi wa serikali, wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujuma kuchangia katika juhudi za taifa za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Ikumbukwe kuwa kila mjamzito, matarajio ni kupata mtoto, hivyo jamii kupitia kampeni hii, imsaidie aweze kutimiza malengo yake. Matarajio hayo ndiyo yanayosababisha kuwepo kwa kampeni hiyo, ili kwamba kila mwanamke anapokuwa mjamzito kuweza kufikia safari yake ya kujifungua akiwa salama yeye na mtoto, jambo linaloongeza furaha na faraja kwa familia, na jamii nzima kwa ujumla.

Zimekuwepo jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali kuhakikisha vifo hivyo vitokanavyo na uzazi vinapungua kabisa nchini, hatua ambayo haijafikiwa licha ya kuwepo kwa jitihada kadha wa kadha katika kuboresha eneo hilo.

Aidha, inawezekana wapo wanawake pindi wanapokuwa wajawazito hawahudhurii kliniki kwa wakati, huku watalaamu wakihimiza kundi hilo kutambua kuwa chini ya wiki 12 za mwanzo wakati wa ujauzito ni muhimu kuhudhuria ili kuanza mapema kumjenga mtoto. Vilevile wapo wanawake wengine hujiona kama wamekuwa wazoefu katika suala zima la uzazi, huku wakilinganisha dalili za ujauzito walizoona wakati huu na uliopita, bila kutambua kuwa mwili una mabadiliko mengi, hivyo wajitahidi kuepuka tabia hizo ili kutokwamisha jitihada za utekelezwaji wa kampeni hiyo.

Kwa upande mwingine, wapo wanawake wanaotumia mitandao ya kijamii, kwa kutoa shida wanazokabiliana nazo kuhusu ujauzito walio nao, kabla ya kufikia hatua ya kuwaona wataalamu wa afya, ambapo hujikuta wakipokea ushauri ambao kwa wakati mwingine unaweza kuwa ndio chanzo cha kuwachelewesha kufika katika vituo vya afya ili kupata huduma.

Kwa mantiki hiyo, niwahimize wanawake kutokuwa chanzo cha kukwamishwa kwa kampeni hiyo kufikia malengo yake kwa sababu mbalimbali na badala yake washiriki kuwa waelimishaji kwa wengine ili vifo hivyo viweze kupungua. Aidha wanaume nao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha pindi wake zao wanapokuwa wajawazito, wanahudhuria kliniki kwa wakati. Ikumbukwe kuwa kampeni hiyo, inahamasisha kila mmoja kuongeza juhudi na mafunzo ili kuhakikisha tatizo hilo linapunguzwa nchini na kwa wakuu wa mikoa waliosaini mikataba ya uwajibikaji yenye kuwafuatilia wajawazito kusimama kidete kuhakikisha kila anayehusika anawajibika ipasavyo.

Aidha, kwa kufanya hivyo pia itasaidia kupatikana kwa takwimu sahihi kutoka katika vituo vya afya. Kutokana na suala hilo, hima kwa wanawake wajawazito kuwahi mapema katika huduma za afya, pindi wafikiapo hatua za mwisho, ili kwamba itokeapo viashiria vyenye dalili za hatari kuweza kubainika mapema na kupatiwa huduma kwa wakati. Vilevile kwa kampenio hiyo, iweze kubainisha upungufu uliopo katika huduma za afya, hususani zinazoweza kusababisha kuendelea kutokea kwa vifo hivyo vya vitokanavyo na uzazi na kwa watoto wachanga, ili kwamba hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi