loader
Picha

Serikali ilivyojizatiti katika sekta ya elimu

DIRA ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inaelekeza kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inalo jukumu la kufanikisha dira hii kwa kubuni na kutunga sera mbalimbali za kusimamia elimu, mafunzo ya ufundi, sayansi, teknolojia, ubunifu, huduma za maktaba na utafiti.

Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu katika ngazi zote inatolewa katika ubora unaokusudiwa. Katika miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwenye sekta ya elimu. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anaeleza kuwa wameendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Inatoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo, ofisi za walimu, uzio wa shule, visima, maktaba na maabara kwa shule zenye mahitaji makubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine chakavu katika shule hizo. Waziri Ndalichako anasema kufikia Julai mwaka huu kumekuwa na awamu sita za ujenzi zilizofanyika katika ujenzi wa miundombinu kupitia mradi wa ‘lipa kulingana na matokeo’ kwa shule 551 zikiwamo za msingi 311 na sekondari 240 zimejengwa.

Anasema miundombinu iliyojengwa ni vyumba vya madarasa 1,937, matundu ya vyoo 4,417, mabweni 333, nyumba za walimu 27, mabwalo 14, majengo ya utawala 22, maabara manne na maktaba tisa kwa gharama ya Sh milioni 84.7. Anasema shule mpya 12 zimejengwa kwa Sh bilioni sita. Kati ya shule hizo, 10 ni za sekondari za Grand, Kumbukumbu ya Sokoine, Joyce Ndalichako, Rwanzoli, Busokelo, Mpepo, Erikiponi, Hondomairo, Bumbuta, Mwakakati na shule za msingi za Luguruni na Majimatitu B. Miundombinu iliyoboreshwa kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania ni pamoja na mabweni 31 katika shule 21 kati yake 20 za sekondari na moja ya msingi kwa gharama ya Sh bilioni 3.6.

Pia wamejenga mabwalo sita katika shule za sekondari tano na moja ya msingi kwa Sh milioni 900, matundu 1,272 ya vyoo kwa shule 53 kwa Sh bilioni 2.7, nyumba za walimu 160 katika shule za sekondari 85 kwa Sh bilioni 11.5 pamoja. Serikali imewajengea wanafunzi wenye mahitaji maalumu; hususani vyoo, madarasa na mabweni kwa shule 17 kwa Sh bilioni 2.3.

Kuhusu vifaa vya kujifunzia na kufundishia, Waziri Ndalichako ameainisha mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni ununuzi na usambazaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Anataja vifaa hivyo ni mashine na karatasi za maandishi ya nukta nundu na shime sikio. Aidha, wizara kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania imenunua vifaa vya kufundishia na kujifunzia na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule za msingi na sekondari. Shule za msingi zitakazonufaika ni Kigongo (Misugwi), Mugeza (Bukoba), Sima A (Bariadi), Ikungi (Mundindi), Nansio (Ukerewe), Patrick Winter (Babati DC). Sekondari ni Rugambwa (Bukoba), Jangwani (Dar es Salaam), Azania ( Dar es Salaam) na Balagdalalu (Hanang), Malangali (Iringa), Tanga Ufundi, Bwiru wavulana (Mwanza), Songea wavulana na Ilboru (Arusha).

Serikali imesambaza nakala 10,000 za vitabu vya aina tano vya maandishi ya nukta nundu vya kusoma, kuandika, kuhesabu, michezo na sanaa, afya na mazingira vya darasa la pili kwa kuzingatia mtaala wa 2015 katika shule za msingi 63 zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Waziri Ndalichako anasema katika kuhakikisha watoto wanaojiunga na elimu ya msingi wanamudu vema stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu,wameandaa mitaala na vitabu vya kiada vya elimu ya awali kutoka shule zote nchini.

Walitoa mafunzo katika vituo 18 na yalihusisha mwalimu mmoja kutoka kila shule na baada ya mafunzo kupatiwa zana hizo, mafunzo hayo yalifanyika Januari na Februari mwaka jana. Wizara imesambaza vitabu vya kiada na ziada kwa ajili ya elimu ya awali na elimu ya msingi. Kuhusu usambazaji wa vifaa vya maabara, Ndalichako anasema wizara imesambaza vifaa vya maabara vya masomo ya sayansi vyenye thamani ya Sh bilioni 16.9 kwa shule za sekondari 1,696.

Kwa upande wa mafunzo ya walimu kwa mtaala ulioboreshwa, waziri anasema mwaka 2015 hadi Juni 2018, wizara imetoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali 16,075, darasa la kwanza hadi la pili walimu 17,719; darasa la tatu hadi la nne walimu 31,966; walimu wa Memkwa 937 na walimu elimu maalumu 2,102 . Wizara imegharimia ukaguzi kwa shule za msingi 1,786 kuhakikisha kuwa ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa kutumia mbinu mpya unafanyika. Katika kuimarisha ubora wa elimu nchini, wizara imenunua pikipiki 2,894 na kuzisambaza katika halmashauri 156 kuwezesha maofisa elimu kata kufanya ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara shuleni.

Pia imenunua na kusambaza magari 45 katika ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule Wilaya kuwezesha ukaguzi wa mara kwa mara wa shule za msingi na sekondari. Kuhusu uimarishaji wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi serikali kwa kushirikiana na serikali ya Canada imeanzisha programu ya ngazi ya stashahada katika masuala ya mafuta na gesi katika Chuo cha Ufundi Arusha na katika mwaka wa masomo 2017/2018, walidahiliwa wanafunzi 25 kati yao wanne ni wanawake na 2018/2019 watadahiliwa wanafunzi 25.

Katika kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo wa Ufundi Arusha, serikali imenunua vifaa, mitambo na mashine za kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia zenye thamani ya takribani Sh bilioni 14 . Aidha, serikali imenunua na kusambaza vifaa vya kisasa vya kufundishia na vinginevyo kwa ajili ya Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro kuwezesha utoaji wa mafunzo kwa walimu wa Ufundi Stadi watakaopata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya umeme viwandani.

FEBRUARI 27 kila mwaka ni siku kubwa kwa watu wa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi