loader
Picha

Majaliwa: Tutaendelea kuongeza uwiano wa jinsia hadi 50 kwa 50

SERIKALI imesema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa inaongeza uwiano wa jinsia baina ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uamuzi ili kufi kia 50 kwa 50.

Ili kufikia hilo, imetaja mikakati iliyoanza kuchukuliwa ili kuzijengea uwezo jinsia zote, ikiwemo ya kufuta kodi za pedi za kike ili kuwezesha watoto wa kike kupata elimu bila kuathiriwa na siku za hedhi.

Mikakati mingine ni kujenga zahanati ili kupunguza vifo vya wanawake na watoto wakati wa kujifungua, kuimarisha elimu ya sekondari ili kupanua wigo wa elimu, na kuanzishwa kwa kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kumpa muda zaidi wa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Mikakati hiyo iliainishwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua Mkakati na Mpango Kazi wa Kujumuisha Masuala ya Jinsia Ndani ya Bunge, wenye lengo la kuhimiza uwiano wa jinsia wakati wa uendeshaji wa shughuli za mhimili huo.

Mbali ya kusifu Bunge kwa hatua mbalimbali za utekelezaji wa uwiano wa kijinsia, alisema serikali pia imekuwa inachukua hatua mbalimbali kufikia azma hiyo kupitia Sera ya Jinsia ya mwaka 2000 na itifaki mbalimbali za kimataifa.

“Bado haitoshi, ni lazima jitihada zaidi zifanywe ili uwiano huu wa kijinsia uweze kufikia 50 kwa 50,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa. Alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali ni kuondoa kodi kwenye taulo za kike, yanayoagizwa kutoka nje ili kushusha bei ya taulo hizo na kuwafanya watoto wengi wa kike kuyanunua na kuyatumia wakiwa shuleni wakati wa hedhi bila kuhofia kudhalilika.

Alisema baada ya hatua hiyo ya serikali, imebainika kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa kike wanaohudhuria masomo wakati wote kutokana na kumudu gharama za kununua taulo hizo na kuzitumia wakati wa hedhi wakiwa masomoni.

Hata hivyo, alionya kuwepo kwa wafanyabiashara ambao bado wanauza taulo hizo kwa bei ya juu licha ya serikali kufuta kodi. Alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni za biashara.

Alisema pia serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya sekondari ili kuwafanya watoto wengi, kunufaika na elimu hiyo huku ikiongeza madarasa na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Alisema hadi sasa takwimu zinaonesha kuwa katika elimu ya juu uwiano wa kijinsia ni kati ya asilimia 30 kwa wasichana na asilimia 70 kwa wavulana, kwenye ajira ni asilimia 37 kwa wanawake na asilimia 63 kwa wanaume na kwenye uongozi ni asilimia 15 ya wanawake na asilimia 85 kwa wanaume.

“Nichukue nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kufikia asilimia 40 kwa wanawake na asilimia 60 kwa wanaume, lakini ni matakwa yangu kuona uwiano unaongezeka na kufikia asilimia 50 kwa 50,” alisema.

Awali, Naibu Spika wa Bunge, ambaye ni pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mpango huo, Dk Tulia Ackson alisema mpango huo utaongeza ushiriki sawa wa wanawake na wanaume ndani ya Bunge na katika utekelezaji wa kazi zake zote.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godfrey Mulisa alisema Tanzania ni moja ya nchi, ambazo zimepiga hatua kubwa katika kuhamasisha uwiano wa kijinsi katika uendeshaji wa vyombo mbalimbali vya uamuzi.

TIMU nne zinazopeperusha bendera ya nchi kimataifa kwenye Ligi ya ...

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi