loader
Picha

Mahakama Yaagiza Mbowe, matiko wakamatwe

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imeamuru Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo ili waeleze ni kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kushindwa kufika mahakamani.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alisema Novemba Mosi mwaka huu, mdhamini wa Mbowe aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo amesafiri nje ya nchi kwenda Afrika Kusini akiwa mahututi.

Hakimu Mashauri alisema mdhamini huyo, alidai asingeweza kuwasiliana na mshitakiwa huyo, hivyo mahakama ilimuamini na kumtaka alete nyaraka za uthibitisho kabla ya kusomwa kwa maelezo ya awali. Alisema jana mdhamini huyo aliiambia mahakama kuwa Mbowe yupo nchini Dubai, akiendelea na matibabu.

“Dubai na Afrika Kusini ni nchi moja? Unataka kuichezea mahakama? Hii inaonekana kwamba mdhamini sio mwaminifu,” alisema Hakimu Mashauri. Mdhamini huyo, Grayson Selestine alidai katika shauri lililopita hakueleza mshitakiwa yupo wapi, lakini alipozungumza naye juzi alimwambia kuwa yupo Dubai kwa ajili ya matibabu; na kwamba vielelezo vitawasilishwa atakaporudi kwa sababu hivi sasa walimkatalia kuchukua vithibitisho.

Kwa upande wa Matiko, Hakimu Mkuu Mkazi Mashauri alisema kuwa kielelezo kilichotolewa na mdhamini wake kuonesha kuwa Katibu wa Bunge amemruhusu kwenda Burundi, sio nyaraka watakayoweza kuitumia.

Alisema Bunge na Mahakama ni mihimili miwili tofauti na kwamba hata kama mshitakiwa ni mbunge, anapokuja mahakamani anakuwa mshitakiwa kama walivyo wengine. “Mshitakiwa haruhusiwi kusafiri bila kuwa na ruhusa ya mahakama na bila kuripoti Polisi, hivyo ameruka dhamana ambayo ni haki yake,” alieleza.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashitaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuomba mahakama itoe hati ya kuwakamata washitakiwa na kuwaleta mahakamani ili waeleze kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kushindwa kufika mahakamani. Alidai vielelezo vilivyotolewa, havina mashiko na mahakama iliagiza mdhamini wa kwanza alete vithibitisho vya matibabu.

Katika hatua nyingine, Wakili wa pili anayemtetea Mchungaji Peter Msigwa, Jamhuri Johnson katika kesi hiyo ya uchochezi, alijitoa kuendelea kumwakilisha mshitakiwa kwa kile alichoeleza kuwa haelewi mwenendo wa kesi hiyo.

Tukio hilo lilitokea baada ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali, na mahakama hiyo ilikubaliana na hoja ya Wakili Johnson kwamba kabla ya kusomwa kwa maelezo ya awali, alimuelekeza mwenendo mzima wa kesi hiyo na alikubaliana.

Aidha, washitakiwa saba waliofika mahakamani hapo jana, waligoma kujibu mashitaka na hoja za awali katika mashitaka yanayowakabili, wakitaka kuwa na uwakilishi wa mawakili wao ndipo wajibu.

Washitakiwa waliokataa kujibu hoja za awali ni Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Matiko na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu. Washitakiwa hao wanawakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambaye hakuwepo mahakamani kwa sababu anaumwa, huku Msigwa pekee ndiye alikana mashitaka dhidi yake.

Hata hivyo, washitakiwa hao walikuwa wakibishana na hakimu kuhusu uelewa wa maelezo waliyosomewa, wakidai hawajasikia na hawaelewi kinachoendelea mahakamani, huku mara kadhaa wakionywa kuhusu kuheshimu mahakama hiyo kwa kutoleta dharau kutokana na vitendo vyao vya kucheka na kuongea mahakama ikiendelea.

Awali, Wakili Nchimbi alidai kuwa Kifungu cha 226 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai namba 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kinatoa maelekezo kwa mahakama kuendelea na usikilizwaji wa maelezo ya awali hata kama mshitakiwa asipokuwepo mahakamani.

Pia alidai Kifungu cha 192 (1) na (2) kinaelekeza kuwa washitakiwa wenyewe, ndio wanatakiwa kujibu hoja za awali kwa sababu hakuna mikanganyiko kisheria na kwamba imeelekeza maelezo yasomwe katika lugha inayoeleweka.

“Washitakiwa hawahitaji kupata maelekezo kutoka kwa mawakili kwa sababu anachotakiwa kufanya ni kujibu kweli au sio kweli hivyo tunaomba kuendelea kwani hakutakuwa na tatizo juu ya haki za mshitakiwa kuhusu hoja za awali,” alidai Nchimbi.

Wakili Johnson alidai kwa kuwa washitakiwa wawili hawapo, wanaomba usikilizwaji wa hoja za awali usiruhusiwe hadi washitakiwa wawepo. Kwa upande wake, Wakili John Mallya akiwa kwa niaba ya Wakili Kibatala, alidai wadhamini wameshatoa maelezo yao ni wapi washitakiwa walipo na washitakiwa wengine hawana mawakili.

Alisema kwamba yeye amepewa mikoba na Kibatala ya kumwakilisha kuelezea kutokuwepo kwake; na sio usikilizaji wa kesi. Mallya alidai kuendelea kusikiliza hoja za awali, bila kuwa na wawakilishi ni kuwakosesha haki yao ya kikatiba, hivyo aliomba maombi hayo kuletwa wakati Kibatala akiwepo.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi