loader
Picha

Waliotumikishwa ukahaba Thailand waeleza masaibu yao

MABINTI wawili kati ya wanane waliorubuniwa kwenda kufanya kazi nje ya nchi na hatimaye kujikuta wakiangukia kwenye biashara ya ukahaba, wamerejea nchini na kueleza masaibu yaliyowakuta.

Mabinti hao ambao hawakutaja majina yao, waliwasili jana kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) saa 7 mchana wakitokea nchini Thailand, walikokuwa wakitumikishwa ukahaba.

Mmoja wa mabinti hao mwenye umri wa miaka 24, aliliambia gazeti hili kiwanjani hapo kuwa walikuwa wakifanya biashara hiyo ya ukahaba mjini Bangkok kwa mwaka mmoja, kabla ya kutoroka na kurejeshwa Tanzania.

Kwa mujibu wa binti huyo, Watanzania waliowafanyia mpango wa kwenda nchini Thailand, waliwarubuni kwa kudai kuwa waliwatafutia kazi za saluni na kuuza maduka makubwa (supermarket).

“Mimi niliambiwa kuwa naenda kufanya kazi ya kuuza ‘supermarket’ na mwenzangu hapa aliambiwa kuwa anaenda kufanya kazi ya saluni, lakini tulipofika huko tulinyang’anywa pasipoti zetu na kuambiwa lazima tuwalipe gharama walizotumia kutusafirisha mpaka huko,” alieleza binti huyo ambaye ni mwenyeji wa Kahama mkoani Shinyanga.

Mabinti hao ambao walikuwa hawajuani na kila mmoja alipelekwa nchini humo kwa wakati wake mwaka jana, walifahamiana wakati wakifanyiwa mpango wa kurejeshwa nchini. Walisema walilazimishwa kufanya ukahaba ili walipe dola za Marekani 5,000 (takriban Sh milioni 11.4) kila mmoja, ambazo ni gharama zilizotumika kuwasafirishia na kuwahudumia kwenda nchini Thailand.

“Tulikuwa tunalazimishwa kutoka kwenda kufanya ukahaba mjini kila siku usiku, na tulikuwa tukilipwa na wateja wetu kati ya dola 50 hadi 200 ambazo tulizipeleka kulipa deni, haya ndio yalikuwa maisha yetu ya kila siku hadi tulipofanikiwa kutoroka,” alieleza binti mwingine mwenye umri wa miaka 23 ambaye anatoka jijini Dar es Salaam.

Binti huyo alirudi akiwa na mtoto wa kiume mwenye umri unaokadiriwa kuwa wa mwaka mmoja, ambaye alimpata huko huko katika shughuli zake za ukahaba. Baada ya kuwatoroka watu waliokuwa wakiwashikilia na kuwafanyisha ukahaba, mabinti hao walisema walisaidiwa na Wazungu waliowafanyia mpango wa kurejea Tanzania.

Mmoja kati yao alifanikiwa kurudishiwa pasipoti yake, lakini mwingine pasipoti yake iliharibiwa, hivyo alisafiri kwa kibali maalumu hadi Tanzania. Walisema walipowasili JNIA, hawakupata usumbufu wowote kwa kuwa walipokewa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).

Kutokana na kadhia waliyokumbana nayo Thailand, walitoa mwito kwa serikali kuyafuatilia mashirika yanayojinadi kuwatafutia kazi mabinti wa Kitanzania nje ya nchi, kwa kuwa ni mashirika hatari kwa mustakabali wa mabinti nchini.

Aidha, waliwataka mabinti wenzao wa Kitanzania, wasitamani kwenda nchi za nje kwa ahadi ya kutafutiwa kazi, bali wawe waangalifu na watu watakaotaka kuwarubuni kwa kisingizio cha kutafutiwa kazi nje ya nchi.

Walisema binti mwenzao mmoja ambaye ni Mtanzania bado amekwama huko. Gazeti hili jana liliripoti kuwa wanawake wanane wa Kitanzania na wengine 16 kutoka nchi zingine, wameokolewa kufanya biashara ya ukahaba, baada ya kudanganywa kwamba wanapelekwa nje ya nchi kupatiwa kazi nzuri.

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais (Menejimenti ya Utumishi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi