loader
Picha

Serikali yazungumza na wanunuzi korosho

SERIKALI imeanza mazungumzo na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka nje, kwa lengo la kuhakikisha kwa muda mfupi zao hilo linanunuliwa. Aidha, imetoa vibali vya kuuza mahindi nje ya nchi na mataifa ya nje kuja kununua zao hilo, huku ikichukua tahadhari ya kutokosekana kwa chakula nchini.

Hayo yameelezwa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Alisema serikali inafanya mazungumzo na mataifa makubwa moja kwa moja na kuwa tayari kuna wanunuzi wakubwa waliopatikana, ambao wameonesha nia ya kununua korosho.

“Leo hii (jana) baada ya kipindi cha maswali, tutakuwa na kikao na baadhi ya wanunuzi na waziri ili kujua ni kiasi gani cha korosho kitanunuliwa,” alisema Waziri Mkuu. Alisema serikali iliweka utaratibu wa kununua korosho kwa njia ya minada ili kuleta ushindani wa bei, jambo ambalo limesaidia korosho kuuzwa kwa bei ya juu ndani ya miaka minne iliyopita.

“Lakini mwaka huu kumekuwa na dosari hasa baada ya minada kutokuwa mizuri kutokana na soko la dunia kuwa na bei ya chini, lakini kwa ushauri wa wataalamu wetu walisema bei ya chini inunuliwe kuwa shilingi 3,000 na ndio maana Rais (John Magufuli) alitoa bei elekezi ambayo wadau waliikubali.

“Siwezi kujibu ni tani ngapi, kuna minada imefanyika na mingine inaendelea ingawa viwango ambavyo vinawekwa na wanunuzi ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya kosorosho iliyopo kwenye maghala,” alieleza.

Majaliwa alitoa rai kwa wananchi na wabunge wanaotoka maeneo ambako korosho inalimwa kuwa wavumilivu, kwa sababu korosho inatafutiwa masoko na serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linanunuliwa, kama ambavyo imefanya kwenye zao la kahawa na tumbaku ambako kulikuwa na kusuasua.

“Nawaomba wakulima wa zao hilo kuwa watulivu kwani serikali inaendelea kutafuta soko la zao hilo kama ilivyo kwenye zao la kahawa na mazao mengine. “Niwahakikishie katika kipindi kifupi kijacho kama tulivyotatua changamoto za zao la kahawa na tumbaku pia kwenye korosho tutafanya vivyo hivyo.

Mheshimiwa mbunge na wabunge wote mliopo hapa najua mnajukwaa la kuwasiliana na wakulima muendele kuwatuliza,” alisema Waziri Mkuu. Aliongeza: “Tunashukuru kuwa angalau wametulia (wakulima) na sisi serikali tunaendesha taratibu zetu kwa haraka ili kuhakikisha zao hili tulitoa kwa haraka sana.”

Alikuwa akijibu maswali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF) aliyetaka kupata kauli ya serikali kuwa imetekeleza kwa kiasi gani ahadi ya kununua korosho na tani ngapi zimenunuliwa.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alimtaka Waziri Mkuu kujibu swali hilo bila kujumuisha takwimu, kwa sababu si swali la kisera. Kuhusu mahindi, Waziri Mkuu alisema serikali imetoa vibali vya wakulima kuuza mahindi nje na mataifa ya nje kununua zao hilo, kwa sharti la serikali kujua kiasi cha mahindi kinachouzwa na bei inayouzwa nje ya nchi.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Lucia Mlowo (Chadema) aliyetaka kujua tamko la serikali kuhusu kukosekana kwa soko la zao la mahindi, licha ya wakulima kulima zao hilo kwa wingi.

“Ni kweli baada ya wakulima kulima kwa wingi zao hilo kumekuwa na tatizo la soko na kuwa wizara ya kilimo ilishatoa maelekezo kwa watendaji mbalimbali kuhusiana na uuzaji wa zao hilo nje ya nchi,” alieleza.

Alisema kabla ya kuuza mahindi nje ni muhimu nchi kujua ina kiasi gani cha zao hilo na kwa bei gani ili kuhakikisha kusiwe na upungufu ndani ya nchi, baada ya kuuza zao hilo na pia kujua kiasi gani cha dola kimepatikana.

Majaliwa alisema kutokana na umakini huo ni vyema mfanyabiashara aliyepata soko la nje, kutoa taarifa kwa mkuu wa wilaya wa eneo husika ili naye awe na takwimu.

Akizungumzia kushushwa kwa bei ya pembejeo baada ya swali la nyongeza la Mlowo, aliyetaka kujua kama serikali ina mpango wa kupunguza bei ya pembejeo kwa wakulima, Majaliwa alisema serikali imekuja na utaratibu wa kununua mbolea kwa pamoja na kuisambaza kwa wakulima ili wanunue kwa bei nafuu na kwa wakati.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi