loader
Picha

Ubalozi mpya wa Israel wazaa matunda

UAMUZI wa Serikali ya Awamu ya Tano kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Israel, umeanza kuzaa matunda baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30 kutoka nchini humo kuja nchini kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.

Timu ya madaktari na wataalamu hao wakiwemo wawili kutoka Marekani na Canada, wanatoka Shirika la Save a Child’s Heart la Israel, wamekutana na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi amesema kati ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni hiyo, 10 watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 20 watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.

Profesa Janabi alibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita JKCI imetoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa 254,881 ambapo kati yake wagonjwa 799 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, 2,056 wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo na wengine wamepatiwa matibabu mengine ya moyo.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa taasisi hiyo na wataalamu kutoka nje ya nchi umesaidia kuwawezesha wataalamu wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na pia kuokoa gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi, ambazo kwa kipindi cha miaka mitatu Tanzania imetumia Sh bilioni 22 ikilinganishwa na Sh bilioni 87.8 ambazo zingetumika kutoa matibabu hayo nje ya nchi.

Kiongozi wa timu ya madaktari hao na Mkurugenzi Mtendaji wa Save a Child’s Heart, Simon Fisher na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo wa shirika hilo, Profesa Sasson Lior, wamemshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao timu hiyo inapata kutoka Serikali ya Tanzania na wameahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kuokoa maisha ya watoto.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wataalamu hao kwa kuja Tanzania kuokoa maisha ya watoto na pia amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.

Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Netanyahu na kuikabidhi kwa Balozi wa Israel nchini, Noah Gendler ambayo pamoja na kushukuru kwa msaada wa matibabu, pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.

“Israel ni marafiki zetu wa siku nyingi, tunasaidiana na kushirikiana kwa mengi, ndio maana niliona tufungue Ubalozi wetu kule Israel ili kurahisisha masuala haya muhimu ya ushirikiano na yenye manufaa kwa watu wetu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa mwito kwa Balozi Gendler na wataalamu hao kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kuja kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini na kuwahakikishia serikali itanunua dawa na vifaa hivyo, na pia watakuwa na uhakika wa soko la Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Pia aliwapongeza madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuokoa maisha ya watu na amewahakikishia serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajengea mazingira bora ya kazi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Faustine Ndugulile. Wakati huo huo, Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini, Gendler na baada ya mazungumzo hayo, Balozi Gendler amesema Israel imetoa nafasi za masomo kwa Watanzania 150 watakaogharamiwa na Serikali ya Israel kwa ajili ya kujifunza utaalamu wa kilimo cha kisasa kwa miezi 11.

Halikadhalika, Rais Magufuli amekutana na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, Profesa Roger Hartl kutoka Marekani aliyepongeza juhudi za Tanzania kuendeleza huduma za matibabu ya kibingwa na ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi yake ya Weill Cornell Medicine ya Marekani na Tanzania.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi