loader
Picha

Uyui kutangaza fursa zake za biashara

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tabora (Uyui) mkoani Tabora imejipanga kutangaza fursa zake za uwekezaji na biashara ikiwemo mahitaji mengi ya uwekezaji katika utoaji huduma kwa wananchi kupitia Jukwaa la Biashara Tabora .

Kwa sasa wilaya hiyo haina hata kituo kimoja cha mafuta, hoteli au nyumba za kulala wageni, stendi za mabasi, benki na maduka ya fedha, masoko pamoja na viwanda vidogo vidogo.

Pamoja na hayo, katika kukabiliana na tatizo la halmashauri hiyo kushika mkia katika matokeo ya mitihani ya elimu ya msingi na sekondari, imeanzisha kampeni ya kuchangia ujenzi wa mabweni 14 inayotarajia kuingiza Sh bilioni 1.5.

Akizungumza na timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Dailynews, Habarileo na Spotileo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora (Uyui), Gift Msuya, alisema jukwaa hilo la biashara ni fursa nzuri kwao itakayotumiwa na halmashauri hiyo kutangaza fursa za uchumi.

Alisema halmashauri hiyo imebarikiwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa asali inayotambulika Tanzania nzima kama asali ya kutoka Uyui. Pia ina kilimo cha tumbaku, mpunga, ufugaji lakini bado uzalishaji na ufungashaji wa bidhaa hizo hauridhishi kutokana na kutokuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika maeneo hayo.

“Kwa mfano katika uzalishaji wa asali na nta, tunazalisha asali bora lakini ufungashaji wake si wa kiwango na ndio maana hata uuzwaji wake ni wa bei ya chini. Pia tunazalisha mpunga wa kutosha katika kata zetu zote 30, kata tisa ndio wazalishaji wakubwa, lakini hakuna kiwanda cha kukoboa na kufanya branding,” alieleza.

Alisema halmashauri hiyo pia ina ng’ombe 44,190 lakini hakuna machinjio ya kisasa wala kiwanda cha ngozi jambo linalosababisha ngozi zinazopatikana zitupwe tu na au kufukiwa. “Mahitaji ya uwekezaji ni mengi.

Tunahitaji uwekezaji ujenzi wa vituo vya mabasi, hoteli, stendi za mabasi na wasafirishaji. Tuna barabara nzuri, tupo jirani na mjini Tabora lakini hatuna huduma muhimu za wananchi, tunazifuata Tabora kilometa 35 kutoka hapa,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Hadija Makuwani, alisema ina hekta 450,000 zinazofaa kwa kilimo, lakini zilizotumika ni 150,000, hivyo hekta 300,000 ziko wazi. Alisema kupitia jukwaa hilo la biashara wanatarajia watapata uwekezaji wa kutosha katika kilimo, mifugo, ujenzi wa ofisi na kumbi za mikutano na kilimo cha umwagiliaji.

Kwa sasa uwekezaji katika maeneo hayo ni mdogo. Halmashauri hiyo ni moja ya halmashauri nane za mkoa wa Tabora. Nyingine ni Sikonge, Kaliua, Nzega, Igunga, Urambo na Tabora Mjini.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Tabora

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi