loader
Uganda kuanza kutoa pasipoti kidijiti 2019

Uganda kuanza kutoa pasipoti kidijiti 2019

UGANDA itaungana na mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika utaratibu mpya uliokubaliwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo wa matumizi ya pasipoti za kisasa za kidijiti kuanzia Januari 2019.

Pasipoti hizo ambazo zitawalazimu wananchi wa Uganda kugharamia zaidi ili kuzipata, watalipa Dola za Marekani 67 sawa na shilingi za Uganda 250,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 67 ya pasipoti zinazotumika sasa hivi zinazowagharimu wananchi shilingi za Uganda 150,000. J

umuiya ya Afrika Mashariki ilipitisha utaratibu wa matumizi ya pasipoti za kisasa za kidijiti katika jitihada za kuendana na wakati kwa sababu katika mataifa yaliyoendelea utaratibu huo ndio unaotumika.Uganda itaungana na nchi za Tanzania, Burundi na Kenya katika kukamilisha zoezi hilo na kuanza kuzitumia pasipoti hizo.

Pasipoti ya kisasa ya Kenya inapatikana kwa dola za Marekani 45.5 sawa na shilingi za Kenya 4,550. Kwa upande wa Tanzania ambayo ilizindua pasipoti yake mapema mwaka huu, gharama ya kuipata pasipoti hiyo imeongezeka kutoka dola za Marekani 22 sawa na Sh 50,000 hadi dola za Marekani 65 sawa na Sh 150,000.

Nchini Burundi, pasipoti hizo za kisasa zilizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana ambapo zinapatikana kwa gharama ya dola za Marekani 134 ambazo ni sawa na faranga za Burundi 240,000. Pasipoti ya kisasa ya kidijiti ya Afrika Mashariki inatekelezwa na nchi zote za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Huo ni utekelezaji wa maelekezo ya mwaka 1997 ya Sekretarieti ya jumuiya hiyo ya kuwa na nyaraka ya kanda ya kusafiria inayoendana na iliyotangazwa na Umoja wa Afrika mwaka 2016. Sababu za pasipoti ya Uganda kuwa ghali zimetajwa kuwa ni kutokana na gharama za utengenezaji wa pasipoti hiyo kuwa juu. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Jacob Simunyu alisema gharama hizo ni za muda na zimenuia kugharamia za uzalishaji wa pasipoti hizo.

“Kama tungeamua kutumia bei ya zamani kwa kweli isingeweza kufidia gharama za utengenezaji kwa sababu ni ndogo ukilinganisha na gharama za kiwanda ambazo zipo juu,” alisema Simunyu akizungumza na wanahabari jijini Kampala.

Kwa mujibu wa waziri huyo, pasipoti hizo zinatarajia kukidhi matakwa taratibu zilizowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa (ICAO). Sheria na taratibu za ICAO ni kuwa pasipoti lazima iwe na sehemu ya kidijiti inayotunza kumbukumbu za mtumiaji. Pasipoti hizi zina sehemu inayotumia kadi ya kidijiti inayoweza kusomeka katika mashine kwa ajili ya kuzijua kumbukumbu muhimu za mtumiaji.

Serikali ya Uganda imewapa raia wake hadi Januari 2021 kama mwisho wa matumizi ya pasipoti za sasa hivi na kuanzia wakati huo zitatumika pasipoti hizi za kisasa tu, hivyo imewataka wananchi kujiandaa na mabadiliko hayo.

Msemaji wa Serikali ya Uganda, Ofwono Opondo aliwaambia wanahabari jijini Kampala kuwa tarehe ya mwisho ya Januari 2021 iliwekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano wa nchi zote wanachama.

Kenya ambayo ilianza kutumia pasipoti mpya Septemba 2017 imeweka tarehe ya mwisho ya matumizi ya pasipoti ya zamani kuwa ni Agosti 2021 wakati Tanzania iliweka mwisho wa matumizi ya pasipoti ya zamani kuwa ni Januari 2020. Taarifa kutoka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaonesha kuwa ni nchi ya Rwanda pekee ambayo haijaweka tarehe ya mwisho ya matumizi ya pasipoti za zamani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5f6366dfdd0e216a79aea03c0929bf29.png

UGANDA imekubali kuongeza maradufu idadi ya ...

foto
Mwandishi: KAMPALA, Uganda

Post your comments