loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Magufuli aeleza sababu za mabadiliko

USIMAMIZI mbovu wa sekta ya madini nchini ni moja ya sababu, zilizofamfanya Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Katika mabadiliko hayo juzi, Rais Magufuli alimteua Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini na kumuondoa aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Angella Kairuki, aliyemteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, wizara ambayo ni mpya.

Rais Magufuli alitoboa siri ya mabadiliko hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, alipowaapisha viongozi mbalimbali waliopata uteuzi hivi karibuni akiwemo Biteko, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Siri ya kumteua Biteko

Akielezea ni kwanini amemteua Biteko kuwa Waziri wa Madini, Rais Magufuli alisema ni kutokana na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumwamini Biteko kwa kumteua kuongoza Kamati ya Nishati na Madini na baadaye kumteua kuongoza Kamati ya kuchunguza wizi wa madini nchini, hivyo kumshawishi kumteua kuwa Naibu Waziri na kisha Waziri kamili wa Madini.

Alisema alikuwa akifuatilia kwa nini kila mara Spika alikuwa akimteua Biteko kwenye mambo yanayohusu madini, ndipo alibaini kuwa utendaji kazi wake katika nafasi zote alizoteuliwa kuongoza, ulikuwa mzuri na yeye akaamua kumteua.

“Mheshimiwa Spika, ulipounda kamati za Bunge ulimteua Biteko kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, ulipounda tena Kamati ya kufuatilia Madini yanavyoibwa, ulimteua tena Biteko kuwa Mwenyekiti, nami nilikuwa namfuatilia, nikaamua kumteua,” alieleza Rais Magufuli.

Alimtaka Biteko achape kazi, kwa vile hatasita kumuondoa, kwa kuwa dhana yake ya kuendelea kufanya mabadiliko kwa watendaji wake, bado iko palepale.

Alisema rasilimali zilizopo nchini ni lazima ziwanufaishe wananchi, hivyo asiporidhika na utendaji wa viongozi anaowateua, hatasita kuwaondoa.

Akerwa usimamizi wa madini

Rais Magufuli alisema pamoja na kutungwa kwa Sheria inayosimamia Sekta ya Madini, lakini cha kusikitisha ni kwamba bado kuna udhaifu mkubwa katika Wizara ya Madini, kwa kushindwa kusimamia sekta hiyo vizuri kwa manufaa ya Taifa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ripoti iliyomfikia hivi karibuni, inaonesha kuwa Tanzania si nchi inayoongoza kwa kuuza dhahabu nje ya nchi katika Afrika Mashariki, licha ya kuongoza kuwa na dhahabu nyingi katika ukanda huo.

Alisema Wizara ya Madini imeshindwa kuwasimamia wachimbaji wadogo wa madini nchini ;na ndiyo maana hajui ni wapi wachimbaji hao wanauza madini yao.

Alisema ni wajibu wa Wizara hiyo, kujua ni wapi wachimbaji wadogo wanauza madini yao, soko la dhahabu lilipo na Taifa linapaswa kunufaika vipi.

“Sheria ya madini imeweka utaratibu mzuri wa kusimamia madini ikiwemo masuala ya mikataba na namna wachimbaji wadogo wanavyoweza kushiriki kuchimba na kuuza madini.

“Lakini cha kusikitisha dhahabu haiinufaishi Tanzania licha ya Wizara kujaa watendaji wote wanaotakiwa,” alieleza Rais Magufuli.

Maagizo mapya kwa wizara, BOT

Kutokana na udhaifu huo, Rais Magufuli alimwagiza Waziri Biteko kuhakikisha anaanzisha Vituo Maalum vya Kuuzia Madini (Mineral Centres) nchini, kama Sheria ya Madini inavyotaka.

Alimtaka Biteko pia kushirikiana na Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili ianze kununua dhahabu ili kuwa na akiba ya madini hayo, kwa kuwa dhahabu ni fedha.

“Kaanze na vituo vya kuuzia madini kama kule Geita, Mwanza, Shinyanga, Mirerani na kwingineko; vituo hivi vitatusaidia kujua kiasi cha madini tunachouza kwa mwaka, lakini pia wachimbaji wadogo wataweza kuchangia mapato kwa kuuza madini yao kwenye vituo hivi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Awaunganisha Waziri Ummy, Dk Chaula kiaina

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alieleza namna alivyoamua kuwapanga katika wizara moja, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliyekuwa na mzozo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, ambaye sasa amemteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ya Afya, Dk Zainabu Chaula.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, japo viongozi hao wawili wote wanatoka Tanga, walikuwa hawaelewani na ndiyo maana akaamua kumteua Dk Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ili wakae wizara moja na Waziri Ummy, kama njia ya kuwapatanisha ili waweze kuchapa kazi kwa bidii.

Alisema katika utekelezaji wa miradi ya afya, ambapo Wizara ya Afya inashirikiana na Wizara ya Tamisemi, viongozi hao wawili wamekuwa wanatofautiana na kutumiana meseji za ugomvi, hatua iliyomfanya ampandishe Dk Chaula kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya ili wafanye kazi kwa pamoja, kama njia ya kuwapatanisha.

Uteuzi wa Dk Mpoki kuwa Balozi

Kuhusu uteuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, DK Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi, Rais Magufuli alisema ni kutokana na kiongozi huyo kusafiri nje ya nchi mara kwa mara.

Alisema baada ya kufuatilia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk John Kijazi kuhusu namna viongozi wanavyosafiri nje, alibaini Dk Mpoki kuomba vibali mara nyingi zaidi ili kusafiri nje na kuona anafaa kuendelea kuitumikia nchi akiwa huko huko nje kwa nafasi ya Balozi.

Viongozi wengine alioeleza bila kuwataja majina kuwa wanalumbana ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo na Mbunge wa Jimbo hilo, huku akisema kuwa malumbano yaliyokuwepo kati ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Mkuu wa Wilaya, yamekwisha baada ya yeye Rais kuwatumia ujumbe maalumu.

Viongozi walioapishwa Viongozi walioapishwa jana mbali ya Biteko na Dk Chaula ni Elius Mwakalinga, ambaye amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Kabla ya uteuzi huo, Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA) na anachukua nafasi ya Joseph Nyamuhanga, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Tamisemi.

Mwingine ni Dorothy Mwaluko aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uwekezaji na kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Pia Rais Magufuli alimwapisha Dk Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Afya. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Naibu Katibu Mkuu mwingine aliyeapishwa ni Dk Francis Michael, ambaye amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo, Dk Michael alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Profesa Faustin Kamuzora, aliapishwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera kuchukua nafasi ya Athumani Diwani, aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika Ndugai, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, mawaziri, naibu mawaziri na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi wa dini

SERIKALI imewataka waliohujumu mali za vyama vya ushirika kujisalimisha ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi