loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndugai amlipua Lissu, ambana Zitto

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amevunja ukimya na kujibu tuhuma za upotevu wa Sh trilioni 1.5, ambazo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) alidai kuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema hazionekani matumizi yake; na kudai kuwa mbunge huyo ni muongo.

Katika hatua nyingine, Bunge limebainisha kumlipa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) takribani Sh milioni 250 kama malipo mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu (miezi 15). Akimzungumzia Zitto bungeni jana mara baada ya kukamilika kwa kipindi cha Maswali na Majibu, Spika Ndugai alimsihi Zitto kuwa na hofu ya Mungu, kwa kuacha kusema uongo, kwa kuwa haipendezi mtu mzima kusema uongo kwa taifa na kimataifa.

Akifafanua, Ndugai alisema: “Zitto aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kwamba CAG alikuwa amefanya ukaguzi Hazina na katika ukaguzi huo aligundua wizi mkubwa, ubadhirifu wa Sh trilioni 1.5 na ametoa ripoti maalumu ya ukaguzi huo na ripoti hiyo imefika ofisi ya Spika na Spika amekalia ripoti hii. “Sasa hayo mengine nilikuwa siyajali sana, kuhusu mimi kwa mfano kutuhumiwa kwamba nimekalia ripoti hiyo na hasa kwenye Instagram ya Januari 8 mwaka huu, ningependa kusema mbele ya Bunge hili na kwa wananchi wa Tanzania kwamba ndugu yetu Zitto anapenda sana tabia za kusema uongo, na haipendezi mtu mzima kusema uongo huo, si utamaduni wetu.

“Kama hiyo barua imetoka kwa CAG imeenda kwa Spika, waheshimiwa wabunge tulikuwa tupo likizo, wewe (Zitto) unajuaje pale katikati, unafanya kazi Ofisi ya CAG au inakuwaje? Lakini niseme tu kwamba barua tajwa yeye alisema ni ya tarehe 8, mimi nimeletewa ofisi ya Dar es Salaam Januari 16, mwaka huu.”

Ndugai aliongeza: “Kwa hiyo haikuwa kweli, lakini pia baada ya kuipata tarehe 16 muda mfupi baadaye nikawa nimeipeleka kwenye Kamati ya PAC (Hesabu za Serikali) kama ilivyo ada, kwa sababu hata ninyi wenyewe ubadhirifu wa Sh trilioni hivi Spika anakaliaje?” Katika akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram Januari 8, mwaka huu, Zitto aliandika: “Prof.

Assad alifanya ukaguzi maalumu kuhusu matumizi ya Sh trilioni 1.5 zilizokuwa hazina maelezo kwenye ukaguzi wa mwaka 2016/17. Taarifa hiyo ya ukaguzi maalumu ipo mezani kwa Spika na Spika ameikalia hajaipeleka PAC ili iwasilishwe bungeni. Mvutano huu wa Spika na CAG ni ujanja tu.” Ndugai alisema kama Bunge liliweza kushughulikia ubadhirifu wa fedha Sh bilioni 300, haitawezekana kukaa kimya kwa Sh trilioni 1.5 kama zitakuwa zimetafunwa kweli. “Kama tulihangaika naye katika sakata la Sh bilioni zaidi ya 300 za Escrow, leo shilingi trilioni 1.5 Spika amekalia, sasa huku ni kupakana matope, taifa zima linamwona Spika kama ni mtu wa ajabu ajabu.”

“Na haya yanatokana na ninyi wenyewe wabunge kuipaka matope ya kila aina ofisi ya Spika. Sasa sijui kwa madhumuni gani, sijui kama ni ku-retire imprest (kutoa maelezo ya matumizi ya fedha), kwa hiyo niseme kwamba taarifa hiyo haikuwa ya kweli, ni taarifa ya uongo. Ndugai alisema suala la fedha, Sh trilioni 1.5, pia lilihojiwa na Rais John Magufuli Aprili 20, mwaka jana na CAG alikanusha fedha hizo kuliwa. “Na kama mnavyojua Aprili 20, mwaka jana, Mheshimiwa Rais alikuwa akiapisha Majaji Ikulu, Dar es Salaam na alimuuliza CAG ‘uliponisomea taarifa ile kabla sijaipeleka bungeni hukuniambia habari ya wizi wa trilioni 1.5, hizo hela zimeibiwa?’ Ninyi wote mliosikiliza CAG alijibuje pale, alisema ‘hakuna mambo kama hayo’ mbele ya Rais, Ikulu.

Ndugai aliongeza: “Na wiki iliyopita nilipeleka jambo hili kwenye Kamati ya PAC, iliulizwa pia kuna wizi wa aina hiyo, yeye mwenyewe akiwepo CAG, Naibu CAG akajibu hakuna wizi wowote wala ubadhirifu wa Sh trilioni 1.5 Ndugai alisema: “Kwa hiyo ushauri wangu kwa waheshimiwa wabunge kwa ujumla wake ni kwamba hebu tujikite katika ushindani wenye tija, si kuendesha siasa zisizokuwa na maana na kutoa taarifa zinakwenda dunia nzima kama vile kuna jambo fulani, ni jambo ambalo halina tija.

Bado ushahidi hajautosha namwekea na wakati wa kwenda Kamati ya Maadili si sasa, lakini tutafika naye tu huko siku moja.” Akifafanua zaidi, Ndugai alisema: “Leo natoa tu taarifa kwa Watanzania wajue katika hili, Zitto ni mwongo, na akitaka nimfanyie utafiti wa mengine ya uongo ambayo ameyasema yapo ya kutosha. Badilika, badilika ndugu yangu, mbona mimi sijawahi kukusingizia, hujisikii vibaya yaani kwenye moyo wako hakuna Mungu?” Lissu alipwa milioni 250/- Kwa upande wa malipo ya Lissu, Spika Ndugai alisema Mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), amelipwa Sh milioni 250 kama malipo mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu (miezi 15).

Spika Ndugai alisema kiasi hicho ni malipo mbalimbali kuanzia Septemba 7 mwaka 2017, ambapo mbunge huyo alishambuliwa hadi Desemba mwaka jana. “Jambo ambalo nataka kulisema na nilikuwa nikikataa kulisema tangu mwanzo linamhusu Tundu Lissu, kwa sasa tumeamua kwenye ofisi yetu kuanza kujibu kwa kuwa nilikuwa nikikataa sana kujibu tangu mwanzo kwa sababu tulikuwa tunaamini kuwa bado yupo kitandani na haipendezi watu wazima kubishana na mgonjwa. “Lakini sasa dalili zote zinaonesha akiongea lazima tujibu, maana kama mtu anaamua kufanya ziara duniani ina maana kuwa anaelewa anachokiongea. Mwanzo unaweza kuhisi kwamba katika kuugua kunakuwa na baadhi ya mambo ambayo yanafanywa yanakuwa yamempita.”

Akifafanua, Ndugai alisema: “ Moja ya madai yake makubwa ni kuwa Bunge hili halijawahi kumpa wala kumjali kifedha tangu apate matatizo Septemba 7, mwaka 2017, bado tunaendelea kumpa pole. “Jambo hili ameendelea kulisema sana na bado anaendelea kulisemea na tutaendelea kutoa ufafanuzi kadri siku zinavyokwenda. Ndugai alisema tangu Septemba mwaka 2017 alipopata matatizo ya kushambuliwa hadi Desemba mwaka jana, Bunge limeshampa Lissu malipo mbalimbali ya zaidi ya Sh milioni 207.8.

“ Lakini itoshe tu kusema kwa Watanzania kwamba Bunge hili kupitia ofisi yangu kutoka Septemba 7, 2017 hadi Desemba mwaka jana, bila kujumlisha za Januari, kupitia ofisi yangu tumeshamlipa Lissu malipo mbalimbali ya jumla ya Sh 208,872,000.” Ndugai aliongeza: “ Ukijumlisha na michango yenu (wabunge) kwa ajili ya matibabu ambayo tulilipa katika Hospitali ya Nairobi alikolazwa shilingi milioni 43, ukijumlisha pamoja unapata shilingi milioni 250. Unapoendelea kusema kila mahali kwamba Bunge hili halijawahi kutoa hata senti moja kwa ajili yake katika jambo hili ni jambo la uongo, uongo…uongo kabisa. Nalitupa upande wake (Lissu) ili akanushe hili nimletee mkeka.”

MGOMBEA urais  wa Zanzibar aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi