loader
Vigogo watumia mashamba kukopa trilioni 1/-

Vigogo watumia mashamba kukopa trilioni 1/-

 WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wamiliki wa mashamba makubwa wamekopa zaidi ya Sh trilioni 1 kwa kuweka rehani ya ardhi bila kuyaendeleza mashamba hayo.

Serikali imesema mashamba sita yanayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji 'Mo' yapo chini ya uangalizi na kama atashindwa kutekeleza masharti watayafuta.

Akijibu hoja zilizoibuka bungeni wakati wa kujadili Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Lukuvi alisema kama fedha hizo zilizokopwa zingetumika kuwekeza kwenye kilimo basi nchi ingepiga hatua kwenye sekta hiyo.

"Mara zote kazi tulizokabidhiwa sisi tunazifanya kwa mujibu wa ilani ya CCM, lakini pili tunatekeleza kwa maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais, Makamu na Waziri Mkuu, maagizo ya cabinet (Baraza la Mawaziri) lakini pia maelekezo ya Bunge lako tukufu.

"Niseme kwamba pamoja na kutekeleza kwa misingi niliyosema, lakini tunatekeleza kwa mujibu wa sheria. Na kwetu sisi Wizara ya Ardhi sheria kuu tunazosimamia ni mbili kwa upande wa ardhi, Sheria Namba 4 na Namba 5 za mwaka 1999. Alisema mpaka sasa wanatumia hati za kimila katika vijiji, wanakaribia milioni 1, wa mashamba wanakaribia 1,000, mashamba makubwa wako 2,000 yenye ekari zisizopungua milioni 6 zinazotumika kwa shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji na wamilikaji hao 2,000 wanazo hati hizi.

Lukuvi alisema: "Sasa jambo ambalo tumeshauriwa hapa na ambalo limezungumzwa na ndugu yangu Msigwa (Peter Mbunge wa Iringa Mjini-Chadema) , alitaka kuzungumza kwamba utekelezaji wa sheria hii una mashaka na imefika mahali mpaka amemhusisha Rais.

"Hata siku moja haijawahi kutokea Rais akaniagiza mimi nifute hati ya mtu fulani au nimpelekee hati ya mtu fulani afute, hajawahi kuniambia. Wanaoanza kupendekeza hati ifutwe ni wananchi. Alisema walipoanza awamu ya tano wizara ya ardhi iliwapelekea dodoso wabunge wakitakiwa kujaza kero na kuwa asilimia 60 ya maoni ya wabunge ilikuwa ni kero ya mashamba pori na migogoro ya ardhi.

" Kwa hiyo baada ya hapo tukatengeneza ratiba ya utekelezaji wa maelekezo yenu (wabunge) tumefuatilia, tumerudisha yale maeneo kwa maelekezo yenu na katika uhakiki wa yale mashamba 2,000 mpaka sasa ni miaka mitatu hii tumeshafuta mashamba 46 kwa mujibu wa sheria, lakini chanzo ni ninyi."

Aliongeza: "Sababu ni moja tu, katika hawa watu 2,000 tuliowapa hati wanayo mashamba makubwa, hati hizi ukipewa kuna masharti ya matumizi huku nyuma, umri wa matumizi umeandikwa kwenye hati hizi. Hati hizi hakuna umri wa matumizi lakini unatakiwa ukipata hilo shamba angalau uhangaike walao 1/8 kwa mwaka uliendeleze ili baada ya miaka nane uwe umeendeleza shamba zima. Lakini wako watu wengi sana ambao wamekopea mashamba haya, matokeo yake siku zote hizi za nyuma walikuwa wanayatumia kwa ajili ya kuweka rehani kupata mtaji wa kufanya biashara nyingine.

" Hapa mbele yangu Mheshimiwa Spika, nimekuja na daftari hili, mimi nina privilege ya kujua siri zenu ninyi wote, humu ndani kuna watu ambao wamepewa ardhi na wamechukua mkopo, hapa kuna zaidi ya Sh trilioni moja nimeshika. Kuna zaidi ya Dola 500 hapa na kuna fedha taslimu zaidi ya Sh bilioni 800 watu wamekopa kwa rehani ya ardhi.

"Ninyi wenyewe mnajua hivi kama kweli kilimo cha Tanzania kingewekezwa zaidi ya Sh trilioni moja, si nchi ingetikisika? Fedha ziko wapi, jiulize fedha ziko wapi, sasa sisi tunao ushahidi baada ya kufanya uhakiki kwamba watu walichukua hizi fedha kwa sababu usimamizi ulikuwa hafifu, wamechukua kama kinga, wamechukua benki pamoja na kuandika madhumuni ya kuendeleza yale mashamba lakini benki hazifuatilii.

"Benki zinataka tu return ya biashara zao, watu wameenda kuwekeza Dubai, wamenunua apartment, wamewekeza biashara za kulipa papo kwa papo, mashamba yamebaki mapori na hayakuendelezwa.

"Sasa hivi wabunge mkisema kuna mashamba pori huku watu wamekopa hela benki lakini watu wanapambana kulima yale mashamba halafu anatokea mtu siku moja anatishatisha miaka 10, 20 yeye anaendelea kuongeza thamani ya kampuni yake kutoka mtaji unaotokana na thamani ya ardhi. Kule kwenye shamba haendi, kwa hiyo nataka kuwahakikishia kwamba kwa maelekezo ya ilani, CCM imetuelekeza tufanye uhakiki na tuchukue haya mashamba na ndio maana tumefanya. Lukuvi alisema mpaka sasa mashamba 46 yamechukuliwa na kuonya wale wote ambao hawatayaendeleza kuwa mashamba yao yatachukuliwa kwa kufuata sheria.

" Kwa sasa tumechukua mashamba 46 na mashamba haya yameshachukuliwa katika mikoa ifuatayo, Arusha mashamba mawili, Kilimanjaro moja, Dar es Salaam mawili, Morogoro 18, Kilosa peke yake ni 12, Iringa moja, Pwani manne, Simiyu mawili, Tanga mashamba 17, Kagera moja, Mara moja na Lindi moja. Bado shamba namba 38 kule Mtama, Lindi.

" Peter hayuko hapa (Msigwa), hakuna sababu ya kuunda kamati teule, kamati teule ya kwenda kuchunguza kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais, kisheria ninyi mnaofikiria maneno haya, hangaikeni na majimbo yenu tu, kwa sababu mheshimiwa ametimiza wajibu wake kisheria.

" Wananchi wana shida na tumetekeleza, fikiria katika uhakiki wa mashamba 2,000 tumegundua 46 kumbe tungefanya nini. Mashamba haya mnaachiwa wenyewe ili muwapangie na wanaitwa wavamizi, wakati wao ndio wamiliki wa mashamba hayo. Akizungumzia mashamba ya Kampuni ya Mohamed Enterprises Lukuvi alisema:

" Mshamba yaliyotajwa ya Mohamed Enterprises Company amesema Peter, Mohamed Enterprise anamiliki mashamba makubwa 21 nchi hii. Yako Tukuyu, Rungwe, Mombo, Korogwe, Same na yote hayo, sasa asipoendeleza tunafanyaje?

" Kwanza niwaambie mashamba yaliyofutwa ni sita, lakini onyo alipata mashamba 12, baada ya kupata onyo, Ofisa Ardhi pale akawa anachezacheza, Naibu Waziri akamdhibiti, amemwondoa. Lakini baada ya hapo nilivyomwagiza Naibu Waziri tumepiga na picha na vielelezo vyote tunavyo, tukagundua ukweli, mashamba sita hana la kufanya.

" Lakini nataka nimwambie hayo sita na yenyewe tumempa angalizo, asipotekeleza hayo tuliyomwambia yako kwenye mstari mwekundu. Nataka kuwaambieni sheria itasimama na itachukua mkondo wake bila kumwonea mtu, lakini bila kumwogopa mtu. Sisi tumeelekezwa kulinda rasilimali ya taifa, kwa hiyo naomba kama wabunge tushirikiane. Haya maneno madogo madogo watu wamechukua rushwa, wamefanya nini hayana maana, tushirikiane katika kusimamia mambo haya.

Baadhi ya wabunge waliokuwa wakijibishana kuhusu suala hilo ni Mbunge wa Simanjiro Ole Millya (CCM), Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga(CCM) na Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa(CHADEMA). Wakichangia taarifa za kamati mbili za Ardhi, Malisili na Utalii na ile ya Kilimo, Mifugo na Maji, wabunge hao walikuwa wakibiashana kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya kuwanyang'anya mashamba kwa wale wote ambao wameshindwa kuyaendeleza. Akichangia, Msigwa alisema akidai hatua zilizochukuliwa hazikufuata sheria.

" Sina shida na unyang'anywaji wa mashamba kama utaratibu huo umefuata sheria, lakini kuna kitu ambacho nataka kusema wakati tupo kwenye kamati kuna taarifa ambayo ilitakiwa iingizwe lakini haikuweza kuingizwa ndani ya taarifa hii.

"Pamoja na sifa nyingi za mheshimiwa (William) Lukuvi ambazo na mimi nilisha wahi kumpa lakini suala hili la mashamba makubwa lina harufu mbaya ya rushwa na ukakasi," alisema Msigwa.

Baada ya muda mfupi, Millya aliomba kutoa taarifa ambapo alieleza kuwa yeye anatoka jimbo la Simanjiro na kwamba takribani mwezi mmoja uliopita Lukuvi alifuta mashamba zaidi ya 200 yakiwemo ya vigogo hao kutokana na kutoendelezwa.

"Mheshimiwa spika naomba nimpe taarifa mbunge anayeendelea kusema mimi natoka jimbo la Simanjiro, takribani mwezi mmoja uliopita Waziri alifuta mashamba zaidi ya mia mbili. Na nina hakika mashamba haya yote yalikuwa hayafuati utaratibu na hakuna harufu yoyote wala asipende kumchafua waziri." Baada ya Millya kueleza hayo, Msigwa aliendelea kwa kueleza:

"Mimi nadhani unaenda haraka mimi sijamchafua sasa ni wapi namchafua nimezungumza nimesema sina tatizo kabisa na mashamba makubwa kunyang'anywa kwa mujibu wa sheria na kufuata utaratibu.

"Nimetoa mfano mmoja, Sumaye alikuwa na shamba lake alilipata kihalali ameliendeleza mpaka wanachukua shamba lake alikuwa na ng'ombe 200 kwenye shamba lake alikuwa na kondoo 350, nyumba kubwa ya umwagiliaji, kisima, ghala la mazao.

"Anaambiwa hajaendeleza mimi nasema unyang'anyaji huu siyo sahihi, lakini najua kuwa rais kubadilisha hati ana mamlaka hiyo rais, mpaka sasa hivi ukiangalia hali ilivyo ukiangalia akina Mo wamenyang'anywa mashamba yao. Msigwa aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo ni lazima kamati ya uchunguzi iundwe ili kuweza kuangalia hali ya mchakato wa unyang'anywaji ulivyofanywa.

Hati hiyo, Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga aliomba kutoa taarifa na kudai kuwa aliyekuwa Mwenyekiti Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye kuwa amejiuzulu kwa kushindikizwa, kauli ambayo ilimfanya Spika wa Bunge Job Ndugai kumtaka Haonga kuthibitisha.

"Mheshimiwa Haonga thibitisha kauli yako kama Nape amejiuzulu kwa kushinikizwa na ameshinikizwa na nani?" Baada ya Spika Ndugai kuhoji, Haonga alifuta kauli akisema hana uthibitisho, amedhani kuwa inaweza kuwa ni sababu lakini kwa kuwa hawezi kuthibitisha anafuta kauli. Baada ya hapo Mlinga aliomba kutoa taarifa ambapo alisema

"Hapa linalopigiwa kelele ni suala la shamba la Mheshimiwa Sumaye ambaye taarifa zake ni hizi. Sumaye alikuwa anamiliki shamba la ekari 326, amekaa nalo miaka 15, ameendeleza ekari 6, amejenga kibanda kimoja kina watu watatu, kilikuwa na miembe mitatu, miche ya mahindi 76, mnazi mmoja, ng'ombe watatu, mbuzi 11, bata sita, na kuku tisa." Hata hivyo, Spika alisema suala la Sumaye liachwe, maana lipo mahakamani.

" Spika alisema kuwa anadhani suala la Sumaye kuhusu mashamba liko mahakamani hivyo si jambo jema kuendelea kulijadili bungeni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/44e744bc28ddd3eb76d13bfcf841f22d.JPG

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi