loader
Binti aliyeolewa ISIS kunyang'anywa uraia

Binti aliyeolewa ISIS kunyang'anywa uraia

SAKATA la binti wa Uingereza, Shamima Begum anayetaka kurejea nchini baada ya kwenda kuolewa na mpiganaji wa kundi la dola ya Kiislamu Syria (ISIS), limechukua sura mpya baada ya serikali kutangaza nia ya kumvua uraia wake.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Sajid Javid aliandikia familia ya Shamima (Shamima) barua ambayo televisheni ya ITV ilionesha; akitaka familia kumjulisha binti yao juu ya uamuzi huo na kusema anayo nafasi ya kukata rufaa.

Javid alisema uamuzi umechukuliwa ikiaminika kwamba wazazi wake wana asili ya Bangladesh hivyo anaweza kuomba uraia wa nchi hiyo.

Mwanasheria wa familia, Tasnime Akunjee, alisema wanapanga kufuata mkondo wa sheria kupinga uamuzi huo ambao umewakatisha tamaa. Pia baadhi ya ndugu wamepinga kuwa binti huyo ana asili ya Bangladesh.

Shamima ambaye aliondoka jijini London akiwa na umri wa miaka 15 akiwa ameongozana na rafiki zake wawili kabla ya kuolewa na mpiganaji wa ISIS, raia wa Uholanzi, sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi Syria akiwa na mtoto wa kiume aliyejifungua hivi karibuni.

Kabla ya kujifungua, alikaririwa akisema anataka kuondoka katika eneo hilo la vita na kurudi nyumbani Uingereza kwa ajili ya usalama wa mtoto wake atakapojifungua ikizingatiwa watoto wake wawili, walifariki dunia kwa nyakati tofauti kutokana na ukosefu wa huduma za afya.

Binti huyo alipokaririwa na vyombo vya habari akisihi raia wa Uingereza kumkubalia arudi nyumbani lakini Waziri wa Mambo ya Ndani, Javid alisisitiza kuwa angefanya kila liwezekanalo kumzuia.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, waziri amezingatia kifungu cha 40(2) cha Sheria ya Uraia wa Uingereza ya mwaka 1981 inayompa nguvu kumwondolea uraia.

Wakati sheria ikizuia waziri kusababisha mtu kukosa utaifa, inaruhusu kuondoa uraia ikionekana Shamima ametenda jambo ambalo ni kinyume na maslahi mapana ya Uingereza na ana hoja za msingi za kuamini kwamba mtu huyo anaweza akawa hivyo.

Akihojiwa na televisheni ya Sky News, Javid alisema “Mtu yeyote anayekwenda kuunga mkono ugaidi kwa namna moja au nyingine, hatuwezi kuweka rehani maisha ya maofisa wa Uingereza, wanajeshi au mtu yeyote ile kwenda kusaidia.”

Javid aliwaambia wabunge kuwa zaidi ya watu 900 waliosafiri kutoka Uingereza kwenda Syria au Iraq kuunga mkono makundi ya ugaidi, wameonesha hawapendi nchi na maadili yake. Alisema watu 100 walishanyimwa uraia kwa mazingira ya namna hiyo.

Baada ya uamuzi huo kutangazwa, msemaji wa mambo ya ndani wa chama cha Liberal Democrats, Ed Davey alikiri kwamba kujiunga katika makundi ya ugaidi ni kosa kubwa linalochochea au kuunga mkono ugaidi.

Lakini alisema Shamima anapaswa kukabiliana na mkondo wa sheria akiwa ndani ya Uingereza. Mbunge kutoka Labour, Stella Creasy, alisema angetamani kuona binti huyo akihukumiwa kwa mfumo wa ndani ya nchi badala ya kumzuia.

Baadhi ya watu walisema hatua ya kumfutia mtu uraia inastahili kuchukuliwa kwa mtu mwenye uraia wa nchi nyingine.

Shamima alipohojiwa na BBC kama ana asili ya Bangladesh alisema hana pasipoti na wala hajawahi kuishi nchini humo.

Aliyewahi kufanya mapitio ya sheria ya ugaidi, Lord Carlile alisema endapo mama yake Shamima alikuwa Mbangladeshi kama inavyoaminika, chini ya sheria ya nchi hiyo, binti huyo pia ana utaifa huo.

Hata hivyo rafiki wa familia ya binti huyo, Dal Babu alisema Shamima hajawahi kuishi Bangladesh.

Wakati huo huo, waathirika wa tukio la ugaidi la Mei 22, 2017 katika eneo la Manchester ambalo watu 23 walifariki dunia na wengine 139 kujeruhiwa, wamepinga kurejeshwa kwa Shamima.

Alex Klis ambaye wazazi wake walipoteza maisha , alisema “Abaki huko huko aliko. Sidhani kama ni mtu mzuri. Sababu kuu ya kutaka kurudi ni kwamba haiwezekani kuishi huko alipo.

Mwenyewe amekiri kwamba huko alipo alikuwa na maisha mazuri. Sasa mantiki ya kuja iko wapi kama alifurahia maisha huko aliko.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/fc359fa92d3205803b0a806132160885.jpg

RAIS Mstaafu wa Awamu ya ...

foto
Mwandishi: LONDON, Uingereza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi