loader
RC ataja fursa za uwekezaji Lindi

RC ataja fursa za uwekezaji Lindi

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, viwanda, madini, utalii, uvuvi na gesi na kutoa wito kwa wawekezaji kufika kuwekeza.

Mkoa wa Lindi upo kusini mwka Tanzania umbali wa kilomita 450 kutoka jiji la Dar es Salaam.

Zambi amebainisha hayo alipotembelea ofisi za Magazeti ya Serikali ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo zilizopo Tazara jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Jukwaa la Fursa za Biashara la mkoa huo.

TSN kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo wanaandaa jukwaa hilo litakalofanyika kuanzia Machi 25 hadi Machi 27, mwaka huu.

Kupitia jukwaa hilo, Mkoa wa Lindi utaweza kutangaza fursa zake za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ili kuwavutia wawekezaji. Akieleza kuhusu fursa hizo, RC Zambi amesema Mkoa wa Lindi una maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha mazao likiwemo la korosho, ufuta, mihogo, alizeti, mbaazi, mahindi, karanga, nazi na mengine mengi.

Alisema kuna ekari zaidi ya 300,000 ndani ya manispaa hiyo ambazo zinafaa kwa uwekezaji kikiwemo kilimo, pia ekari zaidi ya 60,000 zipo katika wilaya ya Kilwa pamoja na eneo lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 1,500 ambalo pia linafaa kwa uwekezaji na maeneo mengine mengi.

“Asilimia 80 ya wananchi wa Lindi wanajihusisha na kilimo. Mazao makuu ambayo wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza kwa kilimo mkoani Lindi ni korosho ambalo linastawi katika wilaya zote, ufuta, mihogo na alizeti; mazao mengine ambayo tunaomba wawekezaji waje kuwekeza ni mbaazi, mahindi, karanga, mpunga, choroko, mtama na nazi,” amesema Zambi.

Amesema zao kama ufuta ni la pili kulimwa kwa wingi mkoani humo lakini kitaifa ni la kwanza na kwa mwaka mkoa huo huzalisha kati ya tani 40,000 hadi 50,000 na ubora wa ufuta huo ni mzuri na hupendwa sehemu kubwa ya dunia.

Viwanda Kuhusu uwekezaji katika viwanda, Mkuu wa Mkoa huyo wa Lindi amesema mkoa wake umetenga eneo maalumu la viwanda lenye zaidi ya ekari 20,000.

Amesema licha ya mkoa huo kuzalisha korosho kwa wingi zinazofikia tani 60,000 hadi 80,000 kwa mwaka, na katika msimu ujao wanatarajia kuzalisha tani 90,000 za korosho, lakini hakuna viwanda vya uhakika vya kubangulia korosho hizo, na matokeo yake korosho hizo zililazimika kusafirishwa nje ya nchi ambako kuna viwanda.

“Natoa mwito kupitia Jukwaa hili la Fursa za Biashara, watu waje kuwekeza kwenye sekta ya viwanda mkoani Lindi; Lindi hakuna kiwanda chenye uwezo wa kubangua tani 5,000 za korosho kwa sasa, na kiwanda cha kubangua korosho cha BUCO ambacho kimeshafanyiwa majaribio, kitaanza kufanya kazi mwezi ujao,” amesema RC Zambi.

Mbali na korosho, pia aliwataka wawekezaji kwenda kuwekeza mkoani humo kwenye viwanda vya kutengeneza mafuta ya ufuta na alizeti kwa kuwa viwanda vilivyopo ni vidogo vidogo.

Madini Katika kuhakikisha Mkoa wa Lindi unanufaika na Jukwaa hilo la fursa za biashara, Mkuu wa Mkoa huyo alisema mkoa wake una kiasi kikubwa cha madini ya graphite katika wilaya za Ruangwa na Lindi Vijijini ambayo yanaweza kuchimbwa kwa miaka 40.

Madini mengine ambayo Zambi alisema wawekezaji wanaweza kwenda kuwekeza kwa uchimbaji mkoani humo ni pamoja na madini ya jasi, dhahabu, makaa ya mawe, chokaa na nickel.

Vivutio vya utalii Kwa upande wa utalii, Zambi alisema kupitia Jukwaa hilo wataweza kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyomo mkoani humo.

Alivitaja vivutio hivyo kuwa ni pamoja na eneo alikopatikana mjusi mkubwa (dinosaurs) mwenye urefu wa mita 24 na upana wa mita 12, lakini pia mabaki ya tawala za kikoloni ya Waarabu na Wajerumani.

Vivutio vingine vya utalii ambavyo vipo katika mkoa huo ni maeneo yalikoanzia vita vya Majimaji huko Kilwa Kipatimu, utalii wa bahari hususani kati ya eneo la Kitunda na Mjini ambako kuna mkondo wa bahari wa kilomita 20, fukwe zenye ubora wa kimataifa, utalii katika hifadhi ya Selous ambayo asilimia 18 ya hifadhi hiyo iko mkoani Lindi katika Wilaya ya Liwale.

Katika kuhakikisha sekta ya utalii inafanya vizuri mkoani humo, Zambi alisema miundombinu ya usafirishaji kikiwemo kiwanja cha ndege cha Lindi, kiko kwenye hatua ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wake umeshakamilika.

Gesi Kutokana na Tanzania kuwa na kiwango kikubwa cha gesi asilia kinachozidi futi za ujazo trilioni 57, RC Zambi ametoa mwito kwa wawekezaji kufika mkoani mwake ili wawekeze kwenye rasilimali hiyo kwa kuwa Lindi ni moja ya mikoa yenye gesi ya kutosha.

Almesema japokuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na makampuni matano yanayotaka kuwekeza kwenye sekta ya gesi, anatoa wito kwa makampuni mengine kufika mkoani Lindi kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi.

Amesema gesi ambayo ipo kwa sasa uwekezaji wake unafikia Dola za Marekani bilioni 30 sawa na zaidi ya Sh trilioni 60 za Tanzania.

Uvuvi Zambi amesema sekta ya uvuvi mkoani Lindi haijaendelezwa na kuwekezwa vya kutosha licha ya kuwa na eneo la kutosha la ukanda wa bahari linaolifika kilomita 300, hivyo kupitia jukwaa hilo la fursa za biashara, amewataka wawekezaji kufika mkoani humo kujionea fursa hiyo muhimu na kuitumia.

Amesema asilimia 15 ya wananchi wa Lindi wanajishughulisha na uvuvi, lakini bado mkoa huo unahitaji wawekezaji katika uvuvi wa kina kirefu cha bahari pamoja na kujenga viwanda vya kusindika samaki.

Amesema miongoni mwa samaki wanaopatikana kwa wingi mkoani humo ni pweza na kamba.

Vibali vya uwekezaji Ili kuondoa tatizo la urasimu katika upatikanaji wa vibali vya watu kuwekeza mkoani humo, RC Zambi amesema Mkoa wa Lindi utashirikiana na mamlaka zote husika ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuhakikisha watu wanaotaka kuwekeza mkoani humo, wanapata vibali hivyo kwa urahisi na kwa haraka.

Meneja Mauzo/Masoko wa TSN, Januarius Maganga, amemweleza RC Zambi kuwa Jukwaa litakalofanyika kwenye mkoa wake mwezi ujao ni Jukwaa la tisa tangu TSN ianzishe Jukwaa hilo la Fursa ya Biashara, aidha alimtembeza Mkuu huyo wa Mkoa katika vyumba vya habari vya magazeti ya Habari Leo na Daily News ambapo alipata maelezo kutoka kwa wahiriri namna utendaji kazi ulivyo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a15fa8726f6f496db05c03abee7c1303.JPG

UKOSEFU wa elimu ya biashara, uthubutu na ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi