loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera Profesa Kabudi, Uandishi wa Insha diaspora tunakuhitaji

KWA mara nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amefanya uteuzi sahihi kwa kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Anachukua nafasi ya mwanadiplomasia nguli, Dk Augustine Mahiga aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria alikokuwa Profesa Kabudi. Binafsi, nachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Profesa Kabudi tukifahamu mbali ya umahiri wake kwenye kujenga hoja kwenye majukwaa ya kimataifa, kwa diaspora, Profesa Kabudi ana uzoefu wa masuala ya diaspora.

Anazijua fursa na changamoto za diaspora kwa vile amepata kuwa diaspora nchini Ujerumani akisoma shahada ya uzamivu (PhD) ya sheria. Hivyo, Watanzania wanadiaspora tumempata Waziri ambaye tuna imani tunaweza kuzungumza naye lugha moja na alibainisha huko nyuma, huu ni wakati wa kufanya mjadala juu ya diaspora kuwa na Hadhi Maalumu.

Uteuzi wa Profesa Kabudi umekuja pia majuma kadhaa kabla ya kufanyika kwa kongamano kubwa la kidunia la Watanzania Wanadiaspora. Kama nilivyopata kuwajulisha wasomaji wa safu hii, Baraza la Diaspora la Watanzania Duniani (TDC Global) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, limeandaa kongamano la kimataifa la kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania ambalo litafanyika sambamba na uzinduzi rasmi wa TDC Global Aprili 9 hadi 11 mwaka huu, mjini Stockholm, Sweden.

Tofauti na mengine yaliyopita, kongamano hilo litafanyika ukumbi uliopo kwenye meli ya Tallink Silja AB bandari ya Vartahamnen. Kongamano hilo la kipekee linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia watakuwepo viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Viongozi Wakuu wa Baraza la Diaspora la Watanzania Duniani, viongozi wa Kamati zote za Baraza la Diaspora la Watanzania Duniani, Viongozi wa Vyama vya Diaspora wa Tanzania kote Duniani na wanadiaspora kutoka kila pande za dunia.

Kubwa litakalojadiliwa ni uwekezaji na ubunifu utakaochagiza maendeleo ya viwanda nchini. Hivyo, kongamano linafanyika wakati mwafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli imeweka msisitizo katika uchumi wa viwanda kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati kikichagizwa na maendeleo ya viwanda 2025. Kuna fursa na changamoto kufikia hatua hiyo.

Hivyo, kongamano la Sweden litakuwa ni jukwaakujadili yaliyo fursa na changamoto pia. Itakumbukwa, kwenye uwasilishaji wa bajeti ya wizara yake ya Mwaka wa Fedha 2018/2019, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Mahiga alionesha dalili za Serikali kulivalia njuga suala hili kwa vitendo kwa kutambua mchango wa diaspora kwa uchumi wa nchi akiweka hadharani kila mwaka shilingi trilioni moja zinaingizwa nchini na Wanadiaspora. Serikali ya Rais Magufuli imeonesha dhamira ya dhati ya kufungua milango ya fursa kwenye kujenga uchumi wa nchi, mathalan sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha juhudi hizi. Uchumi hauwezi kukua bila miundombinu ikiwamo mazingira rafiki ya kufanya biashara.

Serikali imeanza jitihada za kurekebisha sheria kadhaa, ikiwamo taratibu za utoaji vibali vya kuishi na vya kazi. Ilivyo sasa, mwekezaji au anayetaka kufanya kuishi na kufanya kazi Tanzania ana wizara mbili za kwenda ili maombi yake yakamilike kisheria. Anapaswa aende Uhamiaji na Idara ya Vibali vya Kazi Wizara inayohusika na masuala ya kazi. Haya na mengineyo serikali imeshaweka bayana mikakati ya kuyafanyia marekebisho. Hizi ni ishara njema na zinatoa fursa adimu kwa Watanzania wanadiaspora kushiriki kikamilifu.

Hivyo, Kongamano la Diaspora la Aprili mwaka huu, kama ilivyokuwa kwa yaliyopita, iwe ni jukwaa mujarabu la kuweka hoja mezani. Hoja na ushauri wenye kuchangia kusukuma mbele jitihada za Serikali kuinua uchumi wa nchi kwa kuwashirikisha wenye mapenzi mema na Tanzania wakiwamo Wanadiaspora. Kwa kufanya usajili kwa ajili ya Kongamano na kulipia chumba na huduma nyingine wakati wa Kongamano tembelea mtandao https://tdcglobal.org/tdclaunch- conference/ Au, piga namba +4747262181 Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu; 0754 678 252

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi