loader
Njoo Lindi tunakungoja kibiashara, kiuwekezaji

Njoo Lindi tunakungoja kibiashara, kiuwekezaji

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi inamulika na kukuletea fursa za kibiashara na uwekezaji ndani ya Mkoa wa Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, amekuwa akisema kwamba mkoa wake unaendelea na maandalizi katika kuhakikisha jukwa la fursa za biashara linaleta matumaini mapya Lindi.

JIOGRAFIA YA LINDI

Mkoa wa Lindi upo kusini mashariki mwa Tanzania na umepakana na mikoa ya Pwani, Mtwara, Ruvuma, Morogoro na Bahari ya Hindi kwa upande wa mashariki. Mkoa huu unaundwa na wilaya sita ambazo ni Liwale, Ruangwa, Nachingwea, Kilwa, Lindi Vijijini na Lindi Mjini. Mkoa huu ulianzishwa mwaka 1971 na una eneo la kilometa za mraba 67,000 ambapo zaidi ya robo ya eneo lote la mkoa ni sehemu ya Hifadhi ya Wanyama ya Selous ambayo ina ukubwa wa kilometa za mraba 18,000.

NAMNA YA KUFIKA LINDI

Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa michache hapa nchini ambao unafikika kwa njia zote ikiwemo ya barabara, maji kwa maana ya bahari na anga. Kupitia njia ya barabara unaweza kutoka mkoa wowote wa Tanzania hadi Lindi. Barabara kuu itokayo Dar es Salaam hadi Mtwara kupitia Lindi imewezesha mkoa huo kufikika kirahisi kutoka katika pande zote za nchi hii. Ni umbali wa kilomita 450 tu kufika Lindi kutoka jiji mashuhuri la Dar es Salaam na humchukua mtu anayetumia gari kati ya saa tano hadi saba.

WAKAZI

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Maendeleo ya Makazi ya Mwaka 2012, Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652 huku asilimia 90 miongoni mwao wakitegemea kilimo kuendesha maisha yao. Makabila makubwa yanayopatikana katika mkoa huu ni pamoja na Wamwera ambao hasa hupatikana katika wilaya za Nachingwea na Lindi Vijijini. Makabila mengine ni ZambiWamakonde, wanaopatikana katika wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, Wamalaba ambao wako zaidi Lindi Mjini, Wamatumbi na Wangindo ambao wanapatikana katika Wilaya ya Kilwa.

FURSA ZILIZOPO

Kilimo Kilimo ni uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wa mkoa wa Lindi kwa sababu kinachukua asilimia 80 ya shughuli za kiuchumi za wakazi wa mkoa huu. Kilimo cha korosho ndicho kinachoongoza katika mkoa huu kutokana na kulimwa katika wilaya tano kati ya sita za mkoa. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zambi, ufuta ndilo zao la pili linalolimwa kwa wingi katika mkoa wake hasa katika wilaya za Kilwa, Ruangwa na Nachingwea.

Anasema pamoja na kwamba zao hilo ni la pili katika ngazi ya mkoa lakini mkoa wa Lindi unaongoza kwa kuzalisha ufuta kwa wingi nchini. “Mkoa wa Lindi unazalisha tani 40 hadi 50 za ufuta kwa mwaka, ni ufuta unaoongoza kwa ubora na unapendwa na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya dunia,” anasema Zambi. Mbali na ufuta, zao lingine linalolimwa ndani ya mkoa wa Lindi ni muhogo ambao ndicho chakula kikuu cha wakazi wengi wa mkoa huo.

Muhogo mwingi kutoka Lindi unauzwa katika masoko ya Dar es Salaam, Mtwara na Pwani. Zao lingine linalolimwa katika mkoa wa Lindi kwa wingi ni alizeti, ambalo linalimwa hasa katika wilaya mbili za Ruangwa na Nachingwea. Wakazi wa Lindi pia wanajishughulisha na kilimo cha mbaazi ambapo Lindi ni mkoa wa pili kwa uzalishaji wa zao hilo baada ya Manyara.

Mazao mengine yanayolimwa mkoani Lindi ni pamoja na mahindi, karanga, mpunga, mtama, nazi, choroko na dengu. Zote hizo ni fursa kwa wakulima wakubwa ambao wanataka kuwekeza katika mkoa huu ambao unapata mvua za kutosha mara mbili kwa mwaka. Zambi anawakaribisha wafanyabiashara kuchangamkia mazao mengi yanayotoka katika mkoa wa Lindi pamoja na wakulima kuja kwa wingi kuwekeza katika kilimo cha mazao yoyote kama yalivyotajwa na mengine ambayo yanaendana na hali ya hewa ya mkoa huo.

Biashara na Viwanda Wakazi wengi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wa mazao ya biashara kama korosho ambazo zinapatikana kwa wingi katika wilaya za Ruangwa, Lindi Vijijini na Nachingwea na zao la ufuta katika Wilaya ya Kilwa. Pamoja na kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba na inayozalisha mazao mengi ya biashara na chakula, mkoa wa Lindi una ukosefu wa viwanda vya kutosha vya kusindika mazao.

Hili ni eneo zuri la kiuwekezaji kutokana na kuwepo kwa mazao mengi ya kutosha kuweza kulisha kiwanda kwa kipindi chote za msimu. Kiwanda cha mazao ambacho kimejengwa mpaka sasa ni kiwanda cha muhogo. Kiwanda hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa mwezi huu wa Machi.

Nishati na madini

Lindi imejaaliwa kuwa na madini mengi hasa katika Wilaya ya Ruangwa ambapo yanapatikana madini ya risasi (grafaiti). Aina nyingine ya madini yanayopatikana Lindi ni pamoja na madini ya jasi, makaa ya mawe, dhahabu, chokaa na nikeli. Mkoa wa Lindi umejaaliwa kuwa na gesi asilia katika kisiwa cha Songosongo ambayo imezoeleka kuitwa gesi ya Songosongo.

Gesi hii inazalisha umeme ambao umeingizwa katika gridi ya taifa na kuleta manufaa makubwa kwa Watanzania. Kutokana na Tanzania kuwa na kiwango kikubwa cha gesi asilia kinachozidi futi za ujazo trilioni 57, Mkuu wa Mkoa wa Lindi ametoa mwito kwa wawekezaji kufika mkoani mwake ili wawekeze kwenye rasilimali hiyo kwa kuwa Lindi ni moja ya mikoa yenye gesi ya kutosha.

Anasema japokuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na makampuni matano yanayotaka kuwekeza kwenye sekta ya gesi, anatoa mwito kwa makampuni mengine kufika mkoani Lindi kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi. Anasema gesi ambayo ipo kwa sasa uwekezaji wake unafikia Dola za Marekani bilioni 30 sawa na zaidi ya Sh trilioni 60 za Tanzania. Uvuvi Samaki ni moja ya mazao makubwa yanayokuza uchumi wa Lindi kutoka katika sekta ya uvuvi.

Kwa mujibu wa Zambi, mkoa huo una eneo kubwa kwa ajili ya shughuli za uvuvi. “Lindi ina kilomita 200 hadi 300 za bahari zinazofaa kwa shughuli za uvuvi wa samaki ambapo mpaka sasa bado hazitumiki zote kutokana na kukosa wawekezaji katika sekta ya samaki,” anaongeza Zambi. Anasema: ”Lipo eneo la kina kirefu linalohitaji wawekezaji kuweza kuvua samaki katika eneo hilo ambalo hupatikana samaki wa kila sampuli.”

Utalii

Mkoa wa Lindi umejaliwa kuwa na vivutio vingi vinavyoweza kukuza sekta ya utalii ya mkoa na taifa kwa ujumla. Mfano katika mwambao wa bahari ya Hindi mkoa huo umejaaliwa kuwa na fukwe nzuri na za kuvutia ambazo zikitengenezwa zinaweza kuwa kivutio kwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Fukwe hizi zinazidi fukwe za mataifa yaliyoendelea lakini hadi sasa hakuna chochote kilichofanyika kuzigeuza fukwe hizo kuwa fursa kwa wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Kuna mabaki ya tawala za kiarabu katika mji wa Kilwa Kivinje ambapo historia inatueleza kuwa katika eneo hilo kulikuwa na tawala ambazo zilikuwa na sarafu yake iliyokuwa ikitumika maeneo hayo tu. Kuna kumbukumbu nyingi za vita vya Majimaji kama vile makaburi ya wapiganaji wa vita hivyo.

Mbali na hayo Lindi imejaaliwa kuwa ni nyumbani kwa hifadhi kubwa kabisa Taifa ya wanyama ya Selous ambako sehemu kubwa ya hifadhi hiyo inapatikana Lindi katika wilaya ya Liwale. Lindi ina fursa ya utalii wa bahari kutokana na kuwa na ghuba maalumu iliyotengenezwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni sehemu ya bahari iliyoingia nchi kavu na kutengeneza mvuto mkubwa wa aina yake ambao unaleta hamu kwa watalii kutaka kuona. Katika Wilaya ya Nachingwea kunapatikana kambi kubwa ya wapigania Uhuru wa Msumbiji iitwayo Farm 17.

Kambi hii ilikuwa chini ya Edward Mondlane, kiongozi wa kwanza wa chama cha Frelimo mwanzoni mwa miaka ya 1960. Baada ya Mondlane kuuawa kwa bomu lililowekwa ndani ya bahasha na wakoloni wa Kireno, kambi hiyo na nyingine za Msumbiji zikawa chini ya Samora Machel. Katika kambi hiyo kuna majengo yenye ofisi ya Samora na handaki alikopita kiongozi huyo katika mbinu za kuwakwepa wakoloni na njama za kumuua.

 

Mawasiliano Tanzania Standard Newspapers Ltd, Daily News Building, Plot No. 11/4 Mandela Express Way. Po. Box 9033, Dar es Salaam. Simu: +255 286 4862; 0712 516 169; 0655 332 866. Baruapepe: info@tsn.go.tz advertising@dailynews.co.tz. Website: www.tsn.co.tz; www.dailynews.co.tz.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/75d8247a1d7ef394a26f3f231830a1f2.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi