loader
Kusajili ardhi mjini Sh 5,000/-

Kusajili ardhi mjini Sh 5,000/-

SERIKALI imezindua mpango maalumu wa kutambua na kusajili kila kipande cha ardhi mijini kwa gharama ya Sh 5,000/-, leseni ambayo inadumu kwa miaka mitano.

Utambuzi huu hautahusu watu waliojenga katika maeneo hatarishi na kwamba mfumo huo utaongeza usalama. Mpango huu unaoendeshwa kieletroniki, ni wa nchi nzima unaanza kwa Jiji la Dar es Salaam ukigharamiwa na serikali kwa ushirikiano na mamlaka za upangaji huku taarifa zake zikitumika kuandaa daftari la wamiliki wa kila mtaa na baadaye wamiliki watalipia gharama hiyo ya Sh 5,000 kuandaliwa leseni.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hiyo ni hatua ya awali ya kuwatambua wale ambao waliendeleza ardhi zao bila kupimwa kama hatua ya awali ya kupanga maeneo hayo.

“Serikali ya awamu hii imesisitiza kuwa makazi yote holela hayatabomolewa bali yaboreshwe isipokuwa yaliyojengwa katika maeneo hatarishi, kwa hiyo tumekuja na mpango huu ambao utasaidia kuwatambua watu wote ambao waliendeleza ardhi zao bila kupimwa,” amesema Lukuvi.

Amesema hiyo ni hatua ya pili kwa Dar es Salaam ambako kulikuwa na mpango wa kusajili vipande vya ardhi vilivyopangwa na kupimwa na kutoa hati ya eletroniki ulioanza katika halmashauri za Ubungo na Kinondoni.

“Vijana wameanza michoro katika wilaya ya Ilala na Kigamboni ili nao wapate hati za kielekroniki Dar es Salaam, lazima mwaka huu wote mpate,” amesema Lukuvi.

Amesema mwaka 2004 hadi 2007 wizara hiyo ilianzisha mradi wa kutambua miliki katika maeneo yaliyojengwa kiholela katika mradi ule miliki 230,000 zilitambuliwa hadi kufikia mwishoni kwa mwaka jana, jumla ya wananchi 110,000 wamepewa leseni za makazi, kati yao wananchi 4,600 wametumia ardhi yao kukopea.

“Kwa nini waliochukua ni 110,000 tu, kwa sababu gharama ya leseni hizi ambazo zilikuwa za mwaka mmoja tu ilikuwa ni kubwa, zoezi halikwenda vizuri,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema Rais John Magufuli ameagiza makazi holela yasibomolewe isipokuwa waliojenga maeneo hatarishi kama mabondeni na miinuko mikali na maeneo yaliyojengwa kwa ajili ya matumizi ya umma.

“Watu waliojenga katika maeneo hata ninayoyataja hapa hawaruhusiwi kupata hati, kupimiwa, kupelekewa miundombinu wala kupewa leseni ya makazi kwa sababu zoezi hilo tunazindua, lakini wizara haitakuja kusimamia nchi nzima kwa sababu mamlaka za upangaji ni halmashauri,” amesema.

Amesema kwa mara ya kwanza nchini kila mwenyekiti wa mtaa atakuwa na daftari ambalo litakuwa na wamiliki wa ardhi isiyoendelezwa, majengo yaliyopangwa na kupimwa na pia yaliyojengwa kiholela.

Aliwapongeza wataalamu walioandaa mfumo huo wenye manufaa makubwa kwa wananchi na pia kwa Taifa. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipongeza Wizara ya Ardhi kwa kuona umuhimu wa jambo hilo hasa ikizingatiwa migogoro ni mingi katika upande wa ardhi.

“Tumeteseka sana na migogoro ya ardhi hata nilipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kazi yangu ya kwanza ilikuwa ni kutatua migogoro ya ardhi na tuliongeza siku za kufanyia kazi migogoro hiyo hadi siku za Jumapili, tukifika katika jambo hili ni hatua kubwa sana,” amesema Makonda.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika amesema ardhi ili iwasaidie wananchi ni lazima ipimwe. Aidha, Mwanyika alisema asilimia 70 ya wakazi wa Dar es Salaam wanaishi maeneo ambayo hayajapangwa hali ambayo inayowafanya kushindwa kuendeleza.

“Utaratibu wa kupima na kurasimisha utachukua muda mrefu na ni gharama kubwa, hivyo ili kupunguza serikali imeandaa mfumo wa kielekroniki ambao utatumia siku ya mkononi kwa ajili ya kutambua na kuchukua taarifa za wananchi na kuwapatia nyaraka za awali za umiliki ambazo zinatambulika,” alisema.

Alisema mfumo huo umeandaliwa na wataalamu wa nchini ambao utawawezesha wananchi kutumia ardhi yao kama dhamana kwani zinatambulika katika katika taasisi za fedha, na itasaidia pia kuwa na kanzi data za taarifa katika maeneo yasiyopimwa.

Alitoa mwito wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi za ardhi zao.

Akielezea mpango huo, Ofisa Ardhi wa wizara hiyo, David Malisa alisema wizara iliandaa mpango huu kwani Sera ya Ardhi ya Taifa 1995 inaeleza kwamba maeneo yaliyojengwa hayatabomolewa, bali yataboreshwa.

Malisa alisema kwa kwamba Sheria ya Ardhi Namba 4 sura ya 113 inaelekeza kutambua hali ya kutoa nyaraka za awali kwa wamiliki wa ardhi kwa maeneo ambayo hayajapangwa kuwawezesha kutumia ardhi yao.

Alisema changamoto ni kwamba watu wengi wanaishi katika maeneo ambayo hayajapimwa na pia haifahamiki nani wanaishi wapi na ukubwa wa eneo.

“Ukiangalia takwimu za mwaka 2013 Arusha inaongoza kwa asilimia 80 kukaa katika maeneo ambayo hayajapangwa ikifuatiwa na Tanga 79, inafuata wilaya za Dar es Salaam Temeke 75 na Kinondoni 74,” alisema.

Alisema mfumo huo mafanikio ni kusajili vipande vya ardhi 500,000 kwa Jiji la Dar es Salaam maeneo ambayo hayajapangwa na kupimwa na kutambua wamiliki wa viwanja 300,000 vilivyopimwa, lakini hawana hati na kutoa leseni za makazi kwa wamiliki wa vipande 600,000.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/726de846e89b5d6356172ea33fe41975.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi