loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nassari- Spika nielewe, sikutoroka

ALIYEKUWA Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari ameomba Bunge limrejeshe kwenye ubunge.

Amemwomba Spika Job Ndugai aliyetengua ubunge wake wiki iliyopita kwa madai ya kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila taarifa rasmi kwa mhimili huo, amrejeshe.

Amekanusha uvumi uliosambaa kwenye mitandao na kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa ana nia ya kuihama Chadema.

Hivi karibuni Spika Ndugai aliiandikia Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kumtaarifu jimbo la Arumeru Mashariki liko wazi baada ya Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kwa masharti ya kutoulizwa maswali, Nassari alisema Spika hakumtendea haki kwa kuwa hakumpa nafasi ya kujieleza.

Alisema tofauti na inavyotakiwa, Spika alipaswa kumpa nafasi ya kumsikiliza ili aeleze sababu ya kutohudhuria mikutano hiyo ya Bunge.

Alisema si kweli kwamba hakuhudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge akidai alihudhuria Bunge la Septemba mwaka jana.

Alikiri ni kweli Bunge la Novemba mwaka jana na Januari mwaka huu hakuhudhuria lakini alimwandikia Spika barua ya udhuru wake.

“Bunge la Septemba nilihudhuria ila ni kweli Bunge la Novemba mwaka jana na Januari mwaka huu sikuhudhuria ila nilimwandikia Spika Ndugai kupitia msaidizi wake, binafsi nikimwelezea kinachonisibu hadi kushindwa kuhudhuria vikao hivyo viwili,” alisema Nassari.

Akiielezea sababu ya kutokuwapo bungeni, Nassari alisema alimpeleka mkewe hospitali nje ya nchi kutibiwa, alikuwa mjamzito na alikuwa na changamoto za kiafya ambazo zilimfanya ashindwe kumwacha peke yake.

Alisema asingeweza kumwacha mkewe katika hali ya ugonjwa na kuhudhuria vikao vya bunge kwa sababu ya kupata posho ya Sh 300,000.

“Ningekuwa mtu wa ajabu na hata jamii isingenielewa kama ningemwacha mke wangu katika hali ile ya ugonjwa na kukimbilia kuhudhuria vikao vya Bunge kupata posho ya Sh 300,000,”alisema Nassari.

“Nashukuru mke wangu amejifungua salama na tumepata mtoto wa kike aitwaye Michel na hii ni baraka hata kwa Spika kwa kuwa siku niliyokuwa naoa alikuja kule Arumeru na alipewa heshima ya ndafu akiwa kama mzazi na bosi wangu. Basi anielewe tu kama mzazi kuwa mimi mwanawe sikutoroka,” alisema Nassari.

Alidai wapo wabunge waliowahi kukumbwa na matatizo ya kifamilia na wakaiandikia ofisi ya Spika barua na hazikujibiwa, lakini waliendelea kuwasaidia wapendwa hao na hawakufukuzwa kazi na kuhoji kwa nini kwake iwe tofauti.

Alisema kufukuzwa kazi kumemtia simanzi kubwa moyoni lakini kila akimwangalia Michel anafarijika na akawataka wapigakura wake kutokata tamaa wakati akipigania haki yake.

Alisema anaamini Spika Ndugai atamrejeshea ubunge na kama itashindikana atatumia vyombo vya sheria kupigania haki yake.

Uamuzi wa kumfuta ubunge Nassari umekuja siku chache baada ya bunge kusitisha mshahara wa Mbunge wa Singida Mashariki,(Chadema) Tundu Lissu anayeendelea kutibiwa Ubelgiji, lakini amekuwa akizunguka nchi mbalimbali Ulaya na Marekani kuichafua serikali.

WATOTO 84,625 waliokuwa na utapiamlo mkali, wametibiwa kuanzia mwanzoni mwa ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi