loader
Kamati ya Bunge Utawala na Tamisemi imesema ukweli kuhusu Mkurabita

Kamati ya Bunge Utawala na Tamisemi imesema ukweli kuhusu Mkurabita

MJINI Lindi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mwanne Mchemba anasema: “Matumizi ya hati za hakimiliki za kimila zinazotolewa na Mkurabita (Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania) yatasaidia kuondoa migogoro ya ardhi baina ya wakulima ma wafugaji ambayo imewasumbia sana wanasiasa na serikali kwa jumla.

Hizi ni tiba dhidi ya migogoro hiyo.” Mchemba ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Tabora, anaongeza: “Inatia moyo kwamba wananchi wengi wametambua na wanazidi kutambua umuhimu wa hati hizi na urasimishaji ardhi unaoruhusu ubia baina ya mume na mke maana utawasaidia wanawake wasidhulumiwe ardhi na waume zao.”

Ni kwa msingi huo, anatoa mwito unaonifanya niseme kuwa, Kamati ya Bunge Utawala na Tamisemi imesema kweli kuhusu umuhimu wa Mkurabita na urasimishaji ardhi kwa Watanzania. Hii ni baada ya kunukuliwa akitoa mwito kwa wanasiasa na watendaji wengine wa serikali anasema: “Wanasiasa wenzangu tuungane ili Mkurabita tuingie nao hadi kwenye majukwaa ya kisiasa; tuufanye urasimishaji ardhi kupitia Mkurabita kuwa agenda ya kila mwanasiasa katika kila mkutano na eneo lake.”

“Hata wakuu wa idara mbalimbali; ni wakati sasa wote tuimbe wimbo wa Mkurabita ili tuchangie vema zaidi kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda maana Mkurabita ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi.)” Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary Mwanjelwa anasema urasimishaji unaofanywa na Mkurabita ni ukombozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwa hati za hakimiliki zake sasa zinakubalika katika taasisi za fedha zikiwamo benki.

Mratibu wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe anasema: “Hati hizi zinakubaliwa na benki, lakini popote duniani katika aina yoyote ya document (nyaraka) au dhamana, kinachokopa siyo ile hati kama karatasi, bali wazo na andiko la mradi linaloonesha una mradi; biashara au shamba gani na umepanga vipi kuzalisha ili urejeshe mkopo.”

Kuhusu umuhimu wa urasimishaji, Dk Mgembe anasema katika kuelekea uchumi wa kati, wananchi wataka kuwa washiriki wa maendeleo yao huku serikali pia ikitaka wananchi wakiwamo wa vijijini, waondokane na umaskini.

“Mtu anaweza kutaka kuwekeza katika kilimo cha korosho; yeye hana ardhi, ana pesa na wewe huna pesa, una ardhi mnaweza kushirikiana, lakini hawezi kufanya hivyo kama hana uhakika na umiliki wa ardhi unaomwambia. Hati ni uthibitisho halali na wa kisheria utakaomwaminisha,” anasema. Anasema hati hizo zina faida kijamii kwani zinawaunganisha wanafamilia wanaomiliki kwa pamoja kwa kuwa, hakuna anayeweza kuuza shamba bila ushiriki au ukubali wa mwenzie.

“Kama hati ni ya mke na mume mjue nayo inawaunganisha zaidi maana mkitengana mkawa sio mwili mmoja tena, shamba linakuwa kisheria siyo la yeyote kati yenu, mpaka mfuate taratibu za kubadili au kurekebisha umiliki.” “Hii inawahusu hata wananchi wengine, ukiuza sehemu ya shamba, mwende mkafanye marekebisho vinginevyo, inakuwa vighumu kufanya uhamisho wa miliki.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jasson Rweikiza, anaipongeza Mkurabita sambamba na benki mbalimbali kwa kuzungumza hadi benki kuelewa na kukubali kupokea hati za hakimiliki za kimila kama dhamana na moja ya vigezo muhimu vinavyomwezesha mwananchi kupata mkopo sambamba na taratibu nyingine. “Mkurabita wamefanya kazi kubwa na tunashukuru kwamba benki mbalimbali sasa zimeelewa na zinapokea hati hizi hata kwa ajili ajili ya mikopo…” anasema.

Rweikiza anaongeza: “Faida nyingine ya urasimishaji na mwananchi kupata hati hizi ni kwamba, mwananchi husika sasa anamiliki ardhi kisheria na inamfungulia wigo wa kukuza mtaji kibiashara na hata kupata wawekezaji au wabia, kwa kweli hizi ni utajiri mkubwa na bahati nzuri, zinatolewa kwa maandalizi yasiyo na mlolongo mrefu, urasimu wala kutumia muda na gharama kubwa.”

Anasema kujitokeza kwa wingi kwa wananchi katika Kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea ili kupokea hati zao ni ishara kuwa, wametambua umuhimu na faida ya urasimishaji na hati hizo kwani zitakiomboa kiuchumi na kijamii. Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo anasema Mkurabita ni chombo muhimu katika ukombozi wa wananchi kiuchumi na kijamii na ndiyo maana ninasema kweli urasimishaji ardhi na biashara unapaswa kuwa agenda za kisiasa.

Katika taarifa ya Mkoa kwa kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi anasema urasimishaji ardhi kupitia Mkurabita katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwe ulianza mwaka 2009. “Ulianza kwa kuijengea uwezo halmashauri kwa kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa timu ya wilaya, ngazi ya kata na ngazi ya vijiji katika vijiji vya Mbondo, Nahimba na Nakalonji.”

Zambi anasema halmashauri hiyo pia iliwezeshwa kwa kupatiwa na Mkurabita vifaa muhimu kwa utekelezaji wa shughuli za urasimishaji ardhi vikiwamo kompyuta moja, kamera moja printa moja, jenereta na GPS 10. “Matokeo ya mafunzo kwa vitendo ni pamoja na mashamba 2,328 kupimwa na hatimiliki za kimila 2,180 kuandaliwa. Kijiji cha Mbondo kina hatimiliki 507, Nahimba 341 na Nakalonji hati 256 zilizochapishwa,” anasema Zambi.

Kwa mujibu wa Zambi, uwezeshaji wa Mkurabita kwa Halmashauri ya Nachingwea pia ulihusisha ukarabati wa masjala ya ardhi ya Wilaya ya Nachingwea na ujenzi wa masjala za vijiji hivyo hadi kufikia hatua ya umaliziaji (asilimia 80). Anasema kutokana na mradi huo, hadi sasa vijiji 104 kati ya 127 vimepima mipaka yake na kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Takwimu kuhusu halmashauri ya Nachingwea zinaonesha kuwa, katika Kijiji cha Mbondo mashamba 1304 yamepimwa na hati 750 zimeandaliwa huku kijijini Nahimba, mashamba 505 yamepimwa na hati 341 zimeandaliwa. katika Kijiji cha Nakalonji, zimeandaliwa hati 256 kati ya mashamba 519 yaliyopmwa. “Kuhusu utoaji wa hatimiliki za kimila, mwaka 2016 ulifanyika uhakiki wa hatimiliki za mashamba yaliyopimwa katika vijiji na hati 950 zilichapishwa, kusajiliwa na kisha kugawiwa kwa wananchi,” anasema Zambi.

Zambi anasema urasimishaji umeongeza thamani ya ardhi za wananchi na kuwa fursa za kutumia ardhi kama dhamana katika sehemu mbalimbali za kiuchumi na kijamii. “Halmashauri imeandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 24 baada ya kuwezeshwa na Mkurabita sambamba na kupima mashamba 251 katika Kijiji cha Namatunu,” anasema. Anasema changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya wamiliki kuuza kiholela mashamba baada ya upimaji na hivyo, kukwamisha utoaji wa hati kutokana na upimaji wa awali.

“Miongoni mwa mikakati ya kuondokana na changamoto hizi ni Mkurabita kutenga fedha za kumalizia ujenzi wa masjala za vijiji hivyo katika Bajeti ya Mwaka 2019/2020 Taarifa zinasema Sh milioni 70, zilitumika kwa ukarabati wa miundombinu ya masjala za ardhi katika vijiji vya mbondo (Sh 24,428,900), Nahimba (21,872,400) na Nakalonji (24,339,900).

Halmashauri ilitoa usafiri wa kubebea vifaa vya jenzi kama mchanga, mawe na nondo kwa thamani ya Sh 6,249,000 huku wananchi wakitoa nguvu kazi kwa kukusanya mchanga na mawe ya ujenzi wa masjala. Wananchi kadhaa katika Kijiji cha Mbondo wanataja mafanikio ya urasimishaji katika vijiji hivyo kuwa ni pamoja na kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi na mipaka ya miliki huku wakiwa na usalama wa miliki ya ardhi zao. Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mbondo, Selemani Swallehe Mkaringa anasema urasimishaji ni zawadi ya Serikali kwa wananchi wakiwamo wanyonge ambao hawakuwahi kuwa na ndoto ya kumiliki ardhi kihalali na kisheria.

Maria Abdalla Makinda anayemiliki shamba pamoja na dada yake, Halima Abdalla Mkinda, pamoja na Nurdin Maulid Mtwana na Zuwena Ahmad Mchenjele, wanasema watatumia hati zao kutafuta mkopo ili kuendeleza kilimo chao cha korosho.

Uchunguzi umebaini kuwa, kama zilivyo hati nyingine ambazo zimekuwa zikikubalika na benki kabla hati za hatimiliki hizi nazo hazijakubaliwa, wasiojua utaratibu wanapopata hati leo, kesho wanakwenda kuomba mkopo benki, bila kuonesha watatumiaje mkopo hata kurejesha vizuri, hao wasipopewa, wanazusha kuwa hati hizi hazikubaliki jamo ambalo siyo sahihi. Ndiyo maana ninasema, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa imesema ukweli kuhusu Mkurabita.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/455dbedaf2e50ae7bf2312da52c3e573.png

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi