loader
Makumbusho, malikale zitumike kiuchumi

Makumbusho, malikale zitumike kiuchumi

FEBRUARI 27 kila mwaka ni siku kubwa kwa watu wa Songea, mkoani Ruvuma kwani ndiyo siku ambayo wakoloni wa Kijerumani waliwanyonga hadi kufa machifu na askari walioshiriki Vita ya Maji Maji vilivyopiganwa kati ya mwaka 1905 - 1907.

Wazee wa jadi, chifu wa Kingoni, askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na viongozi wengine wa serikali, hujumuika katika eneo la Makumbusho ya Maji Maji lililoko mjini Songea kuwakumbuka mashujaa hao ambao hawakukubali kutawaliwa na wakoloni. Siku hiyo huanza kwa maandamano mpaka eneo walililonyongewa mashujaa wa Vita ya Maji Maji.

Gwaride la maombolezo hufanyika na kuweka silaha za jadi katika mnara ambapo askari wa Vita vya Maji Maji walinyongewa wanne wanne kwa zamu mfululizo kwa siku mbili. Baada ya hapo, maandamano hayo yanayoongozwa na wazee wa Kingoni waliovalia mashuka mekundu kuelekea eneo walipozikwa mashujaa hao umbali wa kama mita 300 ambapo kuna uwanja mkubwa uliozungukwa na sanamu za machifu hao. Katikati ya uwanja huo, kuna sanamu kubwa ya askari yaliyebeba silaha mithili ya askari aliye vitani.

Katika sanamu hiyo, huzunguka askari nadhifu wa JWTZ waliovalia sare zenye mabaka mabaka na kitambaa cheusi juu ya mikononi yao walio tayari kwa amri ya kiongozi wao. Kiongozi hutoa amri na wimbo wa heshima kwa mashujaa hupigwa huku watu wengine wote wakiwa wametulia kimya kwa mfano wa mtu anayenyolewa. Baada ya wimbo huo, mizinga miwili ya heshima hupigwa ambayo pamoja na kutangaziwa kuwa itakuwepo, bado inapopigwa watu hushtuka na wengine mwanandamu aliyezaliwa na mwanamke anayapenda maisha yake! Baada ya heshima za kijeshi, ndipo viongozi mbalimbali wakiongozwa na mgeni rasmi hutajwa mmoja baada ya mwingine kwenda kuweka silaha za jadi katika mnara wa kumbukumbu ya mashujaa hao.

Mgeni rasmi huweka ngao na mkuki, mstahiki meya huweka upinde na mshale, kiongozi wa JWTZ huweka sime, chifu wa Kingoni huweka shoka na mzee wa ila huweka rungu. Sala na maombezi kwa ajili ya mashujaa hao kutoka kwa viongozi mbalimbali wa dini hufanyika na mashada ya maua huwekwa katika kaburi la halaiki na viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo.

Ngoma za asili na risala mbalimbali hutolewa kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa. Mtafiti wa makabila mbalimbali Tanzania, Omela Musa, anasema chanzo cha Vita ya Maji Maji ni uonezi wa Wajerumani waliowachapa viboko wananchi na kuwafanyishwa kazi ngumu kwa manufaa ya wakoloni wenyewe. Vile vile, walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi, mazao ya kuzalisha na kuwatumikia wao. Vita vya Maji Maji vilianzia maeneo ya Kilwa kulipokuwa na mtu aitwaye Kinjekitile Ngwale aliyewashawishi watu kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala Tanganyika akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza.

Jina la vita hii limetokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na maji, punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani. Mzee Musa anasema chifu wa Wangoni wakati huo aliyeitwa Nkosi Mputa Gama bin Gwazerapasi, alipopata taarifa kuwa kuna maji ya miujiza huko Kilwa, aliwatuma watu wake kwenda kuyaleta. Maji hayo yalifikishwa makao makuu ya chifu eneo liitwalo Maposeni.

Mratibu wa Kamati ya Wazee wa Mkoa wa Ruvuma, Kassimu Yasini anasema Vita ya Maji Maji mkoani Ruvuma ilianzia eneo la Maposeni katika Makao Makuu ya Chifu Mputa Gama Agosti 21, 1905 baada ya Wajerumani kuchoma kibanda cha Chifu. “Wazee wa Kingoni walikasirika sana baada ya kuona kibanda cha chifu kumechomwa moto hivyo, kuamuru vita dhidi ya Wajerumani ianze,” anasema Yassini. Anaongeza: “Vita vilipiganwa kwa nguvu sana, wakati Wajerumani wakitumia mtutu wa bunduki, Wangoni walitumia silaha zao duni za mishale, mikuki, mapanga na marungu.”

Kwa mujibu wa mzee huyo, japokuwa Wangoni walikuwa na silaha duni, wingi wao uliwasumbua Wajerumani hali iliyowalazimu kuongeza nguvu ili kupambana na Wangoni. Kwa mujibu wa taarifa toka kwa wazee mbalimbali, Chifu Mputa Gama alikuwa na wasaidizi 12 walioitwa Manduna na mmojawapo alikuwa Nduna Songea Mbano. Huyu alisifika na kuaminiwa na chifu kutokana na uhodari wake katika vita. Aliwaongoza Wangoni katika vita hiyo iliyopiganwa tangu mwaka 1905 mpaka 1907 ambapo kutokana na silaha duni walizotumia babu zetu, walishindwa vita.

Mzee Yasini anasema mwisho wa vita hivyo askari wote na machifu walioshiriki vita hivyo walihukumiwa na Wajerumani kunyongwa hadi kufa. Watu 66 walinyongwa katika mnara wa kunyongea na kuzikwa katika kaburi la pamoja lililopo katika Makumbusho ya Maji Maji mjini Songea. “Nduna Songea Mbano aliyekuwa kiongozi wa vita hivyo aliuawa kwa risasi na kukatwa kichwa ambacho kilichuliwa na Wajerumani,” anasema Mzee Yasini.

Kumbukizi ya vita hii hufanyika kila Februari 27. Makumbusho ya Taifa la Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu shughuli hiyo katika mji wa Songea, mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na JWTZ na Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma. Mwaka huu ni maadhimisho ya 112 ambapo pamoja na mambo mengine, mkazo kubwa umewekwa katika kukumbuka uthubutu wa mashujaa hao kutetea haki na uhuru wao. Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizira ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda anasema, maadhimisho ya kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni kwa Mwaka 2019 yanalenga kuenzi uthubutu wa mababu zetu waliopanda mbegu ya uzalendo, utaifa, amani, upendo na mshikamano wa taifa letu.

“Vitu hivi ni urithi kutoka kwa babu zetu na waasisi wa taifa letu,” anasema Profesa Mkenda katika hotuba kuhusu maudhui ya maadhimisho hayo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Liusius Mwenda. Anasema siku hii pia hutumika kuibua na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Ukanda wa Kusini hususan mkoani Ruvuma. Tangu mwaka 2011 tamasha hili limeshirikisha wageni kutoka Malawi, Msumbiji na Zambia ambapo machifu wa makabila ya Wangoni waishio katika nchi hizo.

Mwaka huu wa 2019 wageni watatu kutoka Malawi walijumuika pamoja na wenzao katika kumbukizi hiyo. “Lengo kuu ni kutumia utalii wa malikale katika kuimarisha urafiki na ujirani mwema baina ya nchi yetu na mataifa mengine,” anasema Mkenda. Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla anasema lengo la serikali kuendelea kuyatunza maeneo ya malikale ni kuhakikisha yanatumika kiuchumi na kitaulii badala ya kihistoria pekee. “Hatuna vita vya wakoloni tena hivyo, vita vyetu viwe vya kujikomboa kiuchumi,” anasema Profesa Mabula.

Anasema ushahidi maridhawa kuwa binadamu wa kwanza duniani aliishi Tanzania ni eneo la Olduvai Gorge ambako kuna mabaki ya mwanadamu wa kwanza. Eneo hili licha ya kuwa ni muhimu kwa historia ya nchi yetu ni kivutio cha utalii kwa wageni na wazawa. “Tunatakiwa kuangalia ni kwa namna gani maeneo haya yanaweza kutumika kiutalii hivyo kunufaika kiuchumi,” anasema Mabula. Anatoa mwito kwa wananchi kutembelea maeneo ya makumbusho kwa sababu ni tunu za nchi na maeneo muhimu kwa elimu na utafiti.

Mgeni rasmi katika kumbukizi ya Mashujaa wa Vita ya Maji Maji mwaka 2019 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme aliyeelezea uthubutu wa mashujaa hao katika kutetea nchi. Alisema uthubutu huo unafanana na uthubutu wa Rais John Magufuli katika kujenga uchumi wa Tanzania. “Njia nzuri ya kuendelea kuwaenzi mashujaa hawa ni kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo dhana ya hapa kazi tu ya Rais wetu John Magufuli, anayoitumia kuhimiza kila Mtanzania kufanyakazi kwa bidii, kulinda rasilimali za taifa, kupambana na kuzuia rushwa na dawa za kulevya,” anasema Mndeme.

Anasema Sera ya Malikale inatoa ruhusu kwa sekta binafsi kushiriki kuyamiliki, kuyaendeleza, kuyahifadhi na kuyatumia kama chanzo cha uchumi maeneo ya makumbusho kama haya ya Vita vya Maji Maji na mengineyo. “Natoa mwito kwa Watanzania wote kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuyaendeleza na kuyahifadhi maeneo haya ili kiwe chanzo cha ajira kwa wananchi wote,” anasema mkuu wa mkoa wa Ruvuma. Analipongeza JWTZ kwa kushiriki kumbukizi ya 112 ya Mashujaa wa Vita vya Maji Maji na kufanya gwaride la heshima kwa mashujaa hao. Joyce Mkinga ni Ofisa Uhusiano Mkuu wa Makumbusho ya Taifa

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2213b682865d36e62fc19f2f9e2bc998.png

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Joyce Mkinga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi