loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lindi changamkieni Jukwaa la Biashara

LEO ndio ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wakazi wa Lindi ya kufanyika kwa Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji mkoani humo.

Kwa takribani wiki tatu sasa timu ya waandishi wa habari kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), imekuwa mkoani humo kwa ajili ya maandalizi ya jukwaa hilo ambalo safari hii litafunguliwa rasmi kesho na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

TSN ndio waandaaji wa jukwaa hilo ambalo ni la tisa na majukwaa mengine manane yalishafanyika katika mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Zanzibar, Tanga na Tabora.

Jukwaa hilo huwakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, wakurugenzi wa taasisi nyeti zinazohusiana na uwekezaji na biashara, wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali na wananchi wa kawaida.

Aidha, majukwaa yote huanza na maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali, wafanyabiashara, taasisi na mashirika ya umma na binafsi yanayotoa huduma kwa wananchi.

Ukweli ni kwamba jukwaa hilo ni fursa adhimu kwa mkoa husika kwani pamoja na kuwakutanisha viongozi hao na wafanyabiashara na watu wa kawaida, pia huibua fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa husika kwa lengo la kuvutia wafanyabiashara, lakini pia kuvutia uwekezaji.

Kwa kipindi kifupi ambacho timu ya TSN imekuwepo Lindi kupitia vyombo vyake vya habari kama vile Daily News, HabariLeo, SpotiLeo na Daily News na HabariLeo digital, imeibua na kuzitangaza fursa lukuki za mkoa wa Lindi.

Baadhi ya fursa zilizobainishwa na kutangazwa ni mahitaji makubwa ya uwekezaji katika maeneo ya madini, fukwe, utalii, misitu, elimu, afya, kilimo hasa katika mazao ya korosho, ufuta, mihogo, mbaazi, alizeti, mpunga na mahindi.

Lindi ina ardhi ya kutosha kukaribisha uwekezaji katika nyanja mbalimbali kwani mkoa huo umejipanga katika matumizi ya ardhi ambapo ipo ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makazi, viwanda, kilimo lakini pia yapo maeneo ya misitu pia yanayohitaji uwekezaji.

Kwa hali ilivyo ni wazi kuwa fursa hizo ambazo leo hadi keshokutwa zitajadiliwa kwa kina kupitia jukwaa hilo, zikipata wawekezaji na wafanyabiashara mkoa wa Lindi na wakazi wake kwa ujumla utabadilika kwa kuwa na maendeleo makubwa.

Ni fursa sasa kwa wakazi wa Lindi popote walipo lakini pia watanzania kwa ujumla kutega sikio na kulifuatilia jukwaa hili, kwani linaweza kuwa mkombozi mkubwa wa uchumi kwao, mkoa lakini pia taifa kwa ujumla.

Ni wakati sasa kwa wajasiriamali, waendesha bodaboda, mama ntilie, wenye nyumba za wageni, wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi, maduka makubwa na madogo kushiriki katika jukwaa hilo ili kubaini fursa zaidi wanazoweza kuzitumia na kujiongezea kipato.

Katika jukwaa hilo watakuwepo wataalamu mbalimbali, taasisi kama vile Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Usajili wa Viwanda (Brela) na taasisi za fedha.

Uwepo wa wataalamu hao, viongozi mbalimbali na mawaziri utasaidia mjadala huo kuwa chanya kwa kuwa changamoto zitakazoibuliwa ni wazi kuwa zitapata majibu na hivyo kuwasaidia wananchi moja kwa moja.

Aidha, pia itakua ni fursa ya kipekee kwa wakazi wa Lindi na watanzania kwa ujumla kuongeza zaidi elimu na uelewa katika maeneo mbalimbali ya biashara na uwekezaji yatakayojadiliwa katika jukwaa hilo.

Ikumbukwe kwamba sehemu yeyote yenye biashara na uwekezaji wa kutosha, wakazi wa sehemu hiyo ni wazi kuwa maisha yao hubadilika kwa kuwa kunakuwa na fursa ya ajira, mahitaji ya huduma muhimu kama vile afya, elimu, miundombinu na biashara.

Hivyo basi, ni wakati sasa wa Watanzania hususani wana Lindi kushiriki kikamilifu kuhudhuria jukwaa hilo na kulifuatilia kupitia Shirika la Utangazaji (TBC) na redio ya Mashujaa kwa kuwa litarushwa mubashara.

Lindi ilikuwa kimya, sasa Lindi inaongea na kwa hali ilivyo baada ya jukwaa hilo ni wazi kuwa ule msemo wa watu wa kusini wa Lindi kuchele kwa maana ya Lindi kumekucha utatimia.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Lindi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi