loader
Lindi wampa Samia maazimio 21

Lindi wampa Samia maazimio 21

JUMLA ya maazimio 21 yamepitishwa na kuidhinishwa na Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji mkoani Lindi na kukabidhiwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, kwa ajili ya kuyawasilisha kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Maazimio hayo yametokana na mada na mijadala iliyojadiliwa kwenye jukwaa hilo, lililokuwa na takribani washiriki 350, lililoandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Akiwasilisha maazimio hayo wakati wa kuhitimishwa jukwaa hilo lililofanyika kwa siku tatu mkoani hapa, Katibu Tawala Wilaya ya Liwale, Mbwana Kambangwa alisema maazimio hayo yanahusu mipango na mikakati ambayo mkoa huo umejiwekea ili kuhakikisha kuwa fursa zilizoibuliwa na jukwaa hilo zinatekelezeka.

Alitaja maazimio hayo kuwa ni washiriki wa kongamano hilo kutakiwa watumie maarifa yaliyopatikana kwa ajili ya kuimarisha uwekezaji katika Mkoa wa Lindi.

Alisema maazimio mengine ni mkoa huo, uhakikishe unafuatilia wawekezaji kutoka nje ya nchi Marekani kwa kushirikiana na wadau kutoka nchi hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itengeneze mazingira yatakayowawezesha kupanua wigo wa kukusanya kodi, kwa kuondoa vikwazo na kutoa elimu ya kutosha kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Mengine ni serikali ihakikishe inawaelimisha wananchi na wawekezaji juu ya punguzo la kodi ya mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kwa viwanda vya kuunganisha boti za uvuvi, matrekta ya kilimo kwa miaka mitano ya mwanzo ya uwekezaji.

Pia alisema serikali ihakikishe inawaelimisha wananchi na wawekezaji juu ya punguzo la kodi ya mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 20 kwa viwanda vya ngozi na dawa za binadamu kwa miaka mitano ya mwanzo ya uwekezaji.

“Pia azimio lingine ni serikali iendelee kuimarisha miundombinu wezeshi kama nishati ya umeme, maji na barabara hususani kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji,” alieleza Kambangwa.

Alisema pia jukwaa hilo limeazimia serikali ya mkoa kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali, ziendelee kufanikisha uwekezaji kwa kutengeneza mazingira rafiki, ikiwemo upatikanaji wa ardhi kwa wakati na vyombo vya habari, vikiongozwa na TSN pamoja na wadau wote wa uwekezaji waendelee kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Lindi.

Pamoja na hayo, alisema pia wameazimia Lindi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, uandae mwongozo wa uwekezaji kwa msaada wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) ishirikiane na mkoa katika kuandaa maeneo maalumu ya uwekezaji kwa ajili ya mauzo ya nje na kanda maalumu.

“Wawekezaji wote waliotwaa ardhi na kushindwa kuiendeleza kwa zaidi ya miaka mitano (5) watanyang'anywa na kupewa wawekezaji wengine ambao watakuwa tayari kuwekeza,” alisema Kambangwa.

Maazimio mengine ni pamoja na taasisi za fedha, ziangalie uwezekano wa kupunguza zaidi viwango vya riba kuendana na mahitaji ya mikopo kwa wajasiriamali na wawekezaji wengine.

Pia Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), wapitie upya utaratibu wa wajasiriamali kupata cheti cha ubora (wapunguze urasimu). Aidha, waweke utaratibu wa kuwatembelea wajasiriamali, kufanya ukaguzi na kuwapatia vibali.

Azimio lingine ni serikali ya mkoa kwa kushirikiana na taasisi za fedha kama vile Benki ya TIB Development na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), iandae maandiko ya miradi mbalimbali ya uwekezaji, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wadau wa gesi asilia, waendeleze mkakati wa kuwapatia ujuzi vijana wa Mkoa wa Lindi ili washiriki katika ajira zitakazotokana na uwekezaji wa sekta ya mafuta na gesi.

“Hadi sasa vijana zaidi ya 700 wamepatiwa mafunzo ya aina hiyo kupitia VETA Lindi,” alisisitiza na kuongeza kuwa serikali ya mkoa, ihakikishe wazalishaji wanaelimishwa juu ya umuhimu na taratibu za kufuatwa ili bidhaa zao ziwekwe Barcode zinazotolewa na GS1 kwa sababu inasaidia kutambulisha na kupata taarifa za bidhaa zao kimataifa.

“Serikali ya mkoa itaandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maazimio haya na kusimamia majukumu ya utekelezaji huo ili kufanikisha malengo ya Jukwaa la fursa za biashara na uwekezaji mkoani Lindi,” alisema.

Azimio lingine alilosema limesisitizwa na jukwaa hilo kupitia Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ni Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Watumishi Housing, PSSF na NHC waendeleze haraka viwanja walivyonavyo mkoani Lindi kwa kuweka miradi ya mfano.

“Kama hawa wenzetu wa NSSF wana viwanja 303 na Watumishi Housing 100 na taasisi nyingine, tunaomba waviendeleze vinginevyo tutawanyang'anya na kuwapa wawekezaji wengine,” alisisitiza Zambi.

Zambi alisema jukwaa hilo limefungua fursa adhimu za Mkoa wa Lindi, na kwamba mkoa huo utahakikisha fursa hizo zinafanyiwa kazi kwa manufaa ya wakazi wa Lindi na taifa kwa ujumla.

“Lindi tumefurahi sana, na niseme tu tumenufaika sana na yote yaliyojiri kwenye jukwaa hili, nawaahidi haya yaliyoibuliwa leo (jana) hayataishia hapa, bali tutahakikisha tunatengeneza mkakati wa kuyatekeleza,” alisema.

Dk Mwakyembe alisema amepokea maazimio yote, yaliyowasilishwa kwenye mkutano huo na kuahidi kuyawasilisha kwa Makamu wa Rais, Samia ambapo pia atamuelezea namna jukwaa hilo lilivyofanikiwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1f6f333480ee3f8d0978a9b676b6fda5.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Lindi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi