loader
Urasimishaji wa mashamba utakavyookoa wakulima wa korosho

Urasimishaji wa mashamba utakavyookoa wakulima wa korosho

NIANZE kwa kurejea agizo la hivi karibuni la Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alilotoa wakati akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mifugo na Maji katika kikao kilichofanyika mjini Mtwara.

Aliwaagiza wataalamu wa timu ya Operesheni Korosho, kubandika majina ya wakulima wote waliolipwa fedha za mauzo ya korosho kwenye mbao za matangazo na kiasi kilicholipwa sambamba na benki iliyohusika. Kwamba kwa kuwa hali hiyo haina athari kwa mlipwaji, kufanya hivyo kutaondoa utata na malalamiko ya baadhi ya wakulima waliolipwa na serikali, lakini wanasema hawajalipwa hali ambayo siyo nzuri kwani ni kuisingizia na kuichafua serikali.

Waziri Hasunga anasema: “Nashangaa kila mkulima akiulizwa anasema hajalipwa. Jambo hili siyo sawa. Nadhani wanafanya hivi kukwepa madeni wanayodaiana huko vijijini.” Akaongeza: “Timu ya wataalamu wa Operesheni Korosho ihakikishe majina yote ya wakulima wa korosho waliolipwa yanabandikwa kwenye ofisi za vijiji.” Serikali kupitia Waziri Hasunga inasema mpaka sasa, tani 222,684 za korosho zimekusanywa huku hadi Machi 14, mwaka huu, Sh bilioni 596.9 zilikuwa zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Sh bilioni 723.

Taarifa zinasema serikali imelenga kufikia Machi 31, mwaka huu, wakulima wote wawe wamelipwa fedha zao za korosho kwani tayari uhakiki wao umekamilka kwa kiasi kikubwa. Hasunga akaonesha kushangazwa kwake akisema: “Nashangaa Mkoa wa Mtwara una ‘kangomba’ 10 (wafanyabiashara haramu wa korosho) na mkoa huu ndio wazalishaji wakubwa wa korosho huku Mkoa wa Lindi unaofuatia kwa uzalishaji ukiwa na kangomba ambao wapo zaidi ya 400.”

Kimsingi, katika takriban kipindi hichohicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Jasson Rweikiza na Makamu wake, Mwanne Mchemba ilitembelea Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Mkoani Lindi, Kamati hiyo ilikagua shughuli mbalimbali zikiwamo za urasimishaji zinazofanywa na Mpango wa Kurasimishaja Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) ulio chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu. Katika ziara hiyo, Kamati ya Bunge ilifika kijijini Mbondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea na kuwakabidhi wananchi waliopimiwa mashamba na vipande vya ardhi na maandalizi ya hati za hakimiliki za kimila kukamilika. Rweikiza alikabidhi hati 100 kwa wananchi husika na kutaja faida za urasimishaji.

Mwenyekiti wa Kamati huyo (Rweikiza), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary Mwanjelwa, Mratibu wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe na baadhi ya wanakamati ambao ni wabunge, wanazitaja faida mbalimbali za urasimishaji ardhi na mashamba ukiwamo usalama wa miliki kisheria na fursa ya dhamana ya kupata mikopo katika taasisi za fedha.

Mwanjelwa anasisitiza faida kubwa ya urasimishaji ardhi na mashamba kuwa ni kuondoa migogoro ya ardhi baina ya mtu na mtu, wakulima na wafugaji, kijiji na kijiji. Hali iliyopo inayonifanya niandike makala haya inaonesha kuwa, urasimishaji huu pia unaweza kusaidia kukomesha lawama zinazoweza kutokea baina ya baadhi ya wakulima na vyombo vya serikali vikiwamo vyama vya msingi vya wakulima.

Ndiyo maana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati (Mwanne Mchemba) anatoa mwito kwa wanasiasa kuufanya urasimishaji kuwa agenda ya wanasisasa ili pamoja na faida nyingize za kiuchumi zikiwamo urahisi wa kuaminika na kukopesheka katika taasisi za fedha kama benki ambazo sasa zinapokea hati za hatimiliki za kimila kama dhamana kwa mikopo, pia kuimarisha usalama hata wa miliki kwani urasimishaji unatoa nguvu ya kisheria ya umiliki.

Mintarafu umuhimu wa hati za hatimiliki za kimila, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi anasema: “Hati hizi zinakubalika katika benki kama dhamana kwa ajili ya kupata mkopo, ingawa kuna changamoto kuwa baadhi ya watumishi katika baadhi ya benki, hawazipi umuhimu mkubwa kama hati nyingine jambo ambalo siyo sahihi.” Kuhusu mwenendo wa ulipaji korosho, Zambi anaiambia Kamati ya Bunge mkoani kwake akisema: “… Tumekwishalipa zaidi ya Sh bilioni 180 na wakulima wanaotudai, hawazidi Sh bilioni 10 na baadhi ya wakulima waliobaki, ni wale wenye matatizo.

Mfano, ‘kangomba’ wamebainika majina zaidi ya 500 walionunua mazao nje ya mfumo.” Anaongeza: “Huyu, unashangaa ana korosho, lakini hana shamba… Wakulima safi waliobaki, watalipwa ndani ya muda mfupi ujao…” Ikumbukwe kuwa, Novemba mwaka jana, Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikutana na wanunuzi korosho na kujadili changamoto zilizopo hadi kufikia makubaliano ya wakulima kununua korosho kwa bei isiyopungua Sh 3000 kwa kilo, huku serikali nayo ikikubali kuondoa utitiri wa tozo na vikwazo vilivyoonekana kuwafanya wafanyabiashara kushusha bei na hivyo, kuwaumiza wakulima.

Licha ya nia njema ya serikali, wafanyabiashara walifanya mgomo uliolenga kuwaumiza zaidi wakulima hali iliyomfanya Rais Magufuli kusema: “Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua wakionesha kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo, serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

Katika kikao cha Septemba 28, Rais Magufuli alienda mbali kwa kuwaambia wafanyabiashara hao kuwa serikali yake ipo radhi kuzinunua korosho zote kwa bei inayowafaa wakulima na kuziuza katika masoko ya kimataifa nchini Marekani na Uchina, endapo watataka kuendelea kuwakandamiza wakulima.

Akionesha kusisitiza kilicho moyoni mwake, Rais Magufuli akasema katika sekeseke hilo: “Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho kuwa serikali ipo na itaendelea kuwapigania,… serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo…” Ni kwa mantiki hiyo ninasema, urasimishaji ardhi na mashamba unaweza kutumika kwa manufaa zaidi kiuchumi kwa wakulima wakiwamo wa mikoa inayolima korosho na hivyo, kuwasaidia wao sambamba na Serikali, kuepuka tatizo la walanguzi wa zao hilo wanaowapunja wakulima kupitia mtindo wa kangomba.

Hali hiyoo, ndiyo imeifanya serikali kuamua kufanya uhakiki kuhakikisha kuwa walanguzi (kangomba) ‘wanakoma’ maana huenda hata wamo baadhi ya wanasiasa wanaotumia mawakala ‘kukamua jasho na uchumi’ wa wakulima wa korosho kwa kuwapunja katika manunuzi kisha wakajidai kuwatetea kumbe ‘wanawachekea mchana huku usiku wakiwazomea.’

Naipongeza serikali kwa uamuzi wake kukusanya na kununua korosho kwa bei rafiki na wakulima na pia, kwa kufanya uhakiki ili walanguzi kupitia mtindo wa kangomba, wabainike au wakimbie; wakome. Haiwezekani mtu auze mazao ambayo hakuyalima na wala haoneshi au haijulikani ameyapataje. Watu wa namna hiyo, ndio walanguzi wanaodhulumu wakulama na ndio waliomfanya Rais Magufuli aachukue hatua hizo kuwalinda wakulima kwa maslahi ya taifa. Kadhalika baada ya pongezi za uhakiki, pia niipongeze serikali kwa kuwalipa wakulima ambao korosho zao zilichukuliwa na kubwa zaidi, nipongeze hatua na mchakato wa kuweka hadharani orodha ya waliolipwa korosho; kiasi na benki iliyotumika.

Haihitaji hata elimu ya msingi kujua kuwa, ‘kangomba’ huenda sasa ndio wanapandikiza sumu ya uongo na kuwanasa wasiojijua ambao licha ya kuwa tayari wamelipwa, bado wanatumika kuisingizia serikali kuwa haijawalipa. Urasimishaji ardhi na mashamba katika mikoa ya Mtwara na Lindi inayolima korosho kwa wingi; na hata mikoa mingine, ukifanyika kwa nguvu ya kutosha, utakuwa utetezi madhubuti kwa siku za usoni katika kukabiliana na walanguzi wa zao hilo. Hii ni kusema kuwa, mtu atakapohitajika kuonesha alipotoa mazao husika, ataonesha shamba ambalo lina ushahidi wa hati za hakimiliki za kimila kwa kuwa zinaonesha ukubwa wa eneo, na mahali eneo lilipo sambamba na wabia wote katika umiliki halali wa shamba au eneo hilo.

Hivyo, uuzaji mazao utakuwa rahisi na hata ulipaji kwa wanaostahili utafanyika haraka na kwa ufanisi zaidi, kuliko sasa ambapo mlanguzi anaweza kuona ‘maji shingoni’, akaomba aazimwe shamba la mtu mwingine kama kuna mwanya wa kufanya hivyo ili kuhadaa vyombo husika. Ndiyo maana wakati Zambi anasema urasimishaji mkoani Lindi ulikuwa na changamto ya baadhi ya wamiliki kuuza kiholelea mashamba baada ya upimaji hali iliyokwamisha utoaji hati kwa mujibu wa upimaji wa awali, Mratibu wa Mkurabita (Dk Mgembe) anasema kuuza au kugawa kiholela bila kufuata taratibu za kubadili na kuhamisha umiliki, kunawawezka wote katika htari ya kukosa umiliki.

Dk Mgembe anasema: “Hata katika familia, kama hati ni ya mke na mume; mjue nayo inawaunganisha zaidi maana mkitengana mkawa sio mwili mmoja tena, shamba linakuwa kisheria siyo la yeyote kati yenu, mpaka mfuate taratibu za kubadili au kurekebisha umiliki.” “Hii inawahusu hata wananchi wengine, ukiuza sehemu ya shamba, mwende mkafanye marekebisho vinginevyo, inakuwa vigumu kufanya uhamisho wa miliki.”

Ndiyo maana, kwa umuhimu wake, wananchi na wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi; pamoja na wakulima wa mazao na mikoa mingine nchini, waione haja na nia njema ya serikali kufanya urasimishaji ardhi na mashamba kwani ndio wanufaika wakuu, lakini niseme mikoa ya Mtwara na Lindi, urasimishaji ni kama almasi ichangamkieni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/40142c2da79c155744174e6eace21583.png

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi