loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wabunge ‘wanapojilipua’ wapigakura ndio ‘wanaokufa’

APRILI 2, mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Bunge linafikia hatua hiyo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka kuwasilisha na kusoma bungeni taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji CAG na kumtia hatiani kutokana na kauli yake kuwa, Bunge ni dhaifu.

Uamuzi wa Bunge ulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa, kauli aliyoitoa Assad wakati akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York Desemba, 2018, Marekani kuwa Bunge ni ‘dhaifu’, ililenga kulishushia hadhi na hivyo kulidharau na kulidhalilisha mbele ya umma na dunia.

Kamati hiyo ilimhoji CAG Januari 21, mwaka huu. Siku hiyo, Bunge pia liliridhia mapendekezo ya kamati hiyo ya kumsimamisha Mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee, kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia tarehe ya azimio hilo kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu.

Baada ya wabunge kuchangia mapendekezo ya kamati kuhusu mbunge huyo wa Kawe, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alilihoji Bunge na kupitisha azimio la Mdee kutoshiriki mikutano miwili ya Bunge. Naibu Spika akasema: “Bunge limeazimia kuwa Mdee hatashiriki mkutano huu (wa Bajeti) wa 15 wa Bunge na Mkutano wa 16 utakaofanyika Septemba na Oktoba, 2019.”

Sina mpango wa kujadili mwenendo wa sekeseke baina ya Bunge na CAG Profesa Assad maana najua, ndugu wakikosana chukua jembe ukalime na wakipatana, chukua kapu ukavune. Nasema hivyo nikijua kuwa, hakuna upande uliochelewa kutafakari na kufanya marekebisho yoyote ili ‘kusafisha hali ya hewa.

Kilichonisukuma hadi kuchukua kalamu na kuandika hapa, ni namna ninavyoona kwa makusudi, au kwa bahati mbaya, wananchi wa baadhi ya majimbo ya uchaguzi nchini, wanafanywa yatima kwa makusudi, kutokana na baadhi ya wabunge wao ‘kujilipua’ kwa gharama ya kilio cha wananchi hao. Kujilipua huko kunawafanya wananchi ndio waumie huku wabunge wao waliojilipua wakibaki kuwa na ubunge wao.

Yote hayo yanakuja kwa kuwa wakati wa mjadala kuhusu sakata hilo, Naibu Spika pia aliagiza Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu.

Hili linakuja baada ya Lema kuchangia hoja ya kamati hiyo na kudai Halima Mdee hajatendewa haki kutokana na kamati hiyo kupendekeza Bunge kumsimamisha kuhudhuria vikao viwili vya Bunge kwa kuunga mkono kauli ya Profesa Assad kuwa Bunge ni dhaifu.

Kusema Halima Mdee hajatendewa haki siyo tatizo maana yeyote angeweza kuona hajatendewa haki na akasema, lakini asipate adhabu yoyote, lakini utata unakuja baada ya Lema kudaiwa kutoa kauli ninayoiita kuwa ni kujilipua kama yeye mbunge, kisha ‘wakafa’ wapigakura wake.

Nasema alijilipua kwa kuwa kama ningekuwa mimi ndiye Lema, baada ya kuona Mdee amesema maneno hayo na kupewa adhabu ya kuwa nje ya Bunge kwa mikutano miwili hali itakayowafanya wapigakura wa Kawe wakose uwakilishi wa hoja na kero zao bungeni, ningejitahidi kuchuja maneno ili ujumbe wangu ufike.

Nisingejidanganya kushikilia msimamo ambao unawaponza wapigakura wangu hivyo, badala ya kushiriki jambo lile lile linalosababisha wananchi wa Kawe kukosa uwakilishi kwa kipindi hicho na ndiyo maana ninasema: “Wabunge wanapojilipua, wananchi ndio wanaokufa.” Huwezi kumtetea aliyefanya kosa kwa wewe kufanya kosa lilelile. Bila kutumia ‘ulimi vizuri’ kufikisha ujumbe ili wananchi wa jimbo lake waendelee kufaidi kura na nauli zao kumtuma bungeni, Lema ‘anachafua sakafu kwa nyayo zinazokanyaga tope lile lile.”

Mbunge huyo wa mkoani Arusha anasema: “Alichokisema Mdee naungana naye na ni kweli kuwa Bunge ni dhaifu.” Ndipo Dk Tulia (Naibu Spika) anaagiza Lema ahojiwe na kamati hiyo kuthibitisha kuwa kweli Bunge ni dhaifu, uamuzi unaowafanya wabunge wa upinzani wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CUF kunyanyuka na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Kimsingi hata tabia ya baadhi ya wabunge kususasusa vikao na kutoka nje ya Bunge, ni ugonjwa unaowaumiza wapigakura maana wahenga wanasema: “Kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji.” Kumbukumbu zangu zinaniambia kuwa, hii siyo mara ya kwanza kwa wabunge hawa Halima Mdee na Godbless Lema kufungiwa kuhudhuria vikao vya bunge na hivyo, wapigakura wao kuwa mithili ya yatima kwa kukosa uwakilishi bungeni katika kipindi cha wabunge hao kutumikia adhabu za bunge.

Kimsingi, hii ni kuwatesa Watanzania hao waliopoteza muda na nguvu zao kwenda kwenye kampeni na kupiga kura, lakini inafika mahali wale waliopigiwa kura, wanafanya mambo wanayojua kuwa, yatawafanya wafukuzwe bungeni kutokana na sheria ama kanuni za mhimili huo huru (Bunge). Siasa hizi za kuwatesa wapigakura kwa makusudi ili kutafuta huruma ya mataifa ya nje nadhani ni mufilisi kwa kuwa zinawatesa wapigakura wasio na hatia.

Ninachoamini, upo uwezekano mkubwa wa mbunge awe wa chama tawala, au chama cha ushindani, kuunga mkono au kukosoa jambo kwa lugha na matendo ya busara ambayo ni mfano wa kuigwa hata na wanasiasa chipukizi, au watoto ambao ni viongozi wa kesho na kesho kutwa. Hii ni tofauti na siasa au uwakilishi wa mbwembwe za kutafuta umaarufu kwa gharama nafuu na huruma za mataifa, huku waliokutuma kuwawalikisha wakikosa uwakilishi kwa kuwa huo siyo uzalendo kwa wapigakura na taifa kwa jumla, bali uzandiki.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACTWazalendo, Kabwe Zitto, aliwahi kunukuliwa katika mitandao ya kijamii akikosoa matamshi ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu. Zitto akasema: “Nataka maendeleo ya watu wetu. Uwekezaji kutoka nje na misaada ni sehemu tu ya juhudi. Mwanasiasa anayetaka nchi inyimwe misaada ni muflisi.” Anaongeza, “Misaada kuwa fimbo kwa nchi zetu ni jambo la kishamba sana. Misaada ikikatwa anaumia nani; JPM (Rais John Pombe Magufuli)? Lissu?… Ninapinga ujinga; siasa za kukatiwa misaada ni siasa za kizamani, ushamba na kasumba ya kutawaliwa.”

Zitto anayasema hayo ikidaiwa ni ukosoaji kutokana na matamshi ya Lissu kuyataka mataifa makubwa wahisani, kuikatia Tanzania misaada, eti inakiuka na kuvunja misingi ya demokrasia. Ninalikumbuka hili la Lissu na Zitto kwa sababu lina sura moja ya wabunge wetu kusema au kufanya mambo wakilenga yaoneshe msimamo wao, lakini wasijue kuwa hayo wanayoyafanya hayana tofauti na ukweli kuwa wanawakomoa wananchi wakiwamo wapigakura wao.

Mfano ni hilo la mbunge kutaka mataifa yalinyime misaada taifa lake na watu wake; bila kujua kuwa kufanya hivyo anawakomoa wapigakura na wananchi kwa jumla hali ambayo ni mithili ya kukata tawi la mti ulilokalia. Hili nalo linanikumbusha mwaka 1995 wakati Baba wa Taifa Mwalilimu Julius Nyerere anaanza kumpigia debe Benjamin Mkapa kuwa Rais wa Tanzania katika awamu ya Tatu katika Uwanja wa Sabasaba mjini Tarime.

Katika mkutano huo wa hadhara Nyerere anasema: “Vyama vya siasa bado vichanga, viacheni vikue vipate uzoefu…” Leo ninayaona maneno ya Nyerere bado yanaishi. Kimsingi, siasa za kutafuta kuadhibiwa ili kuonewa huruma ama na wahisani au mataifa ya nje, ni siasa zilizokondeana na zisizo na tija zinazopaswa kuepukwa na hata zile za kususa vikao na kuabudu maandamano. Hizo ni siasa zilizopitwa na wakati katika zama hizi.

Katika kumaliza makala haya niseme tu kuwa, unyenyekevu na kujishusha ni mambo muhimu katika maisha haijalishi ni kwa mkubwa, au mdogo na kwamba, wawakilishi wetu wakiwamo wabunge na madiwani bila kujali vyama wajue kuwa, wanapojilipua, wananchi ndio wanaokufa hivyo, wasijidai ni wajanja wa kukaanga mbuyu, na kuwaachia wenye meno watafune maana kampeni zikifika, watahojiwa kwa maneno na matendo yao.

Hapa kuna fundisho kuwa, kuna wakati mtu hutakiwi kusema; siyo kwa sabubu unaogopa, hujui au huna cha kusema, bali kwa sababu unataka kuepusha yanayoweza kuepukwa maana, hakuna kitu duniani kinachoweza kusemwa au kufanyika wakati wowote, mahali popote na kwa namna yoyote.

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi