loader
Picha

China yasaidia ujenzi wa chuo cha ulinzi wa taifa

SERIKALI ya China kupitia Jeshi la Ukombozi la China, kikosi cha Anga limetoa msaada wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Taifa kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam unaogharimu Shilingi Bilioni 56.

Ujenzi huo wa awamu ya pili ya chuo hicho utakifanya kuwa cha kisasa na miundombinu rafiki na kukiwezsha chuo hicho kudahili zaidi ya wanafunzi 100 kwa wakati mmoja baada ya ule wa awamu ya kwanza uliofanyika 2013 na kumalizika 2015. Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, aliishukuru Serikali ya China kupitia jeshi la ukombozi la watu wa China kwa msaada huo kwani utasaidia kuongeza kozi na idadi kubwa ya wanafunzi.

“Tunashukuru serikali ya China kwa msaada huu wa ujenzi wa awamu ya pili ya majengo ya chuo chetu. Msaada huu utakifanya chuo kuweza kuchukua wanafunzi wengi kwa wakati mmoja pia kuboresha sehemu ya kuishi vifaa vya mafunzo,” alisema Dk Mwinyi Alisema mafunzo yanatolewa katika chuo hicho yanalenga ulinzi wa taifa na kimataifa kwa sasa na baadaye kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kisayansi katika mikakati ya maendeleo ya taifa.

Dk Mwinyi pia alisema mbali na ujenzi wa chuo hicho pia wamejenga kituo maalumu kwa mafunzo maalum ambacho kipo Mapinga Bagamoyo, Pwani na hivi karibuni wataanza ujenzi wa makao makuu ya jeshi mkoani Dodoma eneo la Kikombo. Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, alisema urafiki wa Tanzania ulianza wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa Rais wa Tanzania, Julius Nyerere na Mao Tse Tung na sasa umerejea kwa kasi na kuahidi serikali yao itaendelea kuisaidia Tanzania kulingana na uwezo wao.

“Ninafurahi kualikwa katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo hili ambalo linajengwa na Serikali ya watu wa China kupitia Jeshi la Anga. Urafiki wa Tanzania na China ni wa kihistoria hivyo nikianza kueleza mambo ambayo serikali hizi mbili zimefanya nitachukua muda mrefu. “Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali na hata mafunzo ya ndani kwa jeshi la maji, jeshi la anga na jeshi la nchi kavu ili kufanya jeshi liwe la kisasa na kukidhi malengo ya taifa,” alisema Wang Ke.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Yakubu Mohamed, Ofisa Mwandamizi, Mwelekezi Mambo ya Nje katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Balozi Peter Kallaghe na maofisa mbalimbali wa JWTZ na jeshi la Anga la China ambao ndio wanajenga na kusimamia ujenzi huo.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi