loader
Picha

Maliasili waunda kamati kukabili changamoto utalii

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeunda kamati yenye jukumu la kutatua changamoto zinazoikabilia sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuja na mapendekezo ya kuiendeleza sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na gazeti hili kuhusiana na mikakati ya Wizara katika kuendeleza utalii nchini inayolenga kuvuka lengo la kuingiza watalii milioni mbili ifikapo 2020 na ifikishe watalii zaidi ya milioni tano.

Profesa Mkenda alisema hapa nchini kuna vivutio vingi vya utalii ambavyo vikitumiwa vema vitaitangaza nchi kimataifa na kuiingizia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni huku akifafanua kuwa jukumu la kamati itakuwa ni kuchunguza changamato zinazoikwaza sekta hiyo pamoja na kutoa mapendekezo ya kuiendeleza.

Alisema kuwa kamati hiyo licha ya kuchunguza vivutio vipya vya utalii pia itafuatilia mfumo mzima wa mafunzo kwenye vyuo vya utalii na kuja na mapendekezo ya mtaala bora zaidi wa kufundishia kwenye vyuo hivyo. Aliongeza kuwa kwa kuwa vyuo vya utalii ni msingi mzuri wa kuendeleza utalii hasa ikizingatiwa kuwa wanazalishwa wafanyakazi kwenye sekta hiyo wakiwamo watoa huduma za utalii kwenye kampuni na hoteli za kitalii, hivyo wanapaswa kuandaliwa vema na kumudu soko.

Profesa Mkenda alisema kamati hiyo itashirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kushughulikia namna ya kuwahudumia watalii wanaowasili nchini kwa njia ya maji, kwa maana ya watalii wa majini huku akisisitiza kuwa eneo hilo lina fursa nyingi ambazo Wizara imejipanga kuzitumia vilivyo.

“Mwaka huu Tanzania imepokea watalii 860 waliowasili nchini kwa kutimia usafiri wa maji hii inaashiria kuwa kuna fursa kubwa zaidi na hasa miundombinu ya kuwahudumia ikiboreshwa zaidi wanaweza kuja wengi kwa kuwa tunaweza sasa kuwaalika kwa wingi zaidi,” alisema.

Aliongeza TPA itajenga gati maalum la kuwahudumia watalii hao wa njia ya maji ikiwa ni pamoja na kuwaandalia utaratibu mzuri wa kutoka bandari ya Dar es Salaam na kwenda sehemu mbalimbali kuona vivutio vya utalii kama mambo ya kale, mambo ya kihistoria yanayopatikana Dar es Salaam , Kilwa na Bagamoyo.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi