loader
Picha

NGO zinazotapeli Kibaha kufutwa

MKUU wa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Assumter Mshama amesema amedhamiria kuyafuta mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO) wilayani humo, ambayo yanafanya shughuli kwa kwa utapeli na ubabaishaji.

Pia, amesema atayaandikia barua ya kujieleza yale ambayo yaliitwa kwenye kikao chake, lakini viongozi wake hawakutokea, ambapo kati ya mashirika zaidi ya 100 yaliyofika ni 21 tu.

Mshama alisema hayo kwenye kikao chake na viongozi wa mashirika hayo ili kubadilishana mawazo na kujua changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao. “Kuna baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni ya mifukoni (briefcase), hayana hata ofisi, haya tutayafuta, kwani ni ya kitapeli na hayapaswi kuendelea kuibia wafadhili ambao wanatoa fedha zao kusaidia watu,” alisema Mshama.

Alisema kuwa watatoa taarifa kwa wafadhili wao kuwa mashirika hayo ni ya kitapeli na hayafanyi kazi, kama yanavyojieleza yanapoomba ufadhili. “Hawa walioshindwa kuja lazima waandikiwe barua za kujieleza kwa nini hawakufika kwenye kikao; na nadhani ndio haya tunayoyasema na wakishindwa kujieleza tutawafuta na tutapeleka taarifa kwa msajili wa mashirika haya ili ayaondoe kwenye usajili,” alisema Mshama.

Aliwataka viongozi wa mashirika hayo, kupeleka taarifa zao za utendaji kazi na wawe wanatoa taarifa serikalini za kila robo mwaka. Alisema ataomba wafadhili kabla ya kutoa fedha, waulize juu ya mashirika hayo kwani mengine yako kwa ajili ya maslahi binafsi na si kuleta maendeleo kwa wananchi.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkami Hangaya alisema kuwa alitoa barua ya mwaliko kwa mashirika yote, lakini yaliyohudhuria ni machache na viongozi wa mashirika yasiyohudhuria, hawakutoa sababu za kutofika.

Hangaya alisema mashirika mengine hayana ofisi. Mengine mawasiliano yao hayapatikani, lakini yanapoomba kufanya kazi, yanaonekana kama kweli yako makini, lakini baada ya muda hawaonekani tena.

Mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC), Catherine Mlenga alisema kuwa wao wamekuwa wakifanya kazi zao na kushirikiana na viongozi wa serikali. Alisema wamekuwa wakitoa taarifa serikalini katika ofisi ya ustawi wa jamii na kwa viongozi wa serikali za mitaa na kata, hivyo wao wanafuata taratibu zote.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: John Gagarini, Kibaha

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi