loader
Picha

Simba yapotelea Kaitaba

SIMBA jana ilionja shubiri baada ya kufungwa mabao 2-1 na Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Huo unakuwa mchezo wa kwanza kwa mabingwa hao kupoteza baada ya kushinda mechi 11 mfululizo.

Kwa msimu mzima mpaka jana inapoteza mechi ya pili baada ya ile ya Mbao mwanzoni mwa msimu huu. Mabao ya Kagera jana yalifungwa kipindi cha kwanza na Khasim Hamis na Ramadhan Kapera huku la Simba likifungwa na Emmanuel Okwi kipindi cha pili.

Kagera waliingia kwenye mechi hiyo na kasi na kupata bao la uongozi dakika ya 17 likiwekwa kimiani na Hamis baada ya kupata krosi nzuri ya Kapera na dakika ya 41 Kapera akafunga la pili kwa kichwa. Matokeo hayo ya Kagera yaliwapeleka mapumziko yakiwa hivyo na Simba ilianza kipindi cha pili kwa mabadiliko kwa kuwatoa Haruna Niyonzima na kuingia John Bocco, James Kotei na kuingia Hassan Dilunga.

Mabadiliko hayo yaliwawezesha kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwa Kagera na kupata bao dakika ya 63 lililofungwa na Okwi baada ya kupata pasi nzuri ya Clatous Chama. Simba walitengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha pili lakini hawakuzitumia ipasavyo na kujikuta wakizipoteza. Zana Coulibaly, Okwi, Chama na Bocco walishindwa kutumia nafasi hizo.

Kwa ushindi Kagera inajiondoa kwenye mstari wa kushuka daraja ikifikisha pointi 39 ingawa bado itahitaji kushinda michezo ijayo ili kujiweka pazuri zaidi huku Simba ikiendelea kubakia nafasi ya tatu kwa pointi 60 katika michezo 24. Simba sasa inatarajiwa kutua jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Alliance kabla ya kurejea Dar es Salaam kujiandaa dhidi ya KMC.

MTENDAJI wa Kijiji cha Manchali A, Wilaya ya Chamwino mkoani ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi