Wapendekeza adhabu ya kifo ifutwe, ibaki kifungo cha maisha

VIONGOZI wa dini na wadau wa sheria wamependekeza adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa makosa ya mauaji na uhaini iondolewe na badala yake iwe kifungo cha maisha.

Adhabu ya kifo inapingwa kwa kile kinachodaiwa kuwa hukiuka haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kuwanyima majaji uamuzi wa kuzingatia mambo ya kupunguza na hali ya mtu wakati wa kutoa hukumu.

Wakiwasilisha mapendekezo hayo mbele ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini, walisema kadhabu hiyo inaleta unyanyapaa na kwamba serikali inapaswa kuzingatia maelekezo ya jumuiya za kimataifa iliyotaka kufutwa kwa adhabu ya kifo.

Mwakilishi wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Mchungaji wa Kanisa la Moriah International, Justin Kaleb alisema adhabu ya kifo inayotolewa chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iondolewe na badala yake iwe kifungo cha maisha.

Alisema utekelezaji wa adhabu hiyo umekuwa na changamoto kwa kuwa wapo wafungwa wenye zaidi ya miaka 30 wakisubiri kunyongwa hadi kufa.

Mchungaji Kaleb alisema adhabu ya kifo ni kinyume na maagizo za Mwenyezi Mungu kwani mwenye mamlaka ya mwisho ya kuua ni Mungu na si mwanadamu.

“Sisi kama viongozi wa dini tunasema kuua si halali hata kama mtu ametenda kosa linalostahili adhabu hiyo, mwenye mamlaka ya kutoa uhai ni Mungu tu hivyo wasijiingize katika mamlaka ambayo hawastahili,” alisema Mchungaji Kaleb.

Pia alisema hata kama hakutakuwa na suluhisho la la kosa kwa kusababisha kifo cha mtuhumiwa bali kifungo cha maisha kitamfanya mfungwa kutumikia kwa kufanya kazi mbalimbali. Sababu nyingine iliyotajwa na viongozi hao wa dini ni kwamba adhabu hiyo inamfanya mfungwa kutojishughulisha na kazi yoyote akiwa gerezani na hivyo kusababisha hasara kwa serikali kutokana na kuwahudumia.

“Adhabu hii huwatia hofu wafugwa kwa sababu baada ya hukumu husubiri adhabu yao lakini imekuwa tofauti wanakaa muda mrefu hivyo huwatia hofu na katika hali hiyo wengine wanakufa,” alisema Mchungaji Kaleb.

Wakili Jebra Kambole alisema adhabu ya kifo inakiuka haki ya kuishi na kwamba ni adhabu ya kikatili ambayo imepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Habari Zifananazo

Back to top button