loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vyombo vya habari vyakumbushwa maadili

VYOMBO vya habari na jamii kwa ujumla wameaswa uhuru wa habari usitumiwe kama kichochoro cha baadhi ya watu kutukana na kudhalilisha wengine, wakiwemo viongozi.

Mwito huo ulitolewa bungeni wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyowasililishwa mwishoni mwa wiki na Waziri Harrison Mwakyembe na kupitishwa jana.

Kabla ya wabunge kuidhinisha na kupitishia wizara hiyo bajeti ya Sh bilioni 30.8 kwa mwaka ujao wa fedha, suala la uhuru wa habari lilijadiliwa na wabunge wengi na kisha na Waziri Mwakyembe kutolea hoja ufafanuzi akisisitiza kuwa hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

Miongoni mwa waliozungumzia suala hilo ni Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye katika kufafanua juu ya hoja ya Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) aliyekuwa akituhumu serikali, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikumbusha wabunge kuwa kigezo cha uhuru wa maoni, wao pia wamekuwa wakitukanwa.

“Uhuru wa kutoa maoni si kwamba ukishakuwa mwanasiasa unatukanwa na kusingiziwa na kila mtu. Hivi wewe ukitoa maoni yako ukapinga jambo, ukafafanua jambo utagombana na nani?

“Tuwafundishe vijana namna ya kutoa maoni yao badala ya kutumia uhuru wa habari kama kichochoro cha kutukana na kudhalilisha. Watu wana utamaduni wao na heshima unakuta kitoto kidogo kinatukana.

“Unapotaka kuiambia serikali lazima uiambie kwenye utaratibu fulani. Kuwa kiongozi ndio utukanwe tu... Nawaonea huruma sana wabunge mnatukwanwa sana,” alisema Ndugai na kusisitiza jukumu la malezi kwa watoto watambue namna bora ya kukosoa. Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisisitiza kuwa hakuna nchi isiyokuwa na sheria.

“Huwezi kusimama kuwa mimi ni mwandishi wa habari utukane useme kwa sababu una uhuru wa habari. Hata huko kwa wakubwa (nchi zilizoendelea) hakuna mtu anayeweza kuandika akatukana serikali au viongozi... uhuru una mipaka yake, haiwezekani.”

Akirejelea hoja za baadhi ya wabunge hususani wa upinzani waliotaja magazeti kadhaa ikiwamo Tanzanite kuwa yanaandika habari za uchochezi na uongo, Nkamia aliongeza Tanzania Daima akisema linamilikiwa na mmoja wa wabunge; akasisitiza kuwa kama ni msumemo ukate kote.

Mbunge wa Mlalo, Rashidi Shangazi (CCM) amesema changamoto iliyopo ni hali ya kila Mtanzania kuwa mwanahabari kwa kusambaza chochote kupitia mitandao ya kijamii.

Alishauri pia vyombo vya habari viangaliwe ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau kutengeneza mitaala.

Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM) ambaye alisisitiza kuwa hakuna uhuru usiokuwa na mipaka, alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki kwa uhuru habari. Akihitimisha michango kabla ya bajeti ya wizara yake kupitishwa, Waziri Mwakyembe alisema wabunge 46 wamechangia hotuba yake. Kati yao, 28 walichangia kwa maandishi na 18 kwa kauli.

Katika kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Dk Mwakyembe alisema habari yoyote inayoandikwa na kuchapisha yenye athari ya kuharibu sifa ya mtu ni kashfa hivyo ni haki kwa mtu aliyekashifiwa kwenda mahakamani kudai fidia kwa maumivu aliyosababishiwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia adhabu ambazo hutolewa kwa vyombo vinavyokiuka sheria, Mwakyembe alisema, “Tanzania ikitumia sheria ndio utasikia haki za binadamu”.

Alisema mwaka juzi yalifungiwa magazeti manne ili wamiliki, waandishi na wadau waelewe kuwa ipo sheria. Mwaka jana hakuna gazeti alilolifungia.

Akijibu malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wachangiaji kuhusu gazeti la Tanzanite huku wakinukuu baadhi ya vichwa vya habari vilivyowahi kuchapishwa na gazeti hilo, Dk Mwakyembe alitaja pia kichwa cha gazeti la Tanzania Daima kuwa hakikuwa sawa.

“Naomba nisiwadanganye, mimi sikufurahishwa na hicho kitu. Hili ni suala la maadili. Mimi ni mwandishi wa habari naongea naelewa maadili yamekiukwa.

“Nimeandika barua ya kumuita anieleze alikuwa ana maana gani? Hilo gazeti (Tanzanite) limetoka tuko kwenye Sikukuu za Pasaka. Tumempelekea barua ameipata na naomba muiamini serikali hatuwezi kufurahia uandishi wa serikali usiofuata maadili.”

Awali, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) alilalamika kuwa licha ya sheria kuwapo, haitekelezwi dhidi ya magazeti yasiyofuata maadili jambo ambalo inawezekana yakakwaza watu wakaamua kuchukua hatua.

MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania anayefanya shughuli zake Marekani, Flaviana ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi