loader
Bomani ataka TGU kujifunza kwa Woods

Bomani ataka TGU kujifunza kwa Woods

JAJI mstaafu Mark Bomani amevutwa na jitihada na mafanikio ya karibuni ya mchezaji gofu maarufu Tiger Woods kurejea kwenye makali na kutaka Chama cha Gofu Tanzania (TGU) kuiga kutoka kwake katika kuhakikisha mchezo huo unaendelea kwa kasi.

Bomani, ambaye ni mlezi wa TGU alisema katika taarifa yake Dar es Salaam jana, kwamba anaungana na wadau waliofurahishwa na mafanikio ya Mmarekani Woods ya kutwaa taji lake la 15 la michuano mikubwa baada ya kutwaa Kombe la US Maters lililofanyika August, Marekani hivi karibuni. Woods, ambaye amekumbana na changamoto kadhaa katika mchezo ikiwa pamoja na majeraha, ametwaa taji kubwa tena ikiwa ni miaka 11 tangu aliposhinda mara ya mwisho.

Bomani alisema: “Ushindi wake unanikumbusha kauli ya mlezi wa kwanza wa Chama cha Gofu Kenya (KGU) Mzee Duncan Ndegwa, ambaye aliandika barua miaka kadhaa iliyopita ya kusisimua kwenda Marekani wakati Woods ameandamwa na matatizo mbalimbali akisema, ‘Tiger Woods bila shaka atarejea kwenye kilele chake na hata pengine kufanya makubwa zaidi ya hapo.”

“Na juzi tu, nilisoma nyota wa zamani wa mpira wa kikapu Marekani (NBA), Micheal Jordan, naye akionesha kustaajabu jinsi Woods alivyoweza kurejea kwenye mafanikio huku akionesha haijawahi kutokea katika michezo.” Aliongeza kuwa ni faraja kwamba rekodi anayofukuzia Woods ya mataji makubwa 18 haipo mbali sana, na raha zaidi mwenye hiyo rekodi ni gwiji Jack Nicklaus ambaye mwaka jana alifanya ziara ya kitalii nchini.

Bomani anaongeza kuwa alipata fursa ya kipekee kukutana na Nicklaus na kujadili masuala ya gofu pamoja na baadhi ya wadau wa gofu. “Nikitazama sasa mustakabali wa gofu Tanzania, nichukue fursa hii kusisitiza kwa Chama cha Gofu Tanzania kuongeza nguvu katika kusimamia maendeleo ya gofu. Ujumbe wangu mahsusi ni kwamba tujifunze kutoka kwa Woods, ambaye kabla hata ya kufikia umri wa miaka mitano alikuwa ameonesha kipaji cha hali ya juu.

Amezitaka klabu za gofu kuwapa kipaumbele kikubwa watoto wadogo ili siku moja Tanzania iweze kujivunia kuwa na mchezaji wa kulipwa kama Tiger Woods. “Hili hata katika shindano la Kombe la Jenerali Waitara 2018 katika klabu ya Lugalo Dar es Salaam niligusia. Natambua TGU na klabu kadhaa kama Lugalo wamefanya kazi kubwa kufuta mtazamo kwamba gofu ni mchezo wa matajiri na wageni, sasa gofu inachezwa na watu wote, lakini bado tunahitaji kuongeza kasi kutafuta vipaji na kuviendeleza,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4373fd3f96dba348fe6330c7ca612aaf.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi